sábado, 3 de junio de 2017

TAFAKARI: SHEEREHE YA PENTEKOSTE



Somo: Mdo 2:1-11

Zab: 104:1, 24, 29-30, 31, 34

Somo II: 1Kor 12:3b-7, 12-13

Injili: Yoh 20:19-23

Nukuu:

Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao,” Mdo 2:3

“Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka,” Mdo 2:4

“Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe,” Mdo 2:6

“Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu,” Mdo 2:11

“Wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu,” 1Kor 12:3b

“Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote,” 1Kor 12:4-6

“Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12

“Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi,” Yoh 20:21

“Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu,” Yoh 20:22

“Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:23

TAFAKARI: “Na tutende kadiri ya Roho wa Bwana na si kadri ya mazoea yetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, mazingira yetu, tamaduni zetu, mitazamo yetu, itikadi zetu na utaifa wetu. Pokea Roho Mtakatifu, na uanze safari mpya ya ubatizo katika Roho Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anasherehekea Sikukuu ya Pentekoste. Ni sikukuu ya kuvuviwa kwa Kanisa na wana wake. Pentekoste ni sikukuu ya kuzaliwa Kanisa. Pentekoste kama ilivyo katika mila na desturi ya Kiyahudi, huadhimishwa baada ya majuma saba, yaani siku 49 baada ya jumapili ya Pasaka. Kwa maana nyingine Pentekoste ni siku hamsini tokea tukio kubwa la Ufufuko wa Bwana yetu Yesu Kristo. Masomo yetu yote matatu ya siku ya leo yanalenga tukio hili kubwa baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu. Ni siku ya kufanywa upya vyote katika Yesu Kristu, yaani, Upyausho. Ni siku ya furaha kubwa kwa kila mbatizwa, tunapoalikwa kama wana Kanisa na familia ya Mungu kutenda kadiri ya Roho wa Bwana na si kadiri ya mazoea yetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, mazingira yetu, tamaduni zetu, mitazamo yetu, itikadi zetu na utaifa wetu. Roho Mtakatifu anasukuma na kutuwezesha kuwaza, kusema, na kutenda zaidi ya mipaka yetu ya kibinadamu. Huku ndiko tunapoalikwa kama wana wa Mungu.

Mitazamo hii imeshavunjwa na Roho Mtakatifu ambaye sifa yake moja kuu ni ‘Umoja katika utofauti wetu.’ Kwa hiyo Roho Mtakatifu leo anatualika wote kuanza yote katika yeye-Roho Mtakatifu na kuyatakatifuza yote katika Kristo.

Somo la kwanza linatupa taswira nzima ya maisha ya kijumuiya na namno walivyokuwa wanaishi kwa hofu na sintokujua nyingi. Roho Mtakatifu anavunja ukimya huu na kuwa furaha na ujasiri mkubwa wa kuishi na kuyaneno mambo makuu ya Mungu. Somo la pili linatupa mwangaza wa maana halisi ya maisha ya Mkristo, ikiwa ni pamoja na kuishi kadiri ya Roho wa Bwana tukisaidiana na kutabikiana katika shida na raha. Umuhimu huu wa maisha ya Mkristu huambatana na matumizi mazuri ya karama, utoaji wa huduma, na utendaji. Na mwisho somo la Injili linatufundisha mambo makuu mawili; zawadi kubwa ya ufufuko wa bwana wetu Yesu Kristo ikiwa ni amani ya kweli, na kusimikwa rasmi kwa Sakramenti ya Upatanisho.

Wapendwa wana wa Mungu katika Kristo mtazame mwenzako uliyekaa naye na umshike mkono umwambie mateno haya; “Pokea Roho Mtakatifu, na uanze safari mpya ya ubatizo katika Roho Mtakatifu.” Umoja katika maisha ya kijumuiya, Roho Mtakatifu anavunja sintofahamu zake, hofu, mashaka na kutujaza nguvu mpya na mtazamo mpya na FURAHA ya kweli kama tulivyosikia kutoka somo la matendo ya Mitume. Kila mmoja anapigwa mshangao kwa tukio la ujio wa Roho Mtakatifu. Wasiojua siri hiyo wanaulizana kama Wayahudi walivyofanya, “Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?” Mdo 2:7. Hilo ndilo bomu la pili la FURAHA katika Kanisa ikiwa la kwanza ni Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Jambo hili linanikumbusha familia mbili za jirani ambapo familia moja kulisikika sauti za furaha na wimbo ulisikika kwa lugha ya kiingereza ukisema, “Happy birthday to you.” Familia ya pili ya jirani yake, yaani kwa Mzee Haijalishi, mwanaye Maria alimuuliza baba yake, “kulikoni hapo kwa jirahi muda huu wanafurahi na kuimba happy birthday to you; ni nani huyo wanayemsherekea?” Mzee Haijalishi bila kusita alimjibu mwanaye Maria na kumwambia, “nafikiri huyo atakuwa anaitwa, ‘to you.” Wapendwa katika Kristo leo ni sikukuu kubwa ya “to you” wetu yaani, Roho Mtakatifu. Huu ndio mshangao wanaopigwa wasio fahamu siri hii. Hata leo katika Kanisa bado wapo watu tunaoshangazwa na mkusanyiko wa sala wa Wanakarismatiki. Hatuachi kuwanenea visivyo na kusema hawa ni wapenda kelele na kulia muda wote. Je, tumeenda kusali nao na kuona sababu za kelele zao? Je, yawezekana umati huu wote wa watu ni wendawazimu? Na nani basi kawatia wendawazimu huo?

Tunapozidi kutafakari matendo haya makuu ya Mungu, Mtume Paulo katika somo la pili anatutabanaisha taswira halisi ya maisha ya wale wote waliobatizwa katika ubatizo huu wa Roho Mtakatifu. Wazo kuu la Mtume Paulo ni kututafakarisha uzuri wa umoja katika utofauti wetu. Uzuri na umoja huu katika utofauti unajionyesha katika karama, utoaji wa huduma na utendaji. Umoja ni tunda la Roho Mtakatifu katika maisha ya Kanisa na wana wake. Kwa hiyo, kielelezo cha karama ni Roho Mtakatifu. Kielelezo cha huduma ni Kristo mwenyewe, na kielelezo cha utendaji ni Mungu mwenyewe. Haya yote ni kwaajili ya kufaidiana, (IKor 12:7). Kila mmoja wetu kwa kile alicho si kwa manufaa yake tu, bali ni kwa ajili ya wengine pia. Jambo hili huenda sambamba na maisha halisi ya kila siku. Iwe furaha au mateso kwangu, mwenzangu na jirani yangu vyote vinanihusu kama mwana Kanisa na mbatizwa.

Uhalisia huu wa maisha unanikumbusha hadithi hii. Mzee Fungamali na mkewe Mama Matumizi walikuwa wakulima na wafugaji maarifu sana katika kijiji cha Changamkeni. Kwa muda mrefu walisumbuliwa sana na panya kwani waliharibu sana nafaka walizokuwa wakivuna kama mahindi na ngano. Baada ya kutafakari jambo hili, waliazimia kununua mtego wa pacha. Basi siku ya jumatano kila wiki huwa kuna gulio katika kijiji chao cha Changamkeni. Mzee fungamali alikwenda na kununua mtengo wa panya ikiwa ni pamoja na kipande cha samaki kama chambo.

Akiwa sebuleni Mzee Fungamali aliutoa mtego huo ndani ya mfuko huku panya mmoja akiwa anaangalia kwa makini kinachoendelea kupitia kati ya moja ya nyufa za nyumba ile. Hakika panya yule alijua mtego huo ni kwa ajili yake na familia yake kwa kile walichokuwa wanakifanya. Ila kwa upendo aliokuwanao panya mchana ule ule aliona ni jambo la busara kutoa angalizo kwa wengine kama; kuku, mbuzi, nguruwe, na ng’omba.

Safari ilianza kwa wanafamilia kuku, “jamani, jamani kuna mtego wa panya ndani ya nyumba ya Mzee Fungamali,” panya alisikika akisema. “Hilo halituhusu sisi. Toa uwendawazimu wako hapa,” Kuku walimjibu kwa dharau. Mguu wa pili ulifika katika familia ya mbuzi. “Waheshimiwa mbuzi, jamani kuna mtego wa wanya katika nyumba ya Mzee Fungamali kuweni waangalifu,” panya alisema kwa msisitizo. “Mtengo wa panya, aaaaha! Mtego huo na mbuzi wapi na wapi bwana? Ondoka zako unatupotezea muda hapa!” Mbuzi walijibu kwa kujiamini na kuona ni kituko cha mwaka.

 asi panya hakuchoka. Aliondoka mara ile hadi katika familia ya ng’ombe. “Waheshimiwa wakubwa zangu ninajambo mahususi la kuwaambia. Nyumbani kwa Mzee Fungamali kuna mtego wa panya. Kuweni waangalifu sana,” panya aliyasema hayo kwa msisitizo mkubwa. “Hivi hujatambua kuwa mtego huo ni kwa ajili yako? Tazama miguu yetu, je hako kamtego kanaweza kubana kwato zetu? Tafakari kwa kina,” ng’ombe walisema huku wakimsikitikia panya. Hata hivyo panya hakukata tamaa na badala yake aliimaliza safari yake kwenye familia ya nguruwe. “Wapendwa mnaopendwa na wengi naomba niwape ujumbe huu muhimu. Kwenye nyumba ya Mzee Fungamali kuna mtego wa panya. Hivyo nawaomba muwe waangalifu sana.” Panya aliyasema hayo kwa unyenyekevu mkubwa huku koo likiwa limemkauka kwa kauli mbiu yake ile. “Ebo! Embu tuondolee giza hapa. Kiguru na njia kote huko ni kutuletea ujumbe wa kipuuzi namna hii? Umekosa la kufanya? Nguruwe walijibu kwa majigambo makubwa na uelewa mpana kadri ya uzoefu wao. Basi panya alijirudisha taratibu katika nyumba ile ya Mzee Fungamali na kuwa makini na mtego ule.

Usiku ule kulikuwa na mvua kubwa sana. Hivyo chatu mmoja mkubwa alijipenyeza na kuingia katika nyumba ya Mzee Fungamali kujisitiri kutokana na mafuriko yaliyotokea kwenye shimo lake. Kutokana na harufu ile ya samaki, chatu huyu alitafuta chanzo cha harusu ile. Mwishowe ilisikika sauti ya kufyatuka mtego, pwaaaa!. Panya wote walishtuka na kutaka kujua kulikoni. Mama wa familia pia alisikia sauti ya mfyatuko huo wa mtego. Alijua hakika panya keshanaswa. Basi, Mama mwenye nyumba aliamka na kwenda kutazama mtego. Mara alisikia maumivu kwenye mguu wake wa kushoto. Chatu yule alimng’ata kwani mtego ulimpana mkiani tu. Kelele za Mama wa nyumba zilimwamsha Mzee Fungamali. Mzee Fungamali alipambana na kuweza kumwua chatu yule, ila hali ya mkewe ikiwa mbaya sana. Alimkimbiza mkewe hospitalini usiku ule ule kwa baiskeli. Alipewa huduma ya kwanza na kulazwa. Asubuhi yake, mama Matumizi aliomba aandaliwe supu ya kuku. Basi kuku alichinjwa na supu ilipelekwa hospitalini. Baada ya siku tatu mama akiwa anapelekewa supu ya kuku, hali yake ilibadilika na jioni yake alifariki. Kijiji kizima kilisikitishwa na msiba ule. Kutokana na umaarifu wa familia ile, Mzee Fungamali alilazimika kuandaa chakula cha kutosha kwa kijiji kizima na wageni kutoka nje ya kijiji kile. Hapa kuku, mbuzi, ngombe walichinjwa kuwezesha kitoweo kwa kundi kubwa lile la watu. TUWE WAANGALIFU KUNA MTEGO WA PANYA!

Wapendwa wana wa Mungu, mambo yote yanayomuhusu mwenzangu ni yangu pia na yananihusu licha ya utofauti wa kimaumbile, hali, na nafasi tulizo nazo katika jamii. Huku ndiko kufaidiana katika shida na raha. Karama, huduma, na utendaji vilenge katika maisha ya kila siku katika jamii tunayoishi na hasa kwa wana Kanisa katika kufaidiana. Mtego wa panya jamani!

Somo la Injili linatufundisha mambo makuu mawili; Amani kama tunda kuu na zawadi nzito ya Kristu mfufuka anapowatokea mitume wake na kusema, ‘Amani kwenu.’ Yoh 20:19-20. Jambo la pili ni kuwekwa rasmi kwa Sakramenti ya Upatanisho au Kitubio. Sakramenti hii ni tiba ya majeraha yetu kiroho na kimwili. Ni upendo wa Mungu katika ukengeufu wetu katika kuuishi Upendo na Huruma ya Mungu. Kwetu sisi waamini, Sakramenti ya kitubio ni heshima kubwa kwa kurudishiwa tena hadhi yetu ya kuwa wana wa Mungu baada ya kuasi. Rejea Mwana mpotevu (Lk 15:11-32). Ni daraja ambalo linatuwezesha kupita pamoja bila kujali uzito wa dhambi zetu, kwa sababu Huruma na Neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Muhumili wake ni Kristu mwenyewe katika Padre ambaye ni Kristu mwingine. Ni heshima kubwa kupita katika daraja hili. Kuna usalama zaidi kwa sababu daraja hili halikujengwa kwa mbao, chuma, wala zege bali ni Kristo mwenyewe. Halinepi wala kutikisika. Hatupaswi kuogopa kupita katika daraja hili. Padre ni nani katika Sakramenti hii ya upatanisho?

Wapendwa wana wa Mungu, niwakumbushe tena nafasi ya Padre katika Kanisa, na katika adhimisho hili la Sakramenti ya Upatanisho. Padre ufahamika kwa kile afanyacho. Kwa kinywa chake anaweza kutamka maneno ya Bwana, (Yoh 14:6). Padre ni Mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu, “Kila Padre ni Kristo mwingine” {“Alter Christus”}. Ni mwanadamu kama wanadamu wengine, aliyetwaliwa kati ya watu kwa mambo yamuhusuyo Mungu, “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1-3. Kama Kristo mwingine hakuna mtu anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padre. Lakini Padre ni chumvi na mwanga wa dunia. Kwa hiyo padre hata baada ya upadrisho wake anaendelea kuwa binadamu. Na hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika pamoja na kukata tama.

Kumbe si halali: Watu kukasirika wanapomwona Padre mnyonge kama wao. Kuwadai mapadre kuwa na akili kama malaika. Kutaka upendo wao unyeyushe ugumu wa kila mkosefu au wawe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya maisha.

Padre ni upendo kwa Mungu: palipo na huzuni Padre huleta furaha. Pasipo na haki Padre hutetea haki. Kwa vijana huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali. Padre utii  na uaminifu kwa watu wote. Padre ni moyo wa uwajibikaji na heshima kwa watu. Wanaoteuliwa kuwa mapadri ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa ndugu zao. Na hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki. Padre ni zawadi kwa Mungu ya watu kwa Mungu. Padre hutoa zaidi na hupokea kidogo, zaidi hulipwa chuki na minong’ono. Kwa sadaka yake Padre inabidi apate heshima. Ni mtu anayemwakilisha Kristo. Kama Mt. Fransisko alivyosea, “kama ningekutana na malaika pamoja na Padri, ningeweza kumsalimia kwanza Padre, kwani Malaika ni rafiki wa Mungu na Padri ni Mhudumu wa Mungu.” Malaika hufuata pale Mungu alipo, lakini Mungu ufuata pale padre alipo. Mt. Yohana Maria Viane alisema: “Acha eneo na sehemu yoyote bila Padre kwa miaka ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu wanyama.” Padre kwa Kanisa ni zawadi kubwa kuliko zawadi zote zitolewazo.

Wakristu wenzangu, Sakramenti ya Kitubio ni upatanisho (1Yoh 4:10), uliotukuka kati ya Mungu na mwanadamu. Jamani nani kati yetu asiyependa kupatanishwa na Mungu ikiwa yeye tu ndiye hatma ya kila kitu kwetu? Mbona hatupendi upatanisho huu? Mbona tunafurahia ufundo wa mizoga ya dhambi zetu? Kwa nini hatutaki uturi huu kutoka Sakramenti hii ya Upatanisho? Leo Sakramenti hii ya Upatanisho imekuwa kama kituo cha polisi. Hatuendi kwa hiari yetu bali kwa pingu na ni pale tu tunapokamatwa. Hii siyo taswira ya Sakramenti ya Upatanisho. Tutafakari mfano huu wa upendo katika Sakramenti ya Upatanisho.

Mzee Mchepuko alijipeleka katika saduku la maungamo na mambo yalikuwa kama hivi. “Habari zako Padre,” Mzee Mchepuko alianza kwa salamu hiyo. “Milele amina mwanangu na karibu katika upatanisho na Mungu,” Padre Mapendo alijibu kwa utulivu. Muda ulipita ukitawaliwa na ukimya. “Mbona kimya mwanangu?” Padre Mapendo aliuliza kwa upole. “Sijui nianzeje Padre, ni muda mrefu sijakanyaga mahali hapa,” alijibu Mzee Mchepuko kwa hofu. “Usiwe na hofu wala woga. Anza tu kusema yote kwa moyo wa toba uliyoyatenda kinyume cha Upendo wa Mungu,” Padre Mapendo alimjibu kwa sauti ya upole. Mzee Mchepuko akayasema yote yaliyokuwa moyoni mwake. Padre Mapendo akamwombea na kumalizia kwa maneno haya; “nami kwa niaba ya kanisa nakuondolea dhambi zako kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.” Yoh 20:23. Kisha Padre Mapendo akampa malipizi ya kusali sala ya Baba Yetu. Muda ukapita ukitawaliwa na ukimya. “Mbona kimya mwanagu,” Padre Mapendo alimuuliza kwa upole. “Sikumbuki tena sala hii Padre,” Mzee Mchepuko alijibu kwa unyenyekevu mkubwa. “Sali sala yoyote unayokumbuka mwanangu,” Padre Mapendo alimjibu wa utulivu. Muda tena ulipita na baadaye ilisikika sauti, ‘ngo, ngooo, ngooooo!’ “Ndicho ninachokumbuka katika Kanisa Padre,” Mzee Mchepuko alijibu kwa upole (akimaanisha KENGELE). “Nenda na amani na furaha kwa kusamehewa dhambi zako,” Padre Mapendo alimalizia. “Asante Padre,” Mzee Mchepuko kwa furaha na tabasamu alijibu.

Hitimisho

Wapendwa katika Kristo, pamoja na michepuko yetu (hali ya dhambi) na kusahau kwetu, Mungu hubaki kuwa UPENDO, HURUMA NA MSAMAHA. Jamani kwendeni kupatanishwa naye!

Tumsifu Yesu Kristo!

Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23

Tusali:-Ee Yesu na yangu yote, nijalie fadhila ya unyenyekevu katika kutumia karama na vipaji vyangu vyema na kuvishirikisha kwa wengine pasipo choyo, ili katika hayo wewe uonekane. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario