SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU MWAKA-A
Somo
I: Kut 34:4b-6, 8-9
Dan: 3:52, 53, 54, 55, 56 (52b)
Somo
II: 2 Cor 13:11-14
Injili:
Yoh 3:16-18
Nukuu:
“Bwana akapita mbele
yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si
mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli,” Kut 34:6
“Akasema, Ikiwa sasa
nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni
watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe
urithi wako,” Kut 34:9
“Kwa maana jinsi hii
Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16
“Amwaminiye yeye
hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la
Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18
“Hatimaye, ndugu,
kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa
upendo na amani atakuwa pamoja nanyi,” 2Kor 13:11
“Neema ya Bwana Yesu
Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote,”
2Kor 13:14
TAFAKARI:
Tu ndani ya Neema ya Bwana Yesu Kristo, pendo la Mungu, na ushirika wa Roho
Mtakatifu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha sherehe ya Utatu Mtakatifu, ambao ni Mungu mmoja,
nafsi tatu; Nafsi tatu Mungu mmoja. Ni Utatu Mtakatifu na Umoja usiogawanyika.
Nazo ni Mungu Baba (Muumbaji), Mungu Mwana (Mkombozi), na Upendo wa Mungu Baba
na Mwana, yaani, Roho Mtakatifu. Nafsi hizi tatu zinaonekana katika utendaji
licha ya kwamba katika utendaji huo wa nafsi moja hautenganishi utendaji wa
nafsi nyingine mbili. Kwa mantiki hii, alipo Mungu Baba yupo pia Mungu mwana na
Roho Mtakatifu. Na ndivyo iliyo kwa Mungu mwana (Mungu Baba na Roho Mtakatifu),
Roho Mtakatifu (Mungu Baba na Mungu Mwana) tokeo la upendo wa Mungu Baba na
Mwana.
Kwa mtiririko huu
katika utendaji ambao unatuwezesha kupata mwanga katika fumbo hili Takatifu,
tunaona katika somo letu la kwanza utendaji wa Mungu Baba, yaani, sifa na
utukufu wake. Ni “… Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi
wa hasira, mwingi wa rehema na kweli,” Kut 34:6. Ukweli huu ujajifunua katika
historia nzima ya uumbaji na wokovu wa mwanadamu. Licha ya mwanadamu kukengeuka
hapa na pale, Mungu hakuacha kuwa Mungu, yaani, mwingi wa rehema na upendo usio
na kipimo. “…maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi
yetu, ukatutwae tuwe urithi wako,” Kut 34:9.
Ni katika safari hii ya wokovu wa
mwanadamu twaona utendaji wa nafsi hii ya pili, yaani, Mungu Mwana. Kristo Yesu
ndiye mwokozi. Hatuwezi kusimama katika kweli ndani ya Kristo kama hatumwamini
Kristo. Na hatuwezi kumwamini Kristo kama tunamuishi Kristo wa Historia. Yesu
Kristo katika maisha yetu na ufuasi wetu kwake ni Kristo aliye hai. Ni kristo
tunayekutana naye kila siku ya maisha yetu. Ni Kristo tunayekutana naye katika
mateso yetu na furaha yetu. Mateso na furaha kwa Mkristo yanamaana tu pale
Kristo anapokuwa kielelezo cha mambo yote. Na hii ndiyo sababu ya Mungu kumtoa
Mwanaye katika historia nzima ya wokovu wetu. “Kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila
mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16.
Wapendwa wana wa Mungu,
Imani yetu juu ya Mwana wa Mungu ndiyo hukumu yetu. “Amwaminiye yeye
hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la
Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18. Kuamini huku si kwa yale tu tuyapendayo
kuyaona na kuyasikia katika maisha yetu, bali ni kuamini hata yale ambaye yapo
juu ya uwezo wetu na mara nyingine hatuyaoni kwa uwezo wetu wa kibinadamu. Ni
kuamini pia yote yawezekana kwa njia yake na kwa uwezo wake. Huku ndiko
kuliamini jina pekee la Mwana wa Mungu. Jina hili lina mamlaka juu ya umilele
wako na mimi. Kuamini huku huendana na kutenda kweli kadiri ya imani juu ya
Kristo, Maandiko Matakatifu, Kanisa na Mapokea yake. Huwezi kuamini mtu fulani
na kutenda kinyume cha imani iliyojenga juu ya mtu yule. Tunapofanya kinyume na
imani ile ni wazi kwamba hatujui tunachoamini. Ni sawa na kuvaa miwani ya giza
kuelekea usipokujua ili hali unaitaji mwanga. “Bali yeye aitendaye kweli huja
kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,”
Yoh 3:21.
Roho Mtakatifu ambaye
ndiye upendo wa Mungu Baba na Mwana, utendaji wake ni kuyatakatifuza yote
yaliyoumbwa na kukombolewa. Nafsi hii, yaani, Roho huyu Mtakatifu kati ya kazi
zake kubwa ni Umoja, mshikamano, na amani. Ndugu, “…nieni mamoja, mkae katika
amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.” 2Kor 13:11. Hivyo
salama yetu ipo ndani ya fumba zima hili yaani, Utatu Mtakatifu. Hivyo kama
asemavyo Mtume Paulo, “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na
ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote,” 2Kor 13:14. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Amwaminiye yeye hahukumiwi;
asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa
Mungu,” Yoh 3:18
Tusali:-Ewe
fumbo la ajabu na uzuri wake, tujazwe neema, na upendo ndani yake. Usifiwe
Utatu Mtakatifu, na Umoja usiogawanyika.
No hay comentarios:
Publicar un comentario