ALHAMISI WIKI 9 YA MWAKA-I
Somo: Tob
6:10-11a; 7:1, 9-17; 8:4-10
Zab:
128:1-2, 3, 4-5
Injili:
12:28b-34
Nukuu:
“Inuka, dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.”
Tob 8:4b
“nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho
yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako
kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:30-31
“Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu,” Mk 12:34b
TAFAKARI: “Wewe hu
mbali na ufalme wa Mungu”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo tujikumbushe katekesi yetu, na hasa nini sababu ya kuumbwa
kwetu? Bila kukukosea, tumeumbwa ili tumjue, tumpende, tumtumikie, na mwisho
turudi kwake mbinguni. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuumbwa kwetu. Kwa maana
nyingine hatupo katika ulimwengu huu kwa bahati mbaya. Tupo katika ulimengu huu
kwa malengo: Tumjue aliyetuumba na makusudi yake, tumpende kwa sababu katupenda
yeye kwanza, tumtumikie kwa mapaji yote aliyotujalia, na baada ya kuyafanya haya
yote kwa uaminifu turudi kwake mbinguni kwenye umilele.
Wapendwa
twaweza kuyafanya hayo yote kama ndani mwetu tunayo hofu ya Mungu. Hofu ya
Mungu ndani mwetu ni ule msukumo wa kuyafanya yale yote yampendezayo Mungu.
Tunayafanya haya si kama watumwa kwa hofu ya Mtwana, bali kwa sababu tu wana na
warithi wa ufalme wa Mungu. Twawajibika kuyafanya haya kutokana na wadhifa wetu
mbele ya Mungu-waana wa Mungu. Hofu hii ya Mungu ndicho kinachoyasukuma maisha
mapya ya ndoa kati ya Tobiti na Sara. Tobiti anamuwasa mke wake, na kusema, “Inuka, dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.”
Tob 8:4b
Injili
ya leo inatupa sababu kuu mbili za kuumbwa kwetu. Sababu hizi ni amri, kwa
maana yake hakuna uchaguzi wa kufanya au kutokufanya. Yatupasa kulitenda hilo
na kulifanya kuwa ndiyo tabia yetu kama wana wa Mungu. Yesu anapoulizwa ni amri
ipi iliyokuwa kubwa kulizo zote, anajibu kwa ufupi uliyobeba mstakabadhi mzima
wa maisha ya mwanadamu. Mjumuhisho huo wa pamoja ni hivi: “nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho
yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako
kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:30-31.
Sehemu ya kwanza ya amri hii imebeba lengo la kuumbwa kwetu
na kuwa hapa duniani, yaani “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa
roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.” Sehemu ya pili
inatutaka tutambue, na kuwapenda jirani zetu. Je, jirani yako ni nani? Jirani
kwa mwono halisi wa Imani yetu kama Wakristo, imevuka mipaka ile ya
kimazingira. Kwa maana hiyo jirani yangu ni yeyote yule mwenye uitaji (rejea
Msamaria mwema Lk 10:33).
Je, hali ndivyo ilivyo kwenye mazingira yetu ya leo Tanzania?
Leo inapotokea ajali badala ya kupata msaada ndiyo kwanza wanakumalizia kabisa.
Tumefikia mahali hata tunazivua maiti nguo. Huku ni kukosa kabisa hofu ya Mungu
na kuwa mbali na ufalme wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nawe
mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili
zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na
ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako,” Mk 12:30.
Tusali: Ee Yesu tuwezeshe
kuwafikia wote tunaokutana nao. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario