sábado, 8 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 19 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 19 YA MWAKA-B
9/8/2015
Somo I: 1Fal 19:4-8
Zab: 33:2-9
Somo II: Efe 4:30-5:2
Injili: Yoh 6:41-51

Nukuu:
“Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu,” 1Fal 19:4b

Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule,” 1Fal 19:5

Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi,” Efe 4:30

tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi,” Efe 4:32

Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato,” Efe 5:1-2 

Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44

“Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu,” Yoh 6:45b

Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima,” Yoh 6:47-48

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51

TAFAKARI: “Kristo yu hai na chakula atoacho Yesu ni mwili wake, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Usife Moyo, tunaye atupiganiaye daima.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa ana adhimisha Dominika ya 19 ya mwaka “B” wa Kanisa. Masomo yote matatu ya leo yanatuelekeza njia ya kufuata, na sababu ya uzima wetu. ‘Ni kweli kwamba kifo cha nyani miti yote huteleza.’ Ila kwa upande wetu, na hasa tunaomwamini Kristo, msemo huu ‘kifo cha nyani miti yote huteleza,’ hauna mashiko. Ni kwa imani thabiti Eliya anajiachilia mikoni mwa Mungu alipofikia mkwamo wa matumaini yake yote na kupata jibu hapo hapo. Maandiko matakatifu yanatuambia, Eliya “Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu,” 1Fal 19:4b. Kujiachia huku kwa Nabii Eliya kunamfanya kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule,” 1Fal 19:5. Ndugu yangu katika Kristo, ‘pasipo njia Mungu ufanya njia.’ Je, waamini jambo hilo?

Ndugu yangu, katika Injili ya leo Mungu yule aliyekuwa mbali sana na wanadamu, ndiye leo Emanueli, yaani ‘Mungu pamoja nasi.’ Ni kwa kupitia fumbo zima la kumwilishwa kwa neno, sote leo kwa kuamini neno huyu wa Bwana tunapata uzima wa milele. Hivyo tangia sasa, Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, (Yesu Kristo) asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44. Uzima wetu leo bila Kristo haiwezekani. Je, mafundisho haya ya Yesu yanasema jambo lolote juu ya maisha yako? Je, ni jambo gani linalokupa uzima leo na sasa? Vipi basi kuhusu maisha yako ya umilele? Je, ni cheo chako leo? Je, ni utajiri wako leo? Je, ni akili zako leo? Je, ni mafanikio yako kitaaluma leo? Ndugu yangu, Yesu anatuambia hivi: “Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu,” Yoh 6:45b. Tunajifunza kwa Baba yetu aliyembinguni haya yafuatayo: Upole, Unyenyekevu, uaminifu, utii, Upendo wa kweli, na zaidi huruma yake.

Msingi wa ufahamu wote wa elimu kuhusu Mungu upo kwenye Imani ya kweli. Kuamini yote aliyotufundisha Kristo na kuyaishi. Kumchukua Kristo katika kweli na haki, na siyo kama tukio la kihistoria ambalo lilikuwa hai wakati fulani tu katika historia yake. Yesu yu hai jana, leo na milele yote. Naye anasema, Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima,” Yoh 6:47-48. Pamoja na kwamba uzima wetu wa leo na sasa wawezwa kusogezwa kwa chakula hiki tukiangaikiacho na kinachoharibika, Yesu tu ndiye chakula cha uzima. Chakula cha uzima ni kile kilichoshuka kutoka mbinguni, yaani neno aliyefanywa mwili, KUMWILISHWA. Huyu ndiye Kristo tunayemwamini na kumfuata. Yesu mwenyewe anasema, Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51. Je, natambua ukweli huu ninaposhiriki mwili na damu ya Yesu? Au huwa nayapokea maumbo haya ya mke na divai kwa mazoea tu? Je, napokea mwili na damu ya Yesu katika hali safi? Je, ni kitu gani kinachonizuia kumpokea Kristo na kujazwa uzima wake? Kwa nini basi nakumbatia vikwazo na kukosa uzima huu wa milele? Nitajifungia hadi lini kwenye gereza hili la kiroho? Kwa mtindo huu nayapenda kweli maisha yangu? Ndugu yangu ambaye upo kwenye kifungo hiki chukua hatua na fanya mabadiliko juu ya maisha yako.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, kutokuishi ukweli huu ni kumuhuzunisha Roho Mtakatifu. Huyu ndiye anayetufunulia siri zote kuhusu ufalme wa Mungu, kutuongoza na kututakatifuza katika kweli na haki. Hivyo,msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi,” Efe 4:30. Kwa ubatizo wetu, kuimarishwa kwetu, na kwa kuwekwa wakfu kwetu kama makleri tunatiwa muhuri huu wa Roho Mtakatifu hata siku ya ukombozi wetu. Je, ndugu yangu, unaishi ahadi zako za ubatizo? Je, wasimama hodari kama askari wa Kristo kwa sakramenti yako uliyopokea ya KipaImara? Je, upo tayari kuufia ukweli kama Kristo kwa maisha yako ya wakfu kama mtawa na mkleri? Hapa ndipo penye changamoto yetu ya Imani kila mmoja wetu kadiri ya wito wake. Tusisahau kuwa wote tunaitwa katika utakatifu ambao ndicho cheo chetu.

Wapendwa wana wa Mungu, kuishi cheo hicho, yaani UTAKATIFU tulioitiwa yatupasa kuishi mfumo huu wa maisha, yaani, kama asemavyo Mtume Paulo, tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi,” Efe 4:32. Msamaha wa kweli ni uthibitisho wa kile tunachokiishi na kukiamini kuhusu Kristo. Kristo pamoja na kuwambwa pale msalabani hakuacha kutoa msamaha. Jambo la pili ni kuishi maisha ya Upendo kama wana wa Mungu. Upendo usiobagua kabila, rangi, ukanda, na wala utaifa. Sote kwa upendo na huruma ya Mungu tumekuwa kama tulivyo na ilivyompendeza Mungu. Utofauti zetu ndio uzuri wa Mungu. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato,” Efe 5:1-2. Ndugu yangu, mimi na wewe tunayokazi moja tu hapa duniani. Nayo ni kumtafuta Mungu kila siku ya maisha yetu. Mungu huyu na Yesu huyu tunakutana naye nyumbani mwetu, kazini mwetu, mabarabarani tunamopita na zaidi katika fumbo la mwili na damu yake. Hapa ndipo penye uponyaji wa kweli.

Wengi wetu kama alivyo Mama Christina, tumejiwekea nidhamu ya kiroho ya kwenda kila siku asubuhi Ibada ya  Misa Takatifu, na tunaona bila kufanya hivyo twamkosea Mungu sana. Lakini mara nyingi tunasahau kuwa Mungu huyu, na Kristo huyu yupo kwa namna tofauti tofauti na tunapishana naye tunapoelekea huko Makanisani.

Mama Christina siku moja alijidamka mapema asubuhi kuwahi misa za wiki kama iliyokuwa ada kwake. Alipofika mlango kuu wa Kanisa lile alikutana na maneno haya; “LEO SIPO HAPA UMENIACHA NYUMBANI KWAKO.” Mara ile mama yule alishtuka na kuanza kujiuliza “kulikoni maneno haya?” Katika tafakari ile alikumbuka jambo hili. “Jana yake alipotoka kazini mfanyakazi wake alimwambia hali yake ni mbaya sana na anahisi ana malaria. Christiana hakufanya lolote, wala kumsikiliza. Hivyo alidai atengewe maji ya kuoga na amechoka sana. Hivyo aliwaza kuhusu kesho kudamka na kwenda Kanisani.”

Ndugu yangu, Mara nyingi Mungu wetu na Yesu wetu tunayemfuata tunamwacha majumabani mwetu, au kupishana naye barabarani tunapoelekea Makanisani.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUPE UZIMA WAKO ILI TUUONE PIA KWA WALE TUNAOKUTANA NAO KILA SIKU. AMINA.

No hay comentarios:

Publicar un comentario