JUMATATU
WIKI YA 9 YA MWAKA-I
Somo: Tob 1:1a, 2; 2:1-9
Zab: 112:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Mk 12-1-12
Nukuu:
“Lakini jirani zangu walinidhihaki,
wakasema, “Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa
alikimbia, na kumbe! Anazika maiti tena,” Tob 2:8
“Basi
alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho,
akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6
“Lakini
wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa
wetu,” Mk 12:7
“Wakamkamata,
wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8
TAFAKARI: “Upendo wa kweli ni kuwa tayari
kuteseka kwa ajili ya wengine.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tulitafakari
neno hili; “Upendo wa kweli ni kuwa tayari kuteseka kwa ajili ya wengine.”
Ukomavu wa imani yetu unao endana na Ukristo wetu, hupimwa kwa kiwango cha
upendo wetu kwa wenzetu na ule utayari wa kuteseka kwa ajili ya wenzetu.
Utayari huu si ule wa kujianda kwa ajili ya kufanya kitu kizuri ya kuwasaidia
wengine, bali ni kuwa tayari kwa lolote linalotokea na kujitosa kwenye jambo
hilo kwa nguvu zako zote, uwezo wako wote, akili zako zote, na hata muda wako
wote.
Tunaona utayari huu kutoka somo letu la
kwanza, pale ambapo Tobiti anapotapa habari ya mtu kunyongwa na kutupwa sokoni.
Tobiti anapata taarifa hii kupitia mtoto wake ambaye alimtuma kwa nia njema
kwamba aende amtafute mtu masikini wa Taifa lao aje ashiriki naye chakula.
Badala ya mtu masikini, anapata taarifa ya mtu aliyenyongwa hadi kufa na
kutupwa sokoni. Binadamu hueshimiwa kutoka na utu wake, hivyo hata akifariki
maiti yake huifadhiwa kwa heshima. Licha la ukweli huu, Tobiti anaenda mbali
zaidi, na kufanya maiti huyu kuwa sehemu ya msiba wake. Hivyo kwa heshima zote
anamzika na kukubali kuingia unajisi kutokana na upendo huu wa ajabu na
kuwajibika. Majirani zake wanambeza kwa tendo hili, na kusema, “Mtu huyu bado
haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia, na kumbe! Anazika
maiti tena,” Tob 2:8.
Wapendwa wana wa Mungu, si mara moja
tumekutana matukio kama haya, na wakati mwingine na maiti zisizokuwa na ndugu wa karibu. Wapo
kati yetu ambao mara tusikiapo habari kama hizi huguswa na kuwajibika kadiri ya
uwezo wetu. Wapo wengine wanapokutana na matukio kama haya ujisemea mioyoni
mwao, “jambo hili halinihusu, kila mtu na mzigo wake.” Labda nikukumbushe
ukweli wa jambo hili. Hakuna binadamu yeyote aliyejizika mwenyewe. Unaweza
kufanya maandalizi ya awali, mfano; kuchimba kaburi na kulipamba unavyotaka,
kununua sanda, kuchonga jeneza, na mambo mengine katika hatua ya awali ya maandalizi,
ila hutoweza kujibeba na kulifunika kaburini ukiwa maiti. Watu wengine lazima
wakuhifadhi.
Kwa maana nyingine, tatizo lolote lile
linalomkumba binadamu mwenzangu laweza kwa namna hiyo hiyo kunipata mimi
mwenyewe. Hivyo hata siku moja usilipige kisogo tatizo la mwenzako. Fanya
chochote kile unachoweza kukifanya, na mara nyingine saidia mapema kabla mambo
hayajaharibika. Kama ni mgonjwa hangaikia kwa bidii zako zote matibabu yake, na
usingoje akifa ndiyo uonyeshe upendo kwa kujitoa. Tunaona maigizo mengi sana ya
wakristo ambao uthamini sana maiti kuliko uhai wa mtu. Tupo tayari kujitoa sana
kwenye msiba kuliko wakati mtu huyu alipokuwa akiitaji huduma za matibabu. Haya
ni maigizo ya upendo.
Katika somo letu la Injili, Yesu anatoa
simulizi la historia nzima ya wokovu wetu, na kufunua mioyoni kwa Wayahudi hitimisho la historia
hiyo kwa kifo chake ambacho wao Wayahudi watakitekeleza kutokana na mioyo yao
kuwa migumu kwa kutokupokea upendo wa Mungu na kuuishi.
Mungu katika kumkomboa mwanadamu
alitumia njia mbalimbali na watu mbalimbali hatua kwa hatua. Lakini hapa
mwishoni amemtuma mwanaye mpendwa Yesu Kristo akiamini kuwa huyu tutamsikiliza.
“ Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye
akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6 Kinyume chake, tumejitwalia na
tunaendelea kujitwalia mambo ya Mungu mwenyewe na kutaka kuwa wamiliki wa kitu
ambacho kwa uhalisia na silika yetu hatuwezi.
Njia iliyorahisi mara nyingi kwa mtu
mwovu ni kuchukua nafasi ya yule anayemwona kuwa ni kipingamizi chake. Kristo
kwa upande wa Wayahudi na sisi sote tusiopenda kupokea na kuuishi upendo wa
Mungu ni wapinzani wa ukweli huu. Kuchukua nafasi ya mpenzani wako katika maani
niliyoisema ni pamoja na kumfifisha mpinzani wako, ambako mara nyingi huchukua
mwelekea wa kukatisha uhali wa mtu yule. Kwa maana, “ile
tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa
mauti,” Yak 1:15. Hivyo Yesu Kristo anatabiri kifo chake na kuwaambia Wayahudi
kwa mfano ule wa wakulima, “wale wakulima
wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk
12:7. Nao wakafanya kadiri ya dhamiri zao mbovu. Ila pamoja na hila hizi za
kibinadamu na za uovu, hatuwezi kufifisha upendo wa Mungu. Kristo ndiye mpango
mzima wa Mungu. Hivyo, Kristo ni, “Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa
jiwe kuu la pembeni,” Mk 12:10.
Wapendwa
wana wa Mungu, kamwe usimtendee binadamu mwenzako ubaya. Binadamu huyu ambaye
hujua familia yake, ukoo wake, kabila lake, na taifa lake anachapa ya Mungu
ndani yake. Ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kutomtendea wema na haki ni
kutomtendea Mungu wema na haki hiyo ambayo ni yake, na kwa kufanya hivyo uku
ukijiita mwana shirika fulani la kitume, wana kikundi fulani parokia, mwana
maombi, nk, ubakia kuwa upendo wa maigizo ambao mara nyingi wewe na mimi ni
waigizaji maarufu.
Tumsifu
Yesu Krito!
Tusali: Ee Yesu
tujalie upendo wa kweli, na tuwe tayari kteseka kwa akjili ya wengine. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario