ALHAMISI WIKI YA 19 YA MWAKA-B
13/8/2015
Somo: Yos 3:7-10a, 11, 13-17
Zab: 113
Injili: Mt 18:21-19:1
Nukuu:
“Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai
yu kati yenu,” Yos 3:10
“Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba
mara sabini,” Mt 18:22
TAFAKARI: “Hakuna uponyaji wa kweli pasipo msamaha.”
Wapendwa wana wa Mungu, ni ukweli kwamba katika maisha yetu
tumeumizwa na kuwaumiza wengine. Kwa mantiki hii kila mmoja wetu anayomaumivu
ya ndani. Ili kuponya maumivu haya ya ndani yatupasa kusamehe tukitambua pia
katika maisha tuliwaumiza watu wengine pia. Injili ya leo inatuwasa kusamehe.
Tendo hili si ombi ila ni amri ya Mungu mwenyewe. Sala yetu ya Baba yetu,
inaeleza tendo hili la kusamehe kama sharti ya yale tuyaombayo kwa Mungu,
“utusamehe sisi kama tunavyo wasamehe wale walio tukosea.” Mfano alioutoa Yesu
kwenye Injili ya leo unaonyesha ni kwa namna gani yatupasa kuwa na utu wa kweli
na kusamehe pasipo sharti. Pili, yatupasa kuishi na watu vizuri. Kwa kufanya
tendo hilo, tutajua kweli ni nani tunayemtumikia na kumfuata. “Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa
Mungu aliye hai yu kati yenu,” Yos 3:10.
Je, kipimo cha kusamehe ni kipi? Mtakatifu Augustino
anatuambia kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo. Hivyo basi, kipimo cha
kusamehe ni kusamehe bila kipimo. Ni kwa mtazamo huu tunaona Yesu anamjibu
Petro, alipotaka kujua ni mara ngapi yampasa kusamehe atakapokosewa. Yesu
anamjibu Petro na kusema, “Sikuambii
hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22. Ndugu yangu, unapotoa msamaha usihesabu uzito wa
kile ulichokosewa, bali tazama huruma ya Mungu kwa yule unayemsamehe na fanya
hivyo kwa moyo mweupe kabisa. Samehe ukijua kuna mambo mengi tu Mungu
amekusamehe ambayo kama ingeyafanya jino kwa jino usingekuwa jinsi ulivyo leo.
Hakika
tusipowasamehe wale waliotukosea katika mtazamo wa Kimungu na wana wake
tulioumbwa kwa sura na mfano wake, Mungu huyu tunayemwamini hatakuwa tayari
kutusamehe makosa yetu. Yesu anaweka wazi ukweli huu anaposema, “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni
atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake,” Mt
18:35. Swala kubwa hapa ni hili, kwa nini tunaweka masharti katika kusamehe?
Je, haitoshi kumsamehe mtu na kuacha neema ya Mungu kufanya kazi ndani yake?
Je, hauoni kwa kufanya hivyo unajiweka huru na kumweka huru yule aliyekukosea?
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU, HUKUACHA HATA MARA MOJA KUTUSAMEHE MAKOSA YETU.
TUJALIE NEEMA YA MSAMAHA WA KWELI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario