martes, 13 de junio de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 10 YA MWAKA-I


JUMATANO WIKI YA 10 YA MWAKA-I

Somo 2Kor 3:4-11

Zab: 99:5, 6, 7, 8, 9

Injili: Mt 5:17-19

Nukuu:

“Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,” 2Kor 3:5

Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha,” 2Kor 3:6

Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu,” 2Kor 3:11

Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17

Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:19a

“Bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:19b

TAFAKARI: “Utoshelezo wetu watoka kwa Mungu kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa undani tutafakari nini kitoshelezo cha mwanadamu. Ni vyema kujitazama wenyewe kwanza kabla ya kumtazama mwanadamu na utoshelezo wake kwa ujumla. Je, wajisikia kutosheka kwa hali na namna unavyoishi? Kulijibu swali hili itakupasa kuyachambua mambo haya yafuatayo; Sehemu ya kwanza jaribu kuyapitia mambo yale yote yanayokupa furaha. Ukiwa bado umebaki katika hatua hii ya kwanza kwa hayo mambo yanayokupa furaha, kila moja wapo ya hilo linalokupa furaha lilinganishe na uzima wako wa milele. Jiulize swali hili: Je, kunauhusiano wa moja kwa moja na maisha yako baada ya kifo, yaani umilele wa maisha yako? Kama hakuna uhusiano wa moja kwa moja na uzima wako wa milele, je,  mkwamo huo upo wapi? Kuchukua hatua katika mkwamo huo, yakupasa kujiona kuwa una siku ya leo tu. Hatua hiyo utakayoichukua iwe na uhusiano wa moja kwa moja na uzima wako wa milele.

Sehemu ya pili ya kutafakari utoshelezo wako jaribu kuyapitia mambo yale yote yasiyokupa furaha. Na bado ukiwa katika mambo hayo, ni vema ukajiuliza swali hili; Je, mahangaiko hayo yanautukufu mbele yake ukilinganisha na hali yako ya sasa na  umilele wa maisha yako baada ya kifo? Kama hayana, je, mkwamo wake upo wapi? Wapo wengi leo wanateseka kwa ajili ya kuteseka, na mateso yao hayana utukufu na uhusiano wa moja kwa moja na umilele wao. Mfano; kutamani nyumba nzuri ya ghorofa ya jirani yako na kutokulala usingizi ukiikodolea macho usiku kucha, hakuta kuwezesha kuwa na nyumba kama hiyo kamwe kama  hutojishughulisha na jambo lolote na hufanyi chochote kubadili hali hiyo. Ukweli ni kwamba, hakuna sababu ya kulalamika chumba kina giza wakati unashindwa kuwasha hata kijinga cha moto kuleta hata mwanga kidogo katika chumba kile.

Wapendwa katika Kristo, tunapoyatamani yale yaliyo nje ya uwezo wetu kama wanadamu twaweza kuyapata au kuyafikia kama tumefanya vyema yale yaliyochini ya uwezo wetu kama binadamu. Hapa ndipo ule msemo unapopata maana, yaani “Grace works on nature,”-“Neema hufanya kazi katika uhasili wa mazingira halisi,” na si vinginevyo. Ni kwa kulitambua jambo hili, Mtume Paulo anatoa kauli hii yenye ukomavu wa Imani: “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,” 2Kor 3:5. Hii ndiyo neema ya Mungu inayotuwezesha kutoka pale tulipo na kwenda pale alipo. Utoshelevu huu kutoka kwa Mungu haudondoki tu kama mana kule jangwani, bali kwa kututaka pia tufanye yale yanayotuhusu kama wanadamu. “Aliye kuumba wewe pasipo wewe, hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,” Mt. Augustino wa Hippo.

Je, hali ilikuwaje kabla ya Yesu Kristo na wakati wake? Ni ukweli usiotia shaka kwamba uhusiano kati ya mwanadamu na Muumba wake ulioneka wa mbali sana, na tena wa kutisha. Mungu alionekana kama mtoa adhabu za papo kwa papo, na wakati mwingine kutafsiriwa kama mpanga mtindo fulani wa maisha ambao kwa upande wetu binadamu hata tungejitahidi kwa namna gani tusingeweza kujitoa katika hali hiyo.

Jambo la kushangaza zaidi wakati wa Yesu, Torati ile ambayo ndiyo ilikuwa mstakabali wa Taifa la wana wa Mungu-Waisraeli, ilikwisha chakachuliwa vya kutosha na hivyo Taifa hili lilikuwa linafuata Tafsiri yake tu kwa sehemu kubwa. Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi) iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati. Ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa.

Yesu anasisitiza kuishika na kuiishi Torati kama mafundisho ya kweli ya Mungu na makusudi yake, anasema, "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza. Kwa maana, amini, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yadi moja wala nukta moja ya Torati haitaondoka, hata yote yatimie," Mt 5:17-18.

Ukweli huu wa Torati kama mafundisho na maagizo ya kweli ya Mungu waweza kuusoma pia katika sehemu nyingine za injili kama ifuatavyo;

-Mt 7:12; 12:5; 22:40;

-Lk 2:22; 10:26; 16:16; 24:44

-Yoh 1:17; 1:45; 7:19; 7:49

Yesu ni ukweli na amekuja kusimamia kweli ya Mungu akitambua ukweli huo utatuweka huru. "Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru," Yoh 8:31-32. Ni ukweli huu anaongelea Mtume Paulo ambao utatutosheleza. “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha,” 2Kor 3:6. Andiko hapa analolisema Mt. Paulo ni ule uchakachuaji wa Torati niliosema hapo mwanzo. Yesu Kristo amekuja kutuhuisha na ile kweli iliyokuwa tangu mwanzo, yaani Torati (mafundisho ya kweli ya Mungu na makusudio yake katika kumkomboa mwanadamu).

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, fanya tafiti moyo na uone ni mambo gani yanayokupa utoshelevu wa kweli ndani yako. La sivyo, maisha yako kama mfuasi wa Kristo yatakuwa kama mchezaji ngumu bora anayetupa makonde yake hewani mwanzo hadi mwisho wa ngumi. Je, hapa kuna ushindi? Kama tunataka ushindi, yaani, utoshelevu wa kweli ndani yetu, lazima utoke kwa Mungu, na kupitia kwa Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Kwani, “amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia,” Yoh 3:36

Tumsifu Yesu Kristo!

Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17

Tusali: Ee Yesu Kristo wewe ndiye utoshelevu wetu wa kweli. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario