sábado, 8 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 18 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 18 YA MWAKA-B
8/8/2015
Somo: Kum 6:4-13
Zab: 17:2-4, 47, 51
Injili: Mt 17:14-20

Nukuu:
Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote,” Kum 6:4-5

ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa,” Kum 6:12 

Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake,” Kum 6:13 

Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya,” Mt 17:15-16

Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu,” Mt 17:17

Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu,” Mt 17:20

TAFAKARI: “Mwamini Yesu pasipo shaka nawe upate uponyaji.”

Wapendwa wana wa Mungu, “basi kwa imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1. Kwa Imani wana wa Israeli walimtumainia Mungu pale walipotengemea msaada wake na hata pale walipokosa mwelekeo. Ni kwa Imani hiyo na uwezo wake Mungu juu ya historia nzima ya wokovu wetu, Wayahudi wanathubutu kusema pasipo shaka:Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote,” Kum 6:4-5. Maneno hayo yanabeba muhimili wote wa maisha yao, na historia nzima ya Taifa hili la Waisraeli. Sala hii imebeba shukrani zote walizotendewa na Mungu tangu mwanzo wa Taifa hili, na wanazidi kumwomba Mungu kudumisha uhusiano huu hadi mwisho wa nyakati.

Kama ilivyo historia hii ya Taifa hili la kiyahudi, hawakuweza kusahau mkono wa Mungu kuwatoa utumwani Misri. Msingi huu wa Imani unarizishwa kwa vizazi vyote, na kutaarifiwa hivi; ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa,” Kum 6:12. Je, leo wewe kama mzazi unawarizisha nini watoto wako? Mungu wetu anayetuwezesha kila kitu katika maisha yetu ndiye tunayepaswa kumcha na kumtumikia. Hivyo, Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake,” Kum 6:13. Je, ni jambo gani linalosukuma maisha yako? Wengi wetu tunasukumwa na vyeo vyetu, nafasi zetu, mali na utajiri wetu, sifa na majigambo yetu. Hivi vyote ni vizuizi vya kuuona uso wa Mungu. Yote tuliyo katika jamii yetu leo na sasa yawe dhamana na njia ya kumjua Mungu, kumpenda, tumtumikie na mwisho turudi kwake mbinguni kwenye umilele.

Imani katika maisha ni jambo la msingi sana. Bila Imani hatuwezi kuishi hata chembe ya uhalisia wa vitu. Ni kwa imani tunajibidisha kusoma na hata kufanya kazi kwa bidii tukiwa na hakika ya mambo yatarawajiwayo. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka, na hasa tukiwa na jemedari wetu mkuu Yesu Kristo. Mama mwenye shida na ugonjwa wa mwanaye anamwendea Yesu kwa mashaka, na kusema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya,” Mt 17:15-16. Mama huyu anataka ishara pasipo kuwa na Imani ya kutosha. Miujiza siyo msingi wa Imani, bali hukomaza Imani. Jambo la msingi ni kuamini kwanza pasipo shaka. Kwa tendo hili la kuwa na shaka katika Imani, Yesu anatoa angalisho: “Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu,” Mt 17:17. Yesu anajua kwa uhakika ipo siku hatutakuwa naye kimwili, na hivyo tuwaamini wale aliowaweka wakfu kwa kazi yake, na hasa Kanisa. Ni kwa Imani kila mbatizwa anaweza kufanya kazi azifanyazo Kristo.

Wanafunzi wa Yesu wanakiri hawakuweza kufanya aliyoyafanya Yesu. Hivyo Yesu anawapa sababu ya kutokufikia lengo lile na matamanio yao. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu,” Mt 17:20. Je, wamwamini Yesu uwapo katika shida tu? Chunguza vizuri maisha yako na mwenendo wako wa kila siku Kiimani.

Tumsifu Yesu Kristo!

EE YESU TUZIDISHIE IMANI.

No hay comentarios:

Publicar un comentario