lunes, 31 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 22 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 22 YA MWAKA-B
Somo: 1The 5:1-6, 9-11
Zab: 27:1, 4, 13-14
Injili: Lk 4:31-37
Nukuu:
Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula,” 1The 5:3

Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza,” 1The 5:5 

Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya,” 1The 5:11 

akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34

Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno,” Lk 4:35

TAFAKARI: “Usalama wetu wa mwili na roho twaupata ndani na katika Kristo”

Wapendwa wana wa Mungu, binadamu wa leo katika hangaika yake yote asubuhi hadi jiona, jumatatu hadi jumapili, januari hadi disemba, mwaka hadi mwaka, na mwisho wa maisha yake hapa duniani, maisha yake husukumwa na mifumo mbalimbali ya maisha. Utazamapo mifumo hii ya maisha, utagundua yote ipo katika ushindani wa leo na kesho na mwisho wa siku ni kuufaidia mwili tu.

Wapendwa wana wa Mungu, maisha yetu hapa duniani, na binadamu kwa ujumla wake, ni mwili na roho. Ujio wa Kristo katika dunia hii, na maisha yetu ni kumkomboa binadamu huyu mwili na roho. Kristo hakuacha kuwalisha wale aliokutana nao mwili na roho. Jambo la kujiuliza mimi na wewe ni “kitu gani kinachokupa amani na usalama kila kukicha? Je, ni haya yanayoshikika au yale yasiyoshikika na ya kiroho? Je, twaishi kwa ujanja ujanja wetu. Kama haya ya leo ndiyo yanayotupa furaha na amani, basi tujue kwa uhakika bado hatujakutana na Kristo. Mtume Paulo anatuambia kuhusu jambo hili, Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula,” 1The 5:3. Wengi wetu amani na salama yetu hutokana na mali tulizonazo au nafasi tulizo nazo. Je, hivi kwa vyenyewe vina umilele?

Ndugu yangu, mpango wako wa maisha uliowekwa ndani yako ni zaidi ya yale uliyonayo au uyafanyayo. Katika Kristo sote tumewekwa katika mizania sawa mbele ya Mungu kwa sadaka yake pale msalabani. Hivyo, ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza,” 1The 5:5. Kwa Kristo, sote tumefunuliwa siri za mbinguni. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu pasipo mastahili yetu. Tunapotambua ukweli huu wa Mungu ndani ya maisha yetu, hatuna budu kutaabikiana katika Kristo na kusaidiana. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya,” 1The 5:11. Wokovu tuupatao bure kutoka upendo wa Kristo, si kwa sababu yetu wenyewe, bali hata wale ambao bado hawajamfahamu Kristo. Tuupatapo upendo wa Kristo na nuru katika maisha haya ni kwa furaha hiyo hiyo twapaswa kuishirikisha kwa wengine ambao bado hawajamfahamu.

Wapendwa katika Kristo, uwepo wa Kristo na jina lake, ni tishio kwa roho zile zilizo kinyume na mpango wa Mungu. Pepo wachafu huelewa na kuogopa uwepo wa Kristo. Hakuna roho chafu zinazoweza kuushinda uwepo wa Kristo. Pepo wachafu hawana amani mara litamkwapo jina la Yesu.  Uwepo wa Kristo ni tishio kwa wale wote wampingao Kristo. Mapepo yanasema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34. Utakatifu wa Yesu na ukamilifu wake ni kielelezo cha maisha yetu na yale yatupasayo kuishi ili kuuridhi ufalme wa Mungu. Ukamilifu na utakaatifu wa Yesu ndio unaompa mamlaka ya kukemea roho chafu na kuwaweka huru wale waliotawaliwa katika ulimwengu huo wa roho. Hivyo Yesu anakemea na kusema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno,” Lk 4:35. Ndugu yangu, kimbilio lako lipo wapi?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU MWEMA, KAMWE USINIACHA KATIKA MASHAKA YANGU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario