martes, 13 de junio de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 10 YA MWAKA-1


ALHAMISI WIKI YA 10 YA MWAKA-I

Somo: 2 Kor 3:15-4:1, 3-6

Zab: 85:8ab-9, 10-11, 12-13

Injili: Mt 5:20-26

Nukuu:

“Basi ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru,” 2Kor 3:17

“Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu,” 2Kor 4:5

Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20

“Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23

Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25

TAFAKARI: “Patana na ndugu yako uwapo pamoja naye njiani.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni jambo la kawaida kuona ndugu wanagombana na mwisho wa siku wanaweka kando tofauti zao na kuwa kitu kimoja. Hapa sina maana ya kuchochea ugomvi nikijua kunakupatana, la hasha! Ninachosema ni kwamba ikitokea ndugu mmepishana kauli si jambo jema mkaendelea kuzibeba tofauti zenu. Ukweli ni kwamba hata kama umekosewa katika tofauti zenu, hakuna mshindi katika ugomvi huo kila mmoja akibaki na tofauti zake. Ushindi wa kweli na wa roho ni kuchukua hatua na kutafuta upatanisho hata kama wewe ndiwe uliyekosewa haki.

Ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, usikubali hata mara moja kumbeba yeyote katika moyo wako hasa kwa sintofahamu zilizotokana na ugomvi wenu. Kwa kukubali kuishi kwa mtindo huo ni sawa na kuuza uhuru wako na kujifungia katika chumba kidogo sana na kushindwa kutoka ilihali funguo za chumba hicho unazo mwenyewe. Usijitengenezee gereza lako mwenyewe pasipo sababu. Roho wa Mungu uliyepewa bure na kufanya makazi ndani yako unamtesa na hapo hapo unakosa neema. Toka kwenye kifungo hicho na uwe huru, na hapo Roho wa Bwana atakuwa nawe na kukupatia wingi wa neema zake. Ndugu yangu, “alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru,” 2Kor 3:17.

Wapo wengi kati yetu huwa wanajisifu kwa kutoshiriki sakramenti kwa kumkomesha ndugu yake au jirani yake aliyemkosea. Utamsikia anasema kwa kujivuna, “nina mwaka mmoja na nuru si pokei Ekaristi Takatifu kwa kumkomesha kwa sababu sina muda wa kupoteza kwa kuongea naye.” Je, jambo hilo kwako ni habari njema? Ndugu yangu, huko ndiko kujihubiria mwenyewe habari za kuzimu. Kwa nini unajijengea jehenamu yako mwenyewe, tena kwa kupenda? Mtume Paulo anasema, “Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu,” 2Kor 4:5. Yafanye maisha yako kuwa habari njema ya wokovu kila mahali uendapo na kuishi na watu. Yafanye maisha yako kuwa barua ya kusomwa na watu ili kwa kupitia kwako wamwone Kristo. “Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama,” 2Kor 3:2-3.

Ndugu yangu, wapo wengi pia kati yetu ni mabingwa sana wa sura mbili mbili. Nachotaka kusema ni kwamba, wapo tunaoshiriki nao katika jumuiya ndogondogo, Kanisani, hata maisha yetu utawani ambao muda wote umebeba zigo kubwa la chuki, visasi, hasira, wivu, majivuno, na yale yote yanayofanana na haya na yasiyompendeza Mungu. Licha ya zigo hilo kuulemea Moyo, hatupo tayari kuliweka chini. Kukiwa kwenye sehemu za Ibadi huwa tunaliacha zigo hili mlangoni, na mara baada ya Ibada zigo hili tunalikimbilia na kujitwisha na mara kunaondoka nalo. Tupo tayari kulibeba zigo hili nyakati zote za majira ya mwaka, na ya Vipindi vyote vya Liturjia vya Mama Kanisa. Leo Yesu anatupa angalizo: “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20. Mbele za watu na jumuiya tunazoishi twajionyesha sisi ni wema na hatuna tatizo na mtu, na wakati mwingine twa tamani hata kwenda mbinguni kwa miguu yetu tukithibitisha utakatifu wetu machoni pa watu.

Wapendwa wana wa Mungu, ukitaka sala yako, na maombi yako yapate kibali mbele ya Mungu, jipatanishe wewe mwenyewe, wewe na uliyekosana naye, na pia wewe na Mungu. Hivyo “basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23. Wengi na hasa wale tuliokosewa hupenda kuyarefusha mambo sana, na wakati mwingine tungependa tunyunyuziwe ubani kwa cheteso cha dhahabu ili tuwe tayari kwa kuyaongelea yale yaliyotutatiza.

Jambo la muhumu kupita yote kama umekosana na ndugu yako au ye yote yule, patana naye mngali injiani. Maana yake nini? Kupatana na ndugu yako mngali njiani ni kufanya juu chini kupatana na ndugu yako angali yu hai. Wengi tumeshuhudia watu hawapendi kupatana na kuishia kuapizana pasipo sababu. Wapo wengine hata baada ya kuzidiwa wakiwa kitandani karibu ya kufa wanapoomba upatanisho na ndugu yake kunakuwa na mkwamo bila mwitikio wowote na mwisho mtu huyo hufariki katika hali ya majonzi makubwa. Hivi unajisikiaje ndugu yako kufa akikuomba upatane naye nawe kwa kiburi chako hukusikia na hatimaye ndugu yako anafariki? Ndugu yangu, “Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25. Je, kwa kutokupatana na ndugu yako angali hai, utajibu nini mbele ya Kadhi-Mungu mwisho wa siku?

Tumsifu Yesu Kristo!

Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20

Tusali:-Ee Yesu uliyempatanishi wetu na Mungu Baba, tujalie moyo wa kusemehe na kusamehewa. Amina

 

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 10 YA MWAKA-I


JUMATANO WIKI YA 10 YA MWAKA-I

Somo 2Kor 3:4-11

Zab: 99:5, 6, 7, 8, 9

Injili: Mt 5:17-19

Nukuu:

“Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,” 2Kor 3:5

Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha,” 2Kor 3:6

Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu,” 2Kor 3:11

Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17

Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:19a

“Bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:19b

TAFAKARI: “Utoshelezo wetu watoka kwa Mungu kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa undani tutafakari nini kitoshelezo cha mwanadamu. Ni vyema kujitazama wenyewe kwanza kabla ya kumtazama mwanadamu na utoshelezo wake kwa ujumla. Je, wajisikia kutosheka kwa hali na namna unavyoishi? Kulijibu swali hili itakupasa kuyachambua mambo haya yafuatayo; Sehemu ya kwanza jaribu kuyapitia mambo yale yote yanayokupa furaha. Ukiwa bado umebaki katika hatua hii ya kwanza kwa hayo mambo yanayokupa furaha, kila moja wapo ya hilo linalokupa furaha lilinganishe na uzima wako wa milele. Jiulize swali hili: Je, kunauhusiano wa moja kwa moja na maisha yako baada ya kifo, yaani umilele wa maisha yako? Kama hakuna uhusiano wa moja kwa moja na uzima wako wa milele, je,  mkwamo huo upo wapi? Kuchukua hatua katika mkwamo huo, yakupasa kujiona kuwa una siku ya leo tu. Hatua hiyo utakayoichukua iwe na uhusiano wa moja kwa moja na uzima wako wa milele.

Sehemu ya pili ya kutafakari utoshelezo wako jaribu kuyapitia mambo yale yote yasiyokupa furaha. Na bado ukiwa katika mambo hayo, ni vema ukajiuliza swali hili; Je, mahangaiko hayo yanautukufu mbele yake ukilinganisha na hali yako ya sasa na  umilele wa maisha yako baada ya kifo? Kama hayana, je, mkwamo wake upo wapi? Wapo wengi leo wanateseka kwa ajili ya kuteseka, na mateso yao hayana utukufu na uhusiano wa moja kwa moja na umilele wao. Mfano; kutamani nyumba nzuri ya ghorofa ya jirani yako na kutokulala usingizi ukiikodolea macho usiku kucha, hakuta kuwezesha kuwa na nyumba kama hiyo kamwe kama  hutojishughulisha na jambo lolote na hufanyi chochote kubadili hali hiyo. Ukweli ni kwamba, hakuna sababu ya kulalamika chumba kina giza wakati unashindwa kuwasha hata kijinga cha moto kuleta hata mwanga kidogo katika chumba kile.

Wapendwa katika Kristo, tunapoyatamani yale yaliyo nje ya uwezo wetu kama wanadamu twaweza kuyapata au kuyafikia kama tumefanya vyema yale yaliyochini ya uwezo wetu kama binadamu. Hapa ndipo ule msemo unapopata maana, yaani “Grace works on nature,”-“Neema hufanya kazi katika uhasili wa mazingira halisi,” na si vinginevyo. Ni kwa kulitambua jambo hili, Mtume Paulo anatoa kauli hii yenye ukomavu wa Imani: “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,” 2Kor 3:5. Hii ndiyo neema ya Mungu inayotuwezesha kutoka pale tulipo na kwenda pale alipo. Utoshelevu huu kutoka kwa Mungu haudondoki tu kama mana kule jangwani, bali kwa kututaka pia tufanye yale yanayotuhusu kama wanadamu. “Aliye kuumba wewe pasipo wewe, hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,” Mt. Augustino wa Hippo.

Je, hali ilikuwaje kabla ya Yesu Kristo na wakati wake? Ni ukweli usiotia shaka kwamba uhusiano kati ya mwanadamu na Muumba wake ulioneka wa mbali sana, na tena wa kutisha. Mungu alionekana kama mtoa adhabu za papo kwa papo, na wakati mwingine kutafsiriwa kama mpanga mtindo fulani wa maisha ambao kwa upande wetu binadamu hata tungejitahidi kwa namna gani tusingeweza kujitoa katika hali hiyo.

Jambo la kushangaza zaidi wakati wa Yesu, Torati ile ambayo ndiyo ilikuwa mstakabali wa Taifa la wana wa Mungu-Waisraeli, ilikwisha chakachuliwa vya kutosha na hivyo Taifa hili lilikuwa linafuata Tafsiri yake tu kwa sehemu kubwa. Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi) iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati. Ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa.

Yesu anasisitiza kuishika na kuiishi Torati kama mafundisho ya kweli ya Mungu na makusudi yake, anasema, "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza. Kwa maana, amini, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yadi moja wala nukta moja ya Torati haitaondoka, hata yote yatimie," Mt 5:17-18.

Ukweli huu wa Torati kama mafundisho na maagizo ya kweli ya Mungu waweza kuusoma pia katika sehemu nyingine za injili kama ifuatavyo;

-Mt 7:12; 12:5; 22:40;

-Lk 2:22; 10:26; 16:16; 24:44

-Yoh 1:17; 1:45; 7:19; 7:49

Yesu ni ukweli na amekuja kusimamia kweli ya Mungu akitambua ukweli huo utatuweka huru. "Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru," Yoh 8:31-32. Ni ukweli huu anaongelea Mtume Paulo ambao utatutosheleza. “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha,” 2Kor 3:6. Andiko hapa analolisema Mt. Paulo ni ule uchakachuaji wa Torati niliosema hapo mwanzo. Yesu Kristo amekuja kutuhuisha na ile kweli iliyokuwa tangu mwanzo, yaani Torati (mafundisho ya kweli ya Mungu na makusudio yake katika kumkomboa mwanadamu).

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, fanya tafiti moyo na uone ni mambo gani yanayokupa utoshelevu wa kweli ndani yako. La sivyo, maisha yako kama mfuasi wa Kristo yatakuwa kama mchezaji ngumu bora anayetupa makonde yake hewani mwanzo hadi mwisho wa ngumi. Je, hapa kuna ushindi? Kama tunataka ushindi, yaani, utoshelevu wa kweli ndani yetu, lazima utoke kwa Mungu, na kupitia kwa Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Kwani, “amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia,” Yoh 3:36

Tumsifu Yesu Kristo!

Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17

Tusali: Ee Yesu Kristo wewe ndiye utoshelevu wetu wa kweli. Amina

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 10 YA MWAKA-I


jumanne wiki ya 10 ya mwaka-I

Somo: 2Kor 1:18-22

Zab: 119:129, 130, 131, 132, 133, 135

Injili: Mt 5:13-16

Nukuu:

Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi,” 2Kor 1:20

Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16

TAFAKARI: “Ninyi ni chumvu ya dunia, na nuru ya ulimwengu: matendo yenu yamtukuze Baba yenu aliye Mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, swala ya imani halina mbadala, yaani kubadilika badilika kama kinyonga. Kwa maana nyingine ni heri kuwa moto au baridi kuliko kuwa viguvugu. Hatumwendei Mungu kwa hali ya kusitasita. Hivyo kujitoa kwa Mungu asilimia tisini na tano haitoshi na hiyo siyo imani ya kweli. Hatumwendei Mungu katika hali ya mashaka huku tukitamka kwa vinywa vyetu “Mungu ni mweza wa vyote.” Basi niwaombe nyote tusafiri pamoja katika neno hili; “Ninyi ni chumvu ya dunia, na nuru ya ulimwengu: matendo yenu yamtukuze Baba yenu aliye Mbinguni.” Ndugu yangu waamini jambo hili?

Mtume Paulo anaelezea Imani ya kweli ni kusimama katika NDIYO itokayo ndani yako. Bila shaka wote tunamfahamu vizuri “chura.” Nina swala moja kwako, Je, unapomtazama chura kasimama au kachuchumaa? Usicheke! Fanya utafiti unipe jibu. Kwa upande wangu hadi leo sielewi pozi la chura ni “mwamko/kusimama” au “mchuchumao/kuchuchumaa.” Hatupaswi kupata ugumu wa kimtazamo na kiimani kama tuupatao kwenye pozi la chura. Hivyo imani yetu yapaswa kuwa NDIYO ya herufi kubwa. “Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi,” 2Kor 1:20. Kama tunataka Mungu atukuzwe kupitia sisi, twapaswa kusimama imara na kuamini kile tunachokisimamia.

Kati yetu tupo ambao ni mabingwa wa kuhama Kanisa moja na kwenda lingine kama walivyo wachezaji wa mpira maarufu ulimwenguni. Tunapoishi Imani yetu hatuna lengo la kumfurahisha mtu fulani au watu fulani. Lengo ni kumtukuza Mungu, na tendo hilo libakie kuwa shuhuda kwa wengine. Mshangao huu na ushuhuda huu ndiyo unaotuelekeza kumtangaza mtu kuwa kwenye heri au Mtakatifu. Ukilenga kumpendezesha mtu, au kundi la watu, utaambulia huzuni na masikitiko kwa sababu yale yote yatupayo furaha ya leo na sasa hayana umilele. Ipo siku yatachuja au kupitwa na wakati.

John Masifa alikuwa mchezaji mzuri sana wa mpira wa mikono. Kwa kupitia kwake, timu yake ya chuo ilipata vikombe vingi sana, na hivyo kulipamba jengo lile la utawala la Chuo kwa tunzo hizo. Hivyo John Masifa aliweka nia ya dhati kabisa mara baada ya kumaliza masomo yake angependa kurudi chuoni pale awe mkufunzi.

Kwa vile Mungu si Edgar, yote yaliwezekana na akarudi Chuoni pale baada ya miaka mitano kama Mkufunzi na mkuu wa chuo. Lakini jambo la kusikitisha hakuviona vile vikombe katika jengo lile la utawala. Hivyo alianza kuvitafuta.

Siku mmoja akiwa anatafuta kipande cha mbao katika moja ya stoo za zamani aliona pipa kumbwa lililosheheni kila aina ya uchafu pembezoni kwa ukuta. Pipa hili lilimvutia, na hivyo alikwenda na kuona kilichoko ndani yake. “Ha! Kumbe vikombe vyote na zile picha zangu vimetupwa huku?” John Masifa alisema kwa masikitiko.

Ndugu yangu, kwa uhakika Imani yetu msingi wake haujengwi kwa yale tu yatufurahishayo moyo kwa wakati fulani katika maisha. Mambo hayo hayana umilele kwa yenyewe. Mwanafalsafa Plato anatusaidia katika jambo hili. Plato anasema yote haya tunayoyaona na hata kuyafanya ni kivuli tu cha uhalisia wa kitu kile kilichopo katika ulimwengu wa mafaa-“good.” Je, kwa nini sana unapoteza muda wako wote na kuweka roho yako kwenye uvuli wa vitu?

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu anatupa mpango mzima wa thamani yetu mbele ya Mungu. Sisi tu chumvi ya dunia, na nuru ya ulimwengu. Je, nini maana ya maneno haya? Bila shaka tu chumvi ya ulimwengu kimtindo wa maisha, namna ya kuishi na wenzetu katika jamii. Yatupasa kuchanganyika na watu kwa matendo yetu mema ili tuwe kikolezo kama ilivyo kazi ya chumvi. Pamoja na matumizi mengi ya chumvi, chumvu hutumika kuhifadhi vyakula visiharibike, kukoleza na kuleta ladha ya chakula, na chumvi pia utumika kuyeyusha barafu. Basi kuchanganyika huku katika jamii kwa matendo yetu mema mfano wa chumvi, yaani kuhifadhi tunu njema za jamii/maadili na kuruhusu uwepo wa Mungu kama hofu yetu. Kama chumvu, tuwe kikolezo cha upendo pasipo na upendo, furaha pasipo na furana, haki pasipo na haki, na uwajibikaji palipo na uzembe. Mwisho kama chumvi, yatupasa kuyeyusha barafu ya chuki na visasi katika jamii, kuyeyusha maovu wanayofanyiwa wazee, walemavu wa ngozi na wanyonge wasio na watetezi.

Wapendwa tusisahau sisi pia ni nuru ya ulimwengu. Kana nuru maisha yetu ya lenge katika maadili mema. Tutambulike mbele ya jamii tunayoishi kwa maadili mema na kupitia kwetu kama barua zinazosomwa, tuwe kielelezo cha wengine kuona nuru hiyo, kuifuata, na kubadilika. “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16. Taifa letu leo linaangamia kwa mmomonyoko wa maadili. Kumbe haitoshi tu kusema, bali mabadiliko haya yaanzie kwangu mwenyewe.

Tanzania yetu ya leo inanitia hofu kubwa sana. Ni jana tu mtu kashitakiwa na kuhukumiwa kwa kosa la wizi wa mali ya umma kwa uthibitisho wa kutosha. Mtu huyo huyo jana usiku kasafishwa kosa lake na wezi wenzake waliovalia ngozi ya kondoo, na leo asubuhi mtu huyo anaomba ridhaa yetu tumkabidi mali ile aliyotuibia jana. Tunashawishika kwa ubwabwa wa maharage na soda ya Pepsi na kuuza uhuru wetu na watoto wetu. Hakika Tanzania kama ni mwili basi saratani imeshakuwa “cronic.” Tuyafungue macho na mioyo yetu kuuona ukweli huu.

Wapendwa katika Kristo, si lengo langu kuongelea siasa kisiasa, bali ninaongelea siasa kama sehemu muhimu ya maisha kijamii ambapo mimi na wewe tunaoufanya mwili wa Kristo, yaani Kanisa ni sehemu ya jamii hiyo. Ni kosa kubwa kwa Mkristo kusema siasa haimuhusu. Au tusichanganye siasa na dini. Kwa kukana ukweli huu ni kutenda siasa. Leo katika Kanisa moja ya mambo muhimu katika masomo ya “fundamental Theology,” ni kuhusu “Political Theology.” Huwezi kumtenganisha binadamu na jamii yake anayoishi. Kufanya hivyo ni kuishi katika ndoto za kugushi mchana kweupeeee! Embu tujikumbushe ile sala ya Bwana wetu Yesu Kristo, “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli,” Yoh 17:11, 15-17. Je, sala hii ya Yesu inasema nini juu ya maisha yako kijamii?

Ndugu yangu, bado tupo ulimwenguni, na inatupasa kuufanya ulimwengu huu kuwa sehemu salama ya kuishi kila mmoja wetu bila kujali itikadi za vyama na wafuasi wake. Kama Watanzania jukumu la kuilinda amani si kwa kundi fulani la watu waliojihesabia haki ya kuongoza milele, bali ni jukumu la kila mmoja wetu. Mambo yatakapo haribika hakuna atakayekutambua wewe kwa dhehebu lako. Kuilinda Amani ni kufanya tendo la siasa kwa sababu linagusa jamii na sisi wote si visiwa wala milima, bali ni sehemu ya jamii hiyo.

Tusifu Yesu Kristo!

Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16

Tusali: Ee Yesu uliye njia, kweli na uzima, tufanye chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Amina

 

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 10 YA MWAKA-I


 
JUMATATU WIKI YA 10 YA MWAKA-I
Somo: 2Kor 1:1-7
Zab: 34:2-3, 4-5, 6-7, 8-9
Injili: Mt 5:1-12
Nukuu:
“Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu,” 2Kor 1:3-4
“Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo,” 2Kor 1:5
“Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja,” 2Kor 1:7
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3
TAFAKARI: “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.
Wapendwa wana wa Mungu, kila kazi au taaluma fulani hapa duniani ina maadili yake ambayo huendana na taaluma ile. Mfano: Kama wewe ni tabibu wa afya ya binadamu jamii inategemea uwe na maadili ya taaluma yako hiyo, na kutokana na uwanja wako huo, jamii inategemea kwa uhakika wote uwe mtetezi wa uhai. Kadhalika nasi kama Wakristo, wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo, yatupasa pasipo shaka kuyaisha maadili yanayoendana na Imani yetu. Maadili hayo hatakama yangekuwa na uzuri gani, na faida gani katika kuyaishi, yanaupande wake wa pili, yaani, mapaswa yake. Kuishi ukweli huo kutakudai sana kujitoa sadaka ili dhima yake ikamilika na kuonekana.
Sehemu hii ya pili, yaani, sadaka itupasayo kuitoa kwa kuyaishi maadili hayo kama wafuasi wa Kristo, ndiyo Mtume Paulo anayoizungumzia katika somo hili la kwanza, mwanzoni mwa waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho. Kwa vile Bwana wetu Yesu Kristo aliona inafaa na kumpendeza Baba wa Mbinguni kupitia njia ya mateso ili mimi na wewe tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi, ni kwa namna hiyo hiyo tunaalikwa kuyapokea mateso yetu kwa furaha ndani na katika Kristo kwa sababu ni katika Yesu Kristo mateso hayo hupata maana. Kwa mantiki hii, “Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu,” 2Kor 1:3-4. Hivyo ndani na katika Kristo mateso hutufariji na kuwa sababu ya furaha yetu.
Mtazamo huu wa Kiimani tunapoyakabili mateso yetu, hautushawishi kufikia hitimisho la mateso hayo kwa nguvu zetu wenyewe. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa mabaji yake saba aliyotukirimia na anayozidi kutukirimia Roho Mtakatifu yanatusaidia kuyakabili yale yatuzungukayo. Hata hivyo hatuwezi kukwepa ukweli huu kwamba yote huwa hivyo na kufanyika hivyo kwa huruama na matakwa yake Mungu kwetu. Hapa ndipo twaweza kuona maana ya mateso na kile kinachotokana na mateso yetu ndani na katika Kristo-UTAKATIFU. Hivyo tumaini letu katika mateso ni hili: “Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo,” 2Kor 1:5. Kwa mantiki hii ni kosa kubwa la kiimani kukata tamaa kama tunamwamini Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, kama wewe ni mdau wa mateso ndani na katika Kristo, yakupasa kuwa FARAJA kwa wale wote wenye mateso, na hasa yale yasiyo na majibu ya moja kwa moja na ya kueleweka. Wewe uijuaye siri hii ya teso lenye uhusiano wake na teso la Kristo, ndiye unayechukua nafasi ya Kristo katika tendo hili la kuwafariji wengine wenye mateso. Hivyo, “Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja,” 2Kor 1:7. Ninaamini pasipo shaka kwamba mateso yetu ndani na katika Kristo yanasababu yake katika wokovu wako/wangu.
Injili yetu ya leo inatuelezea sehemu ya kwanza ya sababu ya kile tulicho na tupasacho kukiishi. Hiki siyo kitu kingine bali ni maadali ya kile tunachopaswa kukiishi kama wafuasi wake Kristo. Maadili haya kwa maneno mengine ni zile HERI ZA MUNGU. Tuelewe kwamba tumeumbwa ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho turudi kwake mbinguni. Kuyafanya haya kwa ukamilifu wake kunatutaka kuyaishi maadili hayo, yaani hizi heri za Mungu kwa uaminifu.
Wapendwa katika Kristo, heri hii ya kwanza, yaani, “HERI WALIO MASIKINI WA ROHO,” “MAANA UFALME WA MBINGUNI NI WAO,” ndio msingi wa heri nyingine zote. Pasipo kuwa na umaskini wa roho, yaani kuwa na nafasi ya kutosha ya Mungu ndani yako, huwezi kuziishi kikamilifu heri nyinge zote. Uhusiano wetu na Mungu ni sehemu muhimu sana kuona sababu ya kuyafanya hayo yote kuelekea katika hitimisho letu, yaani, uzima wa milele. Hivyo umasikini huu wa kiroho hutufanya tuone sababu ya haya yafuatayo; kujua ukweli huo, kufanya jambo hilo, na kuona thamani ya kile tukifanyacho hata kama matokeo yake hatutayaona katika uhasilia wake kwa muda mfupi tunaoishi hapa duniani. Masikini wa roho ni Mkristo yule mwenye hofu ya Mungu, na wale ambao kwa dhamiri zao njema huongozwa na hofu hii ya Mungu ndani yao na kutenda kadiri ya mwono wa kimungu hata kama hawamjui Kristo au Mungu tunayemwanini na kumwabudu.
Hivyo ni yule mwenye umasikini wa roho katika maana niliyoizungumzia hapo juu atakaye ona huzuni za wengine kwa sababu hali hiyo imo ndani mwake, na hivyo ufarijika na kufarijiwa kwa kutenda tendo hilo la huzuni. Upole wa mtu nje ya hali ya kuzaliwa nayo, ni tabia ile aijengayo mtu, na kumwona mwingine zaidi ya mahitaji yake mwenyewe. Ni hali ya kujali zaidi wengine, kuliko kujionea huruma mwenyewe kuliko pitiliza. Msingi huu ni ule ule wa umasikini wa roho. Kuirithi nchi wa wale wapole ni kuwa wahenga. Mtu huwa mhenga kwa sababu ameacha kitu cha kujifunza au kuigwa na wengine. Kinyume cha kuwa Mhenga ni kuwa Lihoko-roho isiyo salama/bad spirit.
Mpendwa ukiwa maskini wa Roho utawajali wenye njaa, na kutenda haki kwa kila mmoja. Ni kwa kufanya tendo hili bila kujibakiza nasi tutakidhiwa mahitaji yetu na Mungu kwa kipimo hicho hicho. Hivyo, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38. Huku ndiko kushibishwa na Mungu kuliko kwa haki.
Mwenye hofu ya Mungu ndani mwake ambao msingi wake umetokana na umasikini wake wa roho, hujazwa rehema (nguvu ya pekee katika kutenda) kwa sababu ndani mwake kuna nafasi ya Mungu, malipo yake ni neema juu ya neema. Hivyo neema hufuata palipo na neema. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Tazama Kristo anavyokupenda!
Usafi wa moyo ni hali ile yakutokuyabeba yasiyoendana na hali na tabia ya Mungu. Makazi ya Mungu na hasa Roho Mtakatifu ni kwenye mahekalu-miili iye isiyo kuwa na hatia yo yote. Uwepo wa Mungu ndani ya mahekalu haya ni fursa ya kumwona Mungu. Roho huyu Mtakatifu hawezi kupata makazi yake kwenye mahekalu yasiyo na nafasi. Hivyo ni wale tu walio masikini wa roho wenye nafasi ya Mungu ndani ya mioyo yao, na hivyo watamwona Mungu. Mioyo safi ni hakikisho la kumwona Mungu muda wote kwani mtu huyu kesha jianda kwa lolote.
Ni katika umasikini wetu wa roho twaona na kujali wengine wawe na utulivu wa ndani kama tulio nao sisi. Wito huu unatusukuma pasipo hiyana kuwa wapatanishi pale amani ile inapokosekana. Kristo akiwa ndiye mpatanishi wetu kwa Baba yake wa Mbinguni, nasi kwa kufanya tendo hilo la upatanishi kwa wengine twahesabiwa haki ya kuwa wana wa Mungu. Ni maskini wa roho pasipo shaka yoyote aishie bila makuu, na ambaye kwa hali hiyo yupo tayari kuifia haki katika kweli. Hawa ndiyo wafia dini wa nyakati zetu ambao wapo tayari kufa kwa ajili ya wanyonge waminywao haki zako na matajiri katika jamii tunayoishi sasa. Ukweli ni kwamba wanapoifia haki hii, ufalme wa mbinguni ni wao. Huku ni kuishi katika hali ya watoto wadogo, wafanyayo yote katika yote bila kujibakiza kwa sababu hawana shaka na baba /mama yao.” Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14
Masikini wa roho, mwenye nafasi ya Mungu ndani yake, hawezi ogoba shutuma zitolewazo juu yake kwa ajili ya haki au kutenda haki. Haki na Wema ni baadhi ya sifa na asili ya Mungu. Hapa ndipo kwenye furaha ya kweli tunapoifia haki tukijua mtetezi wetu ndiye chanzo na ukamilifu wa furaha ya kweli ndani yetu. Yesu anatukumbusha jambo hili na kutupa angalizo kwa kusema, “kwa kuwa itamfaidi mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36.
Wapendwa wana wa Mungu, jambo la kushangaza badala ya kuishi maadili haya ya Ukristo wetu, yaani,  heri hizi za Mungu, tumekuwa tunaishi kwa nyakati zote na mitindo tofauti tofauti ya  HERI NANE ZA SHETANI kama ifuatavyo;
1.     Heri yao waliochoka sana, waliobanwa na shughuli na kukosa muda wa kukutana na wakristo wenzao Jumapili, na shughuli za Jumuiya kila wiki. Kwa maana hao ni wafuasi wangu waaminifu.
2.     Heri yao wanaofurahia kutambua tabia, udhaifu wa makleri na mapungufu ya watumishi wa Mungu. Kwa maana hao ndio vitendea kazi vyangu.
3.     Heri yao Walei na Watawa na Makleri wanaosubiri kuambiwa kufanya kitu na kutegemea kupongezwa hata kama hawakufanya kitu. Hakika hao naweza kuwatumia vyema.
4.     Heri wanaoguswa na kukwazika kwa vitu vidogovidogo na kuacha Ukristo wao; kwa kutokwenda Kanisani, kutoshiriki masakramenti na kuacha kusali. Kwa maana hao ni wamisionari wangu.
5.     Heri yao hao wanaojitangaza au kudai kuwa wanampenda Mungu na wakati mwingine wanawachukia jirani zao na ndugu zao. Hakika  hao ni mali yangu  Milele.
6.     Heri yao watenganishi na waletao fujo na chuki. Wataitwa wana wangu.
7.     Heri yao wasiokuwa na muda wa kusali kabisa, na kuzisadifikisha kazi na majukumu yako kuwa ndiyo sala. Maana hao wananiombea mimi.
8.     Heri yako wewe unayesoma haya na wewe unayeyasikia haya na kufikiri ni kwa ajili ya watu wengine na siyo wewe mwenyewe. Hakika  nimeshakupata tayari.
Tumsifu Yesu Kristo!
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3
Tusali:-Ee Yesu uliye yashinda mateso, nijalie furaha na shangilio katika mateso ndani na katika Wewe; kwa kuwa kwako thawabu kubwa ipo mbinguni. Amina
 
 

TAFAKARI: SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU


SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU MWAKA-A

Somo I: Kut 34:4b-6, 8-9

Dan: 3:52, 53, 54, 55, 56 (52b)

Somo II: 2 Cor 13:11-14

Injili: Yoh 3:16-18

Nukuu:

“Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli,” Kut 34:6

“Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako,” Kut 34:9

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16

“Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18

“Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi,” 2Kor 13:11

“Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote,” 2Kor 13:14

TAFAKARI: Tu ndani ya Neema ya Bwana Yesu Kristo, pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha sherehe ya Utatu Mtakatifu, ambao ni Mungu mmoja, nafsi tatu; Nafsi tatu Mungu mmoja. Ni Utatu Mtakatifu na Umoja usiogawanyika. Nazo ni Mungu Baba (Muumbaji), Mungu Mwana (Mkombozi), na Upendo wa Mungu Baba na Mwana, yaani, Roho Mtakatifu. Nafsi hizi tatu zinaonekana katika utendaji licha ya kwamba katika utendaji huo wa nafsi moja hautenganishi utendaji wa nafsi nyingine mbili. Kwa mantiki hii, alipo Mungu Baba yupo pia Mungu mwana na Roho Mtakatifu. Na ndivyo iliyo kwa Mungu mwana (Mungu Baba na Roho Mtakatifu), Roho Mtakatifu (Mungu Baba na Mungu Mwana) tokeo la upendo wa Mungu Baba na Mwana.

Kwa mtiririko huu katika utendaji ambao unatuwezesha kupata mwanga katika fumbo hili Takatifu, tunaona katika somo letu la kwanza utendaji wa Mungu Baba, yaani, sifa na utukufu wake. Ni “… Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli,” Kut 34:6. Ukweli huu ujajifunua katika historia nzima ya uumbaji na wokovu wa mwanadamu. Licha ya mwanadamu kukengeuka hapa na pale, Mungu hakuacha kuwa Mungu, yaani, mwingi wa rehema na upendo usio na kipimo. “…maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako,” Kut 34:9.

Ni katika safari hii ya wokovu wa mwanadamu twaona utendaji wa nafsi hii ya pili, yaani, Mungu Mwana. Kristo Yesu ndiye mwokozi. Hatuwezi kusimama katika kweli ndani ya Kristo kama hatumwamini Kristo. Na hatuwezi kumwamini Kristo kama tunamuishi Kristo wa Historia. Yesu Kristo katika maisha yetu na ufuasi wetu kwake ni Kristo aliye hai. Ni kristo tunayekutana naye kila siku ya maisha yetu. Ni Kristo tunayekutana naye katika mateso yetu na furaha yetu. Mateso na furaha kwa Mkristo yanamaana tu pale Kristo anapokuwa kielelezo cha mambo yote. Na hii ndiyo sababu ya Mungu kumtoa Mwanaye katika historia nzima ya wokovu wetu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16.

Wapendwa wana wa Mungu, Imani yetu juu ya Mwana wa Mungu ndiyo hukumu yetu. “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18. Kuamini huku si kwa yale tu tuyapendayo kuyaona na kuyasikia katika maisha yetu, bali ni kuamini hata yale ambaye yapo juu ya uwezo wetu na mara nyingine hatuyaoni kwa uwezo wetu wa kibinadamu. Ni kuamini pia yote yawezekana kwa njia yake na kwa uwezo wake. Huku ndiko kuliamini jina pekee la Mwana wa Mungu. Jina hili lina mamlaka juu ya umilele wako na mimi. Kuamini huku huendana na kutenda kweli kadiri ya imani juu ya Kristo, Maandiko Matakatifu, Kanisa na Mapokea yake. Huwezi kuamini mtu fulani na kutenda kinyume cha imani iliyojenga juu ya mtu yule. Tunapofanya kinyume na imani ile ni wazi kwamba hatujui tunachoamini. Ni sawa na kuvaa miwani ya giza kuelekea usipokujua ili hali unaitaji mwanga. “Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,” Yoh 3:21.

Roho Mtakatifu ambaye ndiye upendo wa Mungu Baba na Mwana, utendaji wake ni kuyatakatifuza yote yaliyoumbwa na kukombolewa. Nafsi hii, yaani, Roho huyu Mtakatifu kati ya kazi zake kubwa ni Umoja, mshikamano, na amani. Ndugu, “…nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.” 2Kor 13:11. Hivyo salama yetu ipo ndani ya fumba zima hili yaani, Utatu Mtakatifu. Hivyo kama asemavyo Mtume Paulo, “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote,” 2Kor 13:14. Amina

Tumsifu Yesu Kristo!

“Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18

Tusali:-Ewe fumbo la ajabu na uzuri wake, tujazwe neema, na upendo ndani yake. Usifiwe Utatu Mtakatifu, na Umoja usiogawanyika.

 

lunes, 12 de junio de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 9 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 9 YA MWAKA-I

Somo: Tob 12:1, 5-15, 20

Zab: Tob 13:2, 6efgh, 7, 8

Injili: Mk 12:38-44

Nukuu:

“Lakini Rafaeli akawaita faraghani Tobiti na Tobia, akawaambia, “Mtukuzeni Mungu; tangazeni sifa zake kwa watu wote kwa ajili ya fadhili alizowafanyia,” Tob 12:6a

“Mtukuzeni na kulisifu jina lake. Watangazieni watu wote matendo ya Mungu kama ipasavyo na wala msichoke kumshukuru,” Tob 12:6b

“Yafaa kutunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu ni lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tendeni mema nanyi hamtapata madhara,”Tob 12:7

“Afadhali sala pamoja na ukweli na kusaidia maskini pamoja na kutenda haki kuliko kuwa tajiri na kukosa uaminifu,” Tob 12:8

“Afadhali kusaidia maskini kuliko kulimbikiza dhahabu,” Tob 12:8b

“Sadaka kwa maskini humwokoa mtu na kifo na kumtakasa dhambi zake zote,” Tob 12:9a

“Wale wanaowasaidia maskini watajaliwa uhai,” Tob 12:9b

“Lakini wale wanaotenda dhambi na kufanya uovu hujiletea madhara wao wenyewe,” Tob 12:10

Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa,” Mk 12:38-40

“Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:43-44

TAFAKARI: “Mtukuzeni Mungu; tangazeni sifa zake kwa watu wote kwa ajili ya fadhili alizowafanyia, tendeni mema kwa watu wote”

Wapendwa wana wa Mungu, tukifanya tathimini ya kina kuhusu maisha yetu, na namna Mungu anavyotuchukulia hasa pale tunapokwenda kinyume na matakwa yake, hatunabudi kumtukuza Mungu, kutangaza makuu yake, na kutenda mema kwa watu wote. Malaika Rafaeli anawaasa Tobia na Sara kuwa na mwelekeo huo katika maisha. Kuna Baraka tele tunapotambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu, na kumshukuru kila wakati. Ndugu yangu, ingefaa kila sekunde useme neno ASANTE kwa Mungu. Tupo kama tulivyo; kuwaza, kupanga, kufanya, na uhuru hata wa kwenda kinyume na mpango wake Mungu kwa upendo wake aliotukirimia. Kwa kweli Mungu ni waajabu sana!

Wapendwa ni mara ngapi waona umuhimu huu wa kutoa shukrani kwa Mungu, hata kwa yale madogo anayokutendea, mfano kukukinga na magonjwa, ajali, kukupa afya njema, na hata uelewano mzuri na jirani zako? Kufanya tendo hili la shukrani ni kutangaza makuu ya Mungu kwa kile anachokufanyia. “Mtukuzeni na kulisifu jina lake. Watangazieni watu wote matendo ya Mungu kama ipasavyo na wala msichoke kumshukuru,” Tob 12:6b.

Hatua ya pili ya kutangaza matendo makuu haya ya Mungu inatuwajibisha kwenda mbali zaidi. Huku ni kuona na kutambua kuwa wapo wengine walioumbwa kama wewe ila hawana fursa ulizojaliwa wewe. Kwa kutambua jambo hili, yakupasa kufanya kitu kwa wale wote wanaohitaji upendo huo wa Mungu aliokujalia wewe kwa wakati na nafasi uliyokuwa nayo. Hata kama ni siri yako na Mungu, yakupasa kuonyesha upendo huo kwa wengine. Hivyo, “Yafaa kutunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu ni lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tendeni mema nanyi hamtapata madhara,”Tob 12:7. Huku ni kujiweka karibu na vizuri zaidi na Mungu. Kutenda mema huku kusibakie kama wazo fulani tu la kufikirika katika uzuri wake. Yatupasa kuliweka katika tendo halisi kama Mungu anavyotufanyia matendo halisi na wakati mwingine tunabaki katika mshangao mkubwa.

Hatua hii ya pili katika kushukuru ni muhimu sana. Hapa ndipo tunapouweka upendo wa Mungu katika mazingira yetu ya kibinadamu. Hapa ndipo tunapompa Mungu umbile letu, kama alivyo lifanya neno kuwa mwili. Hapa ndipo ninapomwona masikini kama ndugu na mmoja ya familia yangu. Hivyo, “Afadhali sala pamoja na ukweli na kusaidia maskini pamoja na kutenda haki kuliko kuwa tajiri na kukosa uaminifu,” Tob 12:8. Baraka na neema alizokujalia Mungu si kama upendeleo kwako ila Mungu anakutaka utoe kwa upendo na ukaribu aliokujalia kwa kuzipata mali hizo. Huna kilichochako katika uhalisia wa umiliki wa hicho ulicho nacho. Vitu vyote na mali zote ni vyake Mungu, Zab 24:1. Mali yetu halali ni dhambi zetu. Hivyo, “Afadhali kusaidia maskini kuliko kulimbikiza dhahabu,” Tob 12:8b.

Ni vigumu sana kama tutakuwa na mwelekeo wa kujilimbikizia mali tu kwa sababu ndiyo mtindo wa kimaisha. Tumepewa mali ili tuzitumie vyema si tu kwa sababu yetu binafsi, ila kwa wengine pia. Ndugu yangu, kwa wewe kuwa na mali ulizokuwanazo si kwamba una nafasi ya pekee sana mbele ya Mungu. Kumbuka hata yule ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wake Mungu, yaani, huyo aliyekupa mali hizo, ana nafasi iliyo sawa na wewe mbele yake. Kwa kujali wajibu huu wa kuwaona wengine katika utajiri wako ndipo unapopata uhai. “Wale wanaowasaidia maskini watajaliwa uhai,” Tob 12:9b. Kinyume cha maneno haya ya Mungu kupitia malaika wake Rafaeli ni ukweli usiopingika. Tusipoyafanya haya kwa ukamilifu wake, tutegemee madhara. “Lakini wale wanaotenda dhambi na kufanya uovu hujiletea madhara wao wenyewe,” Tob 12:10

Angalizo: Tunayafanya haya yote si kwa vile jamii inatutaka tuyafanye hivyo, bali ni msukumo wa ndani na ulio wa kweli kutoka kwa Mungu, mara na baada ya kutambua uwepo wa Mungu kwetu na sababu ya maisha yetu hapa duniani. Jambo hili halikuwa msingi wa kweli wa maisha ya mafarisayo. Waliyafanya hayo yote ili kujizolea umaarufu “ujiko/maujiko” kwa binadamu/wanadamu. Yesu anatoa angalizo na onyo kwao na kwetu leo pia. “Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa,” Mk 12:38-40. Hatari ya mafarisayo haikuishia hapo tu katika kupata huo umaarufu/ujiko kutoka kwa wanadamu, bali walienda mbali zaidi hata kuwadhulumu wajane ambao iliwapasa kuwapigania. Je, leo katika jamii yetu Tanzania tunakwepa dhambi hii?

Ndugu yangu, haijalishi Mungu kakujalia utajiri wa namna gani. Unachotakiwa kufanya ni kujua kwamba ulichonacho umeazimishwa tu kwa wakati, na itakupasa siku moja utoe hesabu yake. Basi kabla ya kashfa hilo ya matumizi mabaya ya mali na vipaji uliyokopeshwa kwa muda mfupi kukupata mbele ya uso wa Mungu, tathinini namna unavyotumia mali hiyo na vipaji hivyo alivyokujalia Mungu. Yesu anatupa kielelezo cha namna ya kufanya. Yesu anapowatazama watoa sadaka katika hekalu, anawanong’onezea wanafunzi wake, na kusema “Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:43-44. Je, mali na utajiri ulikuwa nao unatoa vyote kwa wahitaji kwa ukaribu uliokirimiwa na Mungu?

Tumsifu Yesu Kristo!

Tusali: Ee Yesu tujalie neema ya kuishi na kutoa kwa wengine kadiri unavyotukirimia. Amina