domingo, 9 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 19 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 19 YA MWAKA-B
10/8/2015
Somo: 2Kor 9:6-10
Zab: 111
Injili: Yoh 12:24-26
Nukuu:
Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6

Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:7

Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24

Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele,” Yoh 12:25

TAFAKARI: “Unaweza kutoa bila kupenda, ila huwezi kupenda bila kutoa.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunapotembea mabarabarani, tuwapo maofisini, tuwapo majumbani mwetu, tuwapo sehemu za starehe kama kwenye mahoteli na mabaa, tunakutana na omba omba wengi sana na kutokana na kero zao za kutuomba tunajikuta mara nyingi tunatoa bila kupenda. Tunafanya hivyo ili tuondokana na kero ile. Endapo tunafanya jambo hili kwa mtazamo huu, ni sawa na kupanda haba na matokea yake tutavuna hapa. Ni tendo la utoaji lisilo na neema ya Mungu ndani yake. Kwa upande mwingine tunapopenda kweli basi hatuachi kutoa.

Furaha ni kama kikohozi huwezi kukizuia. Upatwapo na kikohozi itakulazimu kukohoa tu. Tendo hili ni sawa na pendo la kweli. Pendo la kweli litakulazimu kutoa bila kujibakiza. Huku ndiko kule kupanda kwa ukarimu kunakotupelekea kuvuna kwa ukarimu. Hivyo Mtume Paulo anasema, “Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6. Kupata neema na baraka za Mungu, ni kulitenda jambo hilo pasipo kulazimishwa na wala si kwa huzuni. Tunafanya kwa upendo wa kweli tukimtazama Yesu Kristo kama kielelezo chetu. Hivyo, kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:7. Je, mtazamo wako wa utoaji upoje?

Injili ya leo inatuzamisha zaidi katika tendo hili la kujitoa kwa ajili ya wengine. Ukweli ni kwamba huwezi kujitoa bila kujibakiza ukabaki katika hali ile ile. Tendo hili la kujitoa bila kujibakiza linatubadili mwono wetu na mfumo mzima wa maisha. Je, Yesu ana maana gani anaposema, “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Ndugu yangu, ni katika kufa tunapata uzima, na, ni katika uzima yatupasa kufa ili uzima ule uendelee siku kwa siku na milele yote. Fumbo hili na mfano huu wa chembe ya ngano Yesu anautoa akionyesha ni kwa mauti gani ataufia ulimwengu ili kuupa uzima wa milele hasa kwa wale wanaomwamini. Vile vile kwa fumbo hili na mfano huu wa chembe ya ngano Yesu anatutaka tuwe mfano kwa maisha tunayoishi kadiri ya wito wa kila mmoja wetu.

Wapendwa tukichukulia maisha ya familia, Baba huleta uzima katika familia yake anapojitoa kabisa na bila kujibakiza. Kwa kufanya hivi mke wake anaongezeka na watoto pia. Ni kwa namna hiyo hiyo Mama katika familia anapojitoa kabisa na bila kujibakiza analeta uzima katika familia yake kwa Mume wake kuongezeka na watoto pia. Kwa upande wa watoto huleta uzima katika familia kwa kutimiza nyajibu zao, mfano, kusoma vizuri na kwa bidii na kutumia rasilimali fedha vizuri ili kesho wawe furaha na matumaini kwa wazazi wao. Mfumo wa maisha haya ni sawa na mshumaa unaotoa mwanga huku ukifa kwa kuyeyuka. Nami kama Mtawa na Padre, yanipasa kufa kila siku ili pale nilipo pawe na uhai wa kweli. Nakufa kila siku kwa kutimiza wajibu wangu vyema. Huku ni kuichukia nafsi yako kwa ajili ya uzima wako na wale walio wako na chini yako. Hivyo Yesu anasema,Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele,” Yoh 12:25. Je, maisha yako na majitoleo yako yanamatokeo ya uzima wa milele?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIJALIE NEEMA YA KUJITOA BILA KUJIBAKIZA. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario