jumamosi
wiki ya 7 ya pasaka
Somo: Mdo 28:16-20,
30-31
Zab: 11:4, 5, 7
Injili: Yoh 21:20-25
Nukuu:
“Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi
wakutane, hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno
kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu,
nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu,” Mdo 28:17
“Basi
kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana
nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli,” Mdo 28:20
“Akakaa
muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga,
akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu,
na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na
mtu,” Mdo 28:30-31
“Yesu
akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate
mimi,” Yoh 21:22
“Kuna na mambo mengi
aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu
usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa,” Yoh 21:25
TAFAKARI:
“Na tuenende katika wema na kutenda mema hata pale tunapokatishwa tamaa; mti wa
matunda ndio urushiwao mawe.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo kadiri ya msomo yetu, napenda niwaalike nyote kwa pamoja
tulitafakari neno hili, “Na tuenende katika wema na kutenda mema hata pale
tunapokatishwa tamaa; mti wa matunda ndio urushiwao mawe.” Ni hali ya
kibinadamu na silika yake kulipa kisasi pale anapofanyiwa ndivyo sivyo. Kwa
upande mwingine si jambo la kawaida kwa yule aliyempokea Kristo kuwa Bwana na
mwokozi wa maisha yake kuyafanya hayo yasiyopendeza machoni mwa Mungu.
Tunayofanyiwa leo kinyume cha utashi wetu na yasiyo haki kabisa, Kristo
alishafanyiwa tena kwa kiwango cha juu kabisa, na kisicho fikirika kwa uwezo
wetu kama wanadamu. Tunapopatwa na sintofahamu kama hizi katika maisha tusiache
kusonga mbele kwa kutenda mema. Kristo mara zote awe ndiye kielelezo na sababu
ya kusonga mbele kwa yale mema yanayopigwa mawe.
Mtume Paulo ambaye kwa
fitina nyingi za Wayahudi, mema yake yote aliyoyafanya mbele zao, yanapigwa
mawe. Ni ukweli usiotia shaka kabisa hakuna arushaye mawe kwenye mti usio na
matunda. Mtume Paulo kwa kubambikiziwa kesi zisizona kweli, aliamua kukata
rufaha kwa dola ya Kirume ili haki itendeke. Hapa lazima tuelewa ukweli huu;
Mtume Paulo hafanyi jambo hili kwa kujitetea, bali kuwasaidia watesi wake
watambue makosa yao na kutenda mema. Hata katika hali hii ya mateso na mahangaiko,
Mtume Paulo anazidi kutoa somo kwa watesi wake. “Ikawa
baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika
akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno
lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali
nimefungwa, tokea Yerusalemu,” Mdo 28:17. Ndugu yangu, Je! katika hali hii
unaweza kutoa ushududa wa Furaha kwa watesi wako na ukabaki kuwa tumaini kwa
wale waliochini yako?
Mtume
Paulo anayo furaha ya ndani na matumaini makubwa katika mateso yake hayo.
Tunaliona jambo hili anapoyasema maneno haya kwa matumaini makubwa. “Basi kwa
ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa
kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli,” Mdo 28:20. Mtume Paulo
anamatumaini makubwa katika ukombozi wa Taifa lake licha ya uasi wao kwa yule
mwenye haki, yaani, Yesu Kristo. Mara baada ya kufika Roma, Mtume Paulo hakuona
walalamikaji wake, wala kushtakiwa kwa lolote. Hata katika hali hii ya uonevu,
Mtume Paulo hakatishwi tamaa kulihubiri neno la Mungu. Hivyo, “Akakaa muda wa
miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu
wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri
habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa
ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu,” Mdo 28:30-31. Ndugu yangu, kila mmoja wetu
kwa nyakati tofauti kesha umizwa na kwa maumivu hayo yamemjengea jeraha kubwa
sana moyoni.
Kwa
kumtazama Mtume Paulo, hakuna sababu ya kutembea na kovu hilo. Usijiwekee ukuta
mbele ya matumaini yako. Vunja ukuta huo na uwe huru mwili na roho. Yawezekana
kwa kipindi hiki unachojizibia kuona mbele mwanga wa Kristo, watesi wako hawana
habari nawe tena. Muda wa kufanya mabadiliko ni huu unaoishi leo na sasa. Jana
ishapita na hakuna tena fursa ya kuiishi. Kesho ni matazamio, na uwezekano wake
yategemea leo na sasa yako. Ndugu yangu, watesi wa Mtume Paulo hawana habari
naye tena kwani kesha waacha Jerusalemu. Furaha yao kwa sasa ni kutouona uwepo
wa Mtume Paulo ambaye alikuwa mwiba kwao. Je, wanaweza kutuliza ukumu ya Mungu
kwa matendo yao yasiyo haki?
Yesu
Kristo anatupa ujasiri wa kuishi kwa kumfuata Yeye tu, na kutoa mashaka yote
tunayokutana nayo katika maisha. Ni katika Kristo tunabaki na uzima wetu. Yesu
Kristo alizua mtafaruku mkubwa kwa Mitume wake aliposema kati yao mmoja wao
hataonja mauti. Hivyo hisia za Mitume zilimwendea Mtume Yohane kwa sababu Yesu
alimpenda sana. Hakika Yesu hakumaanisha kwamba Mtume Yohane hatoonyo mauti,
bali alimaanisha yeyote atakaye mfuata kwa uaminifu atakuwa na uzima ndani
yake. “Yesu
akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate
mimi,” Yoh 21:22. Ndugu yangu, mfuate Kristo kila siku, na kuwa tayari
kujifunza kutoka kwake kila siku. Kufuzu kwa somo (UPENDO) atufundishalo Kristo
kila siku ni kuwa wakamilifu kama Baba yake wa Mbinguni alivyo mkamilifu.
Ukamilifu huu ndiyo kile cheo kitupasacho kama wafuasi wake Kristo, yaani,
Utakatifu.
Hivyo ndugu zangu, yapo
mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa Kristo. Haya tunayoshirikishana kila siku,
ni kukusaidia tu nawe uweze kujijengea tabia ya kuyatafakari makuu ya Kristo
ndani ya maisha yako kila siku. Anza kwa kujihubiria mwenyewe, na ujumbe huo
utakaoupata washirikishe na wengine. Kristo anavyoongea ndani yako, anataka pia
upeleke ujumbe huo kwa wengine, na kutufanya sisi kuwa habari njema ya wokovu
kwa wote. Hivyo basi, “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo
yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu
vitakavyoandikwa,” Yoh 21:25. Ndugu yangu, anza kuyatafakari hayo machache kwa
kuyatazama maisha yako kwa hayo machache, na Mungu atakufunulia makubwa zaidi kila
siku. Wewe si bahati mbaya leo na sasa.
Tumsifu Yesu Krito!
“Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu
akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi,” Yoh 21:22
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nifunulie siri ya mateso yangu, na nijaze furaha ninapoyatazama. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario