JUMATANO WIKI YA 19 YA MWAKA-B
12/8/2015
Somo: Kum 34:1-12
Zab: 65
Injili: Mt 18:15-20
Nukuu:
“Bwana akamwambia, Hii
ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao
wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko,” Kum 34:4
“Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye
peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo,” Mt 18:15
“Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza
kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru,” Mt 18:17
“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana
duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye
mbinguni,” Mt 18:19
TAFAKARI: “Furaha ya Mungu tunapopatana na kuishi katika amani na
upendo.”
Wapendwa wana wa Mungu, makusudi ya Mungu katika maisha
yetu ni sisi sote tuishi kwa amani na upendo kama alivyotupenda yeye mwenyewe.
Mungu kwa kumtuma mwanaye ulimwenguni alikuwa na makusudi hayo hayo ya
kutupatanisha naye baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza. Pamoja na upendo huo
wa Mungu Baba, bado tunaona kati yetu tunaishi kwa kutopendana na mbaya zaidi
ndugu tuliozaliwa tumbo moja. Tunaishi kwa visasi na hata kutakiana mabaya.
Je, tufanyaje nini tunapokoseana kama ndugu? Yesu
anatufundisha namna ya kufanya. Naye anasema hivi: “Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye
peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo,” Mt 18:15. Ni vyema kama umekosana na
ndugu yako mkayazungumza mkiwa naye na kupatana naye. Ni vyema mkayamaliza kama
ndugu. Hamuitaji kuyakuza na kuwafaidia wengine kwa upungufu wenu. Kama
hatakusikia na hayupo tayari kukusikiliza, Yesu anatupa nafasi ya pili. Naye
anasema hivi: “Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza
kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru,” Mt 18:17. Kanisa
likiwa ndio mwili wa Yesu nasi tukiwa viungo vyake, ndiyo sehemu muhafaka wa
kuyazungumza yale yote yaliyokwenda kinyuma na upendo wa Mungu. Je, tunatumia
nafasi hii vyema kuyamaliza yale yanayotusibu? Kwa nini basi tunakimbilia
mahakamani kwa mambo yetu ya familia? Je, tuupatapo ushindi huo wa kimahakama
utatusaidia kuujenga tena ule undugu wetu ulioingia dosari? Ndugu yangu,
tusipokuwa tayari kulisikiliza Kanisa tunahesabiwa kama watu wa mataifa.
Wapenda wana wa Mungu, yatupasa kuyamaliza mambo yote sisi
wenyewe, na pale tunaposhindwa kufanya hivyo, basi tuliachie Kanisa litusaidie
kufikia muhafaka wa matatizo yetu. Hapa ndipo penye furaha ya Mungu wetu aliye
hai. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu
watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba
yangu aliye mbinguni,” Mt 18:19. Je, unataka ushindi wa kidunia au upendo wa
Mungu wako aliye hai? Patana na ndugu yako kindugu, naye Mungu atakuneemesha
katika haki na kweli.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU USINIPE NAFASI YA KUISHI NA KISASI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario