lunes, 10 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 19 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 19 YA MWAKA-B
11/8/2015
Somo: Kum 31:1-8
Zab: 32
Injili: Mt 18:1-5, 10, 12-14
Nukuu:
Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha,” Kum 31:6

akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3

Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4

Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee,” Mt 18:14

TAFAKARI: “Ajinyenyekeshaye mwenyewe ndiye aliye mkuu katika ufalme wa Mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu, unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote. Unyenyekevu unatudai kujifahamu mazuri na mapungufu yetu. Hivyo kukua kimwili na kiroho kuliko kwema na mpango wa Mungu, yaani maisha yenye malengo, kunahitaji sana fadhila hii ya unyenyekevu. Musa kwa kuongozwa na fadhila hii ya unyenyekevu, anajijua vizuri katika mazuri yake na mapungufu yake. Hivyo anasema, “Mimi leo ni mwenye miaka mia na ishirini; siwezi tena kutoka na kuingia, na Bwana ameniambia, Hutavuka mto huu Yordani,” Kum 31:2. Maneno haya ya Musa yanaonyesha unyenyekevu wake ulivyo, na hivyo haoni sababu ya kukwamisha malengo ya Mungu katika safari ya ukombozi. Ni wajibu wake kumkabidhi mwingine aendeleze kazi ile ya ukombozi. Je, ni mara ngapi unaupokea udhaifu wako ili kupisha kazi na matakwa ya Mungu? Yoshua anakuwa mrithi wa Musa. Ni mara ngapi tupo tayari kuachia ngazi na kuona uzuri kwa wengine ili waendeleze pale tulipoachia? Bila unyenyekevu wa kweli hatuwezi kuwa tayari kujipokea na kuwapokea wengine katika mazuri yao na mapungufu yao. Hivyo Mungu anatuwasa, Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha,” Kum 31:6. Mungu wetu ni UPENDO, na tunakuwa watoto wake tunapoishi upendo huo.

Injili yetu ya leo inatuzamisha zaidi katika fadhila hii ya unyenyekevu. Yesu anamfananisha mnyenyekevu na mtoto mdogo. Mwenye fadhila ya unyenyekevu mara zote hujiachilia kwa Mungu kila kitu, kama alivyo mtoto mdogo anavyojiachilia kwa wazazi wake. Kujiachilia huku kunatutoa woga na kutujaza ujasiri. Hivyo Yesu anatuambia hivi: “Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Ndugu yangu, fadhila ya unyenyekevu ni njia itupelekayo kwenye ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4. Kujinyenyekeza kwetu hakutupunguzii utu wetu bali kunatujengea utu huo kwa watu na zaidi, mbele ya Mungu. Unyenyekevu hautufanyi wajinga, bali ni shule ya kutuongezea maarifa ya kuishi kile tulichoitiwa kila mmoja kadiri ya wito wake. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee,” Mt 18:14. Unyenyekevu utupeleka kwa Baba. Kuishi fadhila hii ni tendo la kujisalimisha nafsi kuliko kwema.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUJALIE UNYENYEKEVU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario