sábado, 22 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 21 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 21 YA MWAKA-B
23/8/2015
Somo I: Yos 24:1-2a, 15-18b
Zab: 34:1-2, 15-22
Somo II: Efe 5:21-32
Injili: Yoh 6:60-69
Nukuu:
Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao,” Yoh 24:16-17

Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23

Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27

Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24

Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31

Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,” Yoh 6:63 

Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 6:65
Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69 

TAFAKARI: “Tumeunganishwa na Kristo kwani Yeye anayo maneno ya uzima uzima wa milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 21 ya mwaka “B” wa Kanisa. Masomo yote matatu ya leo yanatupa na kutuelezea upendo wa Mungu unaojionyesha katika mfungamanisho wetu na Kristo. Hivyo, “tumeunganishwa na Kristo kwani yeye anayo maneno ya uzima wa milele.” Upendo huu wa Mungu na Imani yetu juu yake bila Kristo hakuna maana yoyote. Ukamilifu wa historia yetu ya wokovu unatimia kwa “tendo la neno kufanyika mwili na kukaa kwetu.” Huu ni upendo mkuu ambao Mungu kaufanya kwa watu wake.

Hivyo kwa kupitia mwono huu wa upendo wa Mungu kwa watu wake, Waisraeli hawapo tayari kumwasi Mungu na kuabudu miungu mingine. Nao wakasema, “tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao,” Yoh 24:16-17. Ndugu yangu unaonja upendo wa Mungu katika maisha yako ya kila siku? Je, únalo lolote la kumshukuru Mungu unapotazama historia yako kama wafanyavyo Waisraeli?

Upendo huu wa Mungu kwa watu wake yatupasa kuuona katika mambo yote yenye kutupeleka katika umoja wake, upendo wake, ushirikiano wake na hata katika maagano yetu katika maisha. Ni kwa kupitia umoja huo, upendo huo, na ushirikiano huo wa Mungu na mwanaye mpenzi, Yesu Kristo Mungu hujidhihirisha kwetu kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Upendo wa Mungu na mshikamano na mwanaye tunauona katika masakramenti yake, na hasa leo tunavyotafakari kwa ukaribu sakramenti hii ya ndoa. Naye Mtume  Paulo anasema, Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23. Hapa upendo wa Mungu kupitia Kristo mwenyewe unaonekana kwa utii huu wanaoishi wana ndoa, na hasa kwa mke kumtiii mumewe. Je, ndoa zetu leo ni salama? Akina mama mnaishi ukweli huu katika agano lenu la ndoa? Leo baadhi ya wanawake wamefikia kuwaita waume zao vyama chakavu. Je, hayo ndiyo makusudio ya Mungu na muungano wenu huo?

Kwa upande wa wanaume yawapasa kuwapenda wake zao katika kweli na haki. Upendo huu unafananishwa na upendo wa Kristo na Kanisa lake. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27. Wanaume zieshimuni ndoa zetu kwani ndio utakatifu wenu mnapoziishi katika kweli na haki. Wake zenu hawahitaji mambo ya pekee sana zaidi ya kuyasadifu yale wayatendayo kila siku katika familia. Tabia ya kuwaita wake zetu magoli kipa ni chukizo mbele ya Mungu. Muunganiko wenu ni makusudio ya Mungu, na ndivyo alivyoona inafaa.

Utii wa kweli si utumwa kwenu, bali ni ukamilifu wa makusudio ya Mungu katika maisha ya umilele. Wito wenu wa ndoa ni kuufikia umelele wa maisha yenu mlioandaliwa kupitia sakramenti hiyo. Hivyo, kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24. Ni kuwa na utii katika Kristo kwa sababu yeye anayo maneno la uzima wa milele. Ni kwa kupitia NENO huyu vyote vilifanyika, na kwa kupitia NENO huyu vyote huwa na uzima wa milele. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31. Tendo hili la ajabu katika sakramenti hii ya ndoa halimwesabii haki mmoja wa wanandoa kuwa na mambo yake ya pekee na binafsi tena. Hakuna msamiati huu tena wa kusema hiki changu na hiki chako. Kwa kufanya hivyo ni kuujeruhi mwili huu mmoja. Je, jambo hili lina ukweli katika ndoa yako? Je, ni mambo mangapi ya siri unayoyafanya bila kumuhusisha mwenzi wako wa ndoa? Je, hujui kwa kufanya hayo unaijeruhi ndoa yako? Ndugu yangu kama unaishi ukweli huu na kinyume cha sakramenti hiyo ya ndoa, elewa kwamba ndoa hiyo ishakufua katika uhalisia wa mambo na ukweli wa Kimungu. Kilicho baki ni maagizo kuu, na wote mmekuwa wasanii katika sakramenti hii Takatifu.

Wapendwa wana wa Mungu, hayo yote yanauzima yakiwa ndani na katika Kristo. Ni katika roho na siyo mwili yote upata uzima. Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,” Yoh 6:63. Ni kwa kupitia Kristo tunapewa Roho huyu wa Mungu kuyaishi yale yote kila mtu kadiri ya wito wake. Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 6:65. ‘Kristo ndiye njia, kweli, na uzima,’ Yoh 14:6.

Mafundisho haya ya Yesu kuhusu kujiachia kwake kunakoendana na wito wa kila mmoja wetu, yanakuwa mafundisho magumu sana kwani yanatuhitaji kujiachilia kwake kabisa. Yatupasa kuushinda ubinadamu wetu kila siku. Yesu anapowauliza kukata tamaa kwa wanafunzi wake na hivyo kurudi nyuma, Simoni Petro anajibu, “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69. Wapendwa Kristo anayo maneno ya uzima. Je, uzima wako unaupata wapi?


Tumsifu Yesu Kristo!

No hay comentarios:

Publicar un comentario