IJUMAA WIKI YA 9 YA MWAKA-I
Somo: Tob 11:5-17
Zab: 145: 1-2, 6b-7, 8-9a, 9bc-10
Injili: Mk 12:35-37
Nukuu:
“Tobiti
akamkumbatia Tobia na kulia kwa furaha: “Ninakuona mwanangu! Wewe ni mwanga wa
macho yangu!” Kisha akasema,“ Atukuzwe Mungu! Litukuzwe jina lake milele!
Watukuzwe malaika wake wote watakatifu. Yeye aliniletea mateso haya lakini sasa amenionea huruma,
na naweza kumwona mwanangu Tobia!”” Tob 11:11c-15.
“Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Bwana
alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako
Kuwa chini ya miguu yako,” Mk 12:36
TAFAKARI: “Yote yawezekana
kwa Mungu, mwamini”
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, baada ya mateso ya muda
mrefu ya kupofuka kwake Tobiti, Mungu
kupitia malaika wake Rafaeli, anaponywa upofu wake. Mungu aliye yote katika
yote, huwatumia watu tunaoishi nao kufikisha hazma yake kwetu, na hasa wale
wanaomtegemea na kumwamini. Wakati mwingine masharti ya uponyaji yaweza kuwa
njia za kawaida kabisa ambazo kwayo hutupa mtihani mwingine kuyasadiki mambo
makuu hayo ya Mungu. Kwa maana nyingine, Mungu utumia vile alivyoviumba kwa
kuponyesha vile vilivyodhaifu. Upofu wa Tobiti unaponywa kwa nyongo ya samaki.
(Rejea pia simulizi la Jemedari Naaman 2Fal 5:1-14)
Majaribu katika maisha licha ya kukuza imani yetu, utujengea
ustahimilivu. Ustahimilivu huu ni maandalizi ya kutumika vyema baada ya
kulishinda jaribu hilo. Ni kufundwa vyema ili kuwa mkufunzi mzuri kwa wale
watakao patwa na tatizo mfanano kama lako. Kumbe wakati mwingine hatupaswi kulalamika
tu kusikokuwa na maana na kukata tamaa. Kuyashinda majaribu ni kuvumilia katika
Imani thabiti hadi mwisho. “Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye
atakayeokoka,” Mt 10:22b.
Uvumilivu katika majaribu tukiwa na Imani thabiti ndiyo njia
pekee ya kushinda tukitumaini pia mkono wa Mungu. Bila shaka uvumilivu huu
katika Imani ya kweli ndiyo jibu la uponyaji wa upofu aliokuwa nao Tobiti. “Tobiti
akamkumbatia Tobia na kulia kwa furaha: “Ninakuona mwanangu! Wewe ni mwanga wa
macho yangu!” Kisha akasema,“Atukuzwe Mungu! Litukuzwe jina lake milele!
Watukuzwe malaika wake wote watakatifu. Yeye aliniletea mateso haya lakini sasa amenionea huruma,
na naweza kumwona mwanangu Tobia!” Tob 11:11c-15. Mara zote
tuyashindapo majaribu yetu sifa na shukrani tumrudishie Mungu aliye yote katika
yote.
Injili
yetu ya leo, Yesu anaondoa mashaka ya waandishi
juu ya Mamlaka aliyokuwa nayo. Yesu anajibu kama ifuatavyo, na kadiri ya
utabiri ulivyo juu yake. “Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Bwana
alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako
Kuwa chini ya miguu yako,” Mk 12:36. Mamlaka ya Yesu na uhasilia wake yaliwekwa
wazi siku ile aliyojeuka sura mlimani akiwa na wanafunzi wake: Petro, na
Yakobo, na Yohana nduguye. Mambo yalikuwa hivi, “Alipokuwa katika
kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika
lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye;
msikieni yeye,” Mt 17:5. Hapa tunaona uthibitisho wa Yesu kuwa ni mwana wa
Mungu, si kwa kujitamkia Yeye, bali Mungu mwenyewe. Jambo la pili tunafunuliwa
njia sahihi ya kufuata katika nyakati zote za maisha yetu hapa duniani. Yesu
Kristo ni mwana mpendwa wa Baba aliyependezwa naye na ni huyu tu twapaswa
kumsikiliza.
Ni
katika uthibitisho huo wa Yesu unaompa mamlaka ya kutamka maneno haya: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa
Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ndugu yangu nikueleweje unapoyaamini
matunguri na kuyapa kipao mbele katika mafanikio yako? Shetani aweza
kukupumbaza kwa muda mfupi tu na kukuinua kwa mbwembwe kwa muda mfupi tu, kwa
sababu hana umilele. Ila anguko lake ni kubwa sana na kishindo chake usikika
pande zote. Hii ni Imani ile aliyoifananisha Yesu ya yule mtu asikiaye maneno
yake na kutokuyafanya, ambaye Yesu anamfananisha na “mtu mpumbavu (Azaniye
anajua kumbe hajui), aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha,
mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko
lake likawa kubwa.” Mt 7:26-27. Ndugu yangu usisahau kwamba, “THE BLOOD OF
JESUS IS THE MASTER KEY.” Ndugu yangu, yote yanawezekana kwa Mungu, mwamini.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho,
ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22b.
Tusali: Ee Yesu nijalie
uvumilivu katika majaribu yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario