lunes, 31 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 22 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 22 YA MWAKA-B
Somo: 1The 5:1-6, 9-11
Zab: 27:1, 4, 13-14
Injili: Lk 4:31-37
Nukuu:
Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula,” 1The 5:3

Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza,” 1The 5:5 

Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya,” 1The 5:11 

akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34

Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno,” Lk 4:35

TAFAKARI: “Usalama wetu wa mwili na roho twaupata ndani na katika Kristo”

Wapendwa wana wa Mungu, binadamu wa leo katika hangaika yake yote asubuhi hadi jiona, jumatatu hadi jumapili, januari hadi disemba, mwaka hadi mwaka, na mwisho wa maisha yake hapa duniani, maisha yake husukumwa na mifumo mbalimbali ya maisha. Utazamapo mifumo hii ya maisha, utagundua yote ipo katika ushindani wa leo na kesho na mwisho wa siku ni kuufaidia mwili tu.

Wapendwa wana wa Mungu, maisha yetu hapa duniani, na binadamu kwa ujumla wake, ni mwili na roho. Ujio wa Kristo katika dunia hii, na maisha yetu ni kumkomboa binadamu huyu mwili na roho. Kristo hakuacha kuwalisha wale aliokutana nao mwili na roho. Jambo la kujiuliza mimi na wewe ni “kitu gani kinachokupa amani na usalama kila kukicha? Je, ni haya yanayoshikika au yale yasiyoshikika na ya kiroho? Je, twaishi kwa ujanja ujanja wetu. Kama haya ya leo ndiyo yanayotupa furaha na amani, basi tujue kwa uhakika bado hatujakutana na Kristo. Mtume Paulo anatuambia kuhusu jambo hili, Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula,” 1The 5:3. Wengi wetu amani na salama yetu hutokana na mali tulizonazo au nafasi tulizo nazo. Je, hivi kwa vyenyewe vina umilele?

Ndugu yangu, mpango wako wa maisha uliowekwa ndani yako ni zaidi ya yale uliyonayo au uyafanyayo. Katika Kristo sote tumewekwa katika mizania sawa mbele ya Mungu kwa sadaka yake pale msalabani. Hivyo, ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza,” 1The 5:5. Kwa Kristo, sote tumefunuliwa siri za mbinguni. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu pasipo mastahili yetu. Tunapotambua ukweli huu wa Mungu ndani ya maisha yetu, hatuna budu kutaabikiana katika Kristo na kusaidiana. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya,” 1The 5:11. Wokovu tuupatao bure kutoka upendo wa Kristo, si kwa sababu yetu wenyewe, bali hata wale ambao bado hawajamfahamu Kristo. Tuupatapo upendo wa Kristo na nuru katika maisha haya ni kwa furaha hiyo hiyo twapaswa kuishirikisha kwa wengine ambao bado hawajamfahamu.

Wapendwa katika Kristo, uwepo wa Kristo na jina lake, ni tishio kwa roho zile zilizo kinyume na mpango wa Mungu. Pepo wachafu huelewa na kuogopa uwepo wa Kristo. Hakuna roho chafu zinazoweza kuushinda uwepo wa Kristo. Pepo wachafu hawana amani mara litamkwapo jina la Yesu.  Uwepo wa Kristo ni tishio kwa wale wote wampingao Kristo. Mapepo yanasema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34. Utakatifu wa Yesu na ukamilifu wake ni kielelezo cha maisha yetu na yale yatupasayo kuishi ili kuuridhi ufalme wa Mungu. Ukamilifu na utakaatifu wa Yesu ndio unaompa mamlaka ya kukemea roho chafu na kuwaweka huru wale waliotawaliwa katika ulimwengu huo wa roho. Hivyo Yesu anakemea na kusema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno,” Lk 4:35. Ndugu yangu, kimbilio lako lipo wapi?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU MWEMA, KAMWE USINIACHA KATIKA MASHAKA YANGU. AMINA

sábado, 22 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 21 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 21 YA MWAKA-B
23/8/2015
Somo I: Yos 24:1-2a, 15-18b
Zab: 34:1-2, 15-22
Somo II: Efe 5:21-32
Injili: Yoh 6:60-69
Nukuu:
Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao,” Yoh 24:16-17

Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23

Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27

Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24

Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31

Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,” Yoh 6:63 

Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 6:65
Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69 

TAFAKARI: “Tumeunganishwa na Kristo kwani Yeye anayo maneno ya uzima uzima wa milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 21 ya mwaka “B” wa Kanisa. Masomo yote matatu ya leo yanatupa na kutuelezea upendo wa Mungu unaojionyesha katika mfungamanisho wetu na Kristo. Hivyo, “tumeunganishwa na Kristo kwani yeye anayo maneno ya uzima wa milele.” Upendo huu wa Mungu na Imani yetu juu yake bila Kristo hakuna maana yoyote. Ukamilifu wa historia yetu ya wokovu unatimia kwa “tendo la neno kufanyika mwili na kukaa kwetu.” Huu ni upendo mkuu ambao Mungu kaufanya kwa watu wake.

Hivyo kwa kupitia mwono huu wa upendo wa Mungu kwa watu wake, Waisraeli hawapo tayari kumwasi Mungu na kuabudu miungu mingine. Nao wakasema, “tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao,” Yoh 24:16-17. Ndugu yangu unaonja upendo wa Mungu katika maisha yako ya kila siku? Je, únalo lolote la kumshukuru Mungu unapotazama historia yako kama wafanyavyo Waisraeli?

Upendo huu wa Mungu kwa watu wake yatupasa kuuona katika mambo yote yenye kutupeleka katika umoja wake, upendo wake, ushirikiano wake na hata katika maagano yetu katika maisha. Ni kwa kupitia umoja huo, upendo huo, na ushirikiano huo wa Mungu na mwanaye mpenzi, Yesu Kristo Mungu hujidhihirisha kwetu kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Upendo wa Mungu na mshikamano na mwanaye tunauona katika masakramenti yake, na hasa leo tunavyotafakari kwa ukaribu sakramenti hii ya ndoa. Naye Mtume  Paulo anasema, Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23. Hapa upendo wa Mungu kupitia Kristo mwenyewe unaonekana kwa utii huu wanaoishi wana ndoa, na hasa kwa mke kumtiii mumewe. Je, ndoa zetu leo ni salama? Akina mama mnaishi ukweli huu katika agano lenu la ndoa? Leo baadhi ya wanawake wamefikia kuwaita waume zao vyama chakavu. Je, hayo ndiyo makusudio ya Mungu na muungano wenu huo?

Kwa upande wa wanaume yawapasa kuwapenda wake zao katika kweli na haki. Upendo huu unafananishwa na upendo wa Kristo na Kanisa lake. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27. Wanaume zieshimuni ndoa zetu kwani ndio utakatifu wenu mnapoziishi katika kweli na haki. Wake zenu hawahitaji mambo ya pekee sana zaidi ya kuyasadifu yale wayatendayo kila siku katika familia. Tabia ya kuwaita wake zetu magoli kipa ni chukizo mbele ya Mungu. Muunganiko wenu ni makusudio ya Mungu, na ndivyo alivyoona inafaa.

Utii wa kweli si utumwa kwenu, bali ni ukamilifu wa makusudio ya Mungu katika maisha ya umilele. Wito wenu wa ndoa ni kuufikia umelele wa maisha yenu mlioandaliwa kupitia sakramenti hiyo. Hivyo, kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24. Ni kuwa na utii katika Kristo kwa sababu yeye anayo maneno la uzima wa milele. Ni kwa kupitia NENO huyu vyote vilifanyika, na kwa kupitia NENO huyu vyote huwa na uzima wa milele. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31. Tendo hili la ajabu katika sakramenti hii ya ndoa halimwesabii haki mmoja wa wanandoa kuwa na mambo yake ya pekee na binafsi tena. Hakuna msamiati huu tena wa kusema hiki changu na hiki chako. Kwa kufanya hivyo ni kuujeruhi mwili huu mmoja. Je, jambo hili lina ukweli katika ndoa yako? Je, ni mambo mangapi ya siri unayoyafanya bila kumuhusisha mwenzi wako wa ndoa? Je, hujui kwa kufanya hayo unaijeruhi ndoa yako? Ndugu yangu kama unaishi ukweli huu na kinyume cha sakramenti hiyo ya ndoa, elewa kwamba ndoa hiyo ishakufua katika uhalisia wa mambo na ukweli wa Kimungu. Kilicho baki ni maagizo kuu, na wote mmekuwa wasanii katika sakramenti hii Takatifu.

Wapendwa wana wa Mungu, hayo yote yanauzima yakiwa ndani na katika Kristo. Ni katika roho na siyo mwili yote upata uzima. Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,” Yoh 6:63. Ni kwa kupitia Kristo tunapewa Roho huyu wa Mungu kuyaishi yale yote kila mtu kadiri ya wito wake. Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 6:65. ‘Kristo ndiye njia, kweli, na uzima,’ Yoh 14:6.

Mafundisho haya ya Yesu kuhusu kujiachia kwake kunakoendana na wito wa kila mmoja wetu, yanakuwa mafundisho magumu sana kwani yanatuhitaji kujiachilia kwake kabisa. Yatupasa kuushinda ubinadamu wetu kila siku. Yesu anapowauliza kukata tamaa kwa wanafunzi wake na hivyo kurudi nyuma, Simoni Petro anajibu, “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69. Wapendwa Kristo anayo maneno ya uzima. Je, uzima wako unaupata wapi?


Tumsifu Yesu Kristo!

miércoles, 12 de agosto de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 19 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 19 YA MWAKA-B
13/8/2015
Somo: Yos 3:7-10a, 11, 13-17
Zab: 113
Injili: Mt 18:21-19:1
Nukuu:
Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu,” Yos 3:10

Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22 

TAFAKARI: “Hakuna uponyaji wa kweli pasipo msamaha.”
Wapendwa wana wa Mungu, ni ukweli kwamba katika maisha yetu tumeumizwa na kuwaumiza wengine. Kwa mantiki hii kila mmoja wetu anayomaumivu ya ndani. Ili kuponya maumivu haya ya ndani yatupasa kusamehe tukitambua pia katika maisha tuliwaumiza watu wengine pia. Injili ya leo inatuwasa kusamehe. Tendo hili si ombi ila ni amri ya Mungu mwenyewe. Sala yetu ya Baba yetu, inaeleza tendo hili la kusamehe kama sharti ya yale tuyaombayo kwa Mungu, “utusamehe sisi kama tunavyo wasamehe wale walio tukosea.” Mfano alioutoa Yesu kwenye Injili ya leo unaonyesha ni kwa namna gani yatupasa kuwa na utu wa kweli na kusamehe pasipo sharti. Pili, yatupasa kuishi na watu vizuri. Kwa kufanya tendo hilo, tutajua kweli ni nani tunayemtumikia na kumfuata. Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu,” Yos 3:10.

Je, kipimo cha kusamehe ni kipi? Mtakatifu Augustino anatuambia kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo. Hivyo basi, kipimo cha kusamehe ni kusamehe bila kipimo. Ni kwa mtazamo huu tunaona Yesu anamjibu Petro, alipotaka kujua ni mara ngapi yampasa kusamehe atakapokosewa. Yesu anamjibu Petro na kusema, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22. Ndugu yangu, unapotoa msamaha usihesabu uzito wa kile ulichokosewa, bali tazama huruma ya Mungu kwa yule unayemsamehe na fanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa. Samehe ukijua kuna mambo mengi tu Mungu amekusamehe ambayo kama ingeyafanya jino kwa jino usingekuwa jinsi ulivyo leo.

Hakika tusipowasamehe wale waliotukosea katika mtazamo wa Kimungu na wana wake tulioumbwa kwa sura na mfano wake, Mungu huyu tunayemwamini hatakuwa tayari kutusamehe makosa yetu. Yesu anaweka wazi ukweli huu anaposema, Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake,” Mt 18:35. Swala kubwa hapa ni hili, kwa nini tunaweka masharti katika kusamehe? Je, haitoshi kumsamehe mtu na kuacha neema ya Mungu kufanya kazi ndani yake? Je, hauoni kwa kufanya hivyo unajiweka huru na kumweka huru yule aliyekukosea?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU, HUKUACHA HATA MARA MOJA KUTUSAMEHE MAKOSA YETU. TUJALIE NEEMA YA MSAMAHA WA KWELI. AMINA

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 19 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 19 YA MWAKA-B
12/8/2015
Somo: Kum 34:1-12
Zab: 65
Injili: Mt 18:15-20
Nukuu:
Bwana akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko,” Kum 34:4

Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo,” Mt 18:15

Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru,” Mt 18:17

Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:19 

TAFAKARI: “Furaha ya Mungu tunapopatana na kuishi katika amani na upendo.”

Wapendwa wana wa Mungu, makusudi ya Mungu katika maisha yetu ni sisi sote tuishi kwa amani na upendo kama alivyotupenda yeye mwenyewe. Mungu kwa kumtuma mwanaye ulimwenguni alikuwa na makusudi hayo hayo ya kutupatanisha naye baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza. Pamoja na upendo huo wa Mungu Baba, bado tunaona kati yetu tunaishi kwa kutopendana na mbaya zaidi ndugu tuliozaliwa tumbo moja. Tunaishi kwa visasi na hata kutakiana mabaya.

Je, tufanyaje nini tunapokoseana kama ndugu? Yesu anatufundisha namna ya kufanya. Naye anasema hivi: Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo,” Mt 18:15. Ni vyema kama umekosana na ndugu yako mkayazungumza mkiwa naye na kupatana naye. Ni vyema mkayamaliza kama ndugu. Hamuitaji kuyakuza na kuwafaidia wengine kwa upungufu wenu. Kama hatakusikia na hayupo tayari kukusikiliza, Yesu anatupa nafasi ya pili. Naye anasema hivi: Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru,” Mt 18:17. Kanisa likiwa ndio mwili wa Yesu nasi tukiwa viungo vyake, ndiyo sehemu muhafaka wa kuyazungumza yale yote yaliyokwenda kinyuma na upendo wa Mungu. Je, tunatumia nafasi hii vyema kuyamaliza yale yanayotusibu? Kwa nini basi tunakimbilia mahakamani kwa mambo yetu ya familia? Je, tuupatapo ushindi huo wa kimahakama utatusaidia kuujenga tena ule undugu wetu ulioingia dosari? Ndugu yangu, tusipokuwa tayari kulisikiliza Kanisa tunahesabiwa kama watu wa mataifa.

Wapenda wana wa Mungu, yatupasa kuyamaliza mambo yote sisi wenyewe, na pale tunaposhindwa kufanya hivyo, basi tuliachie Kanisa litusaidie kufikia muhafaka wa matatizo yetu. Hapa ndipo penye furaha ya Mungu wetu aliye hai.Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:19. Je, unataka ushindi wa kidunia au upendo wa Mungu wako aliye hai? Patana na ndugu yako kindugu, naye Mungu atakuneemesha katika haki na kweli.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU USINIPE NAFASI YA KUISHI NA KISASI. AMINA

lunes, 10 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 19 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 19 YA MWAKA-B
11/8/2015
Somo: Kum 31:1-8
Zab: 32
Injili: Mt 18:1-5, 10, 12-14
Nukuu:
Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha,” Kum 31:6

akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3

Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4

Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee,” Mt 18:14

TAFAKARI: “Ajinyenyekeshaye mwenyewe ndiye aliye mkuu katika ufalme wa Mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu, unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote. Unyenyekevu unatudai kujifahamu mazuri na mapungufu yetu. Hivyo kukua kimwili na kiroho kuliko kwema na mpango wa Mungu, yaani maisha yenye malengo, kunahitaji sana fadhila hii ya unyenyekevu. Musa kwa kuongozwa na fadhila hii ya unyenyekevu, anajijua vizuri katika mazuri yake na mapungufu yake. Hivyo anasema, “Mimi leo ni mwenye miaka mia na ishirini; siwezi tena kutoka na kuingia, na Bwana ameniambia, Hutavuka mto huu Yordani,” Kum 31:2. Maneno haya ya Musa yanaonyesha unyenyekevu wake ulivyo, na hivyo haoni sababu ya kukwamisha malengo ya Mungu katika safari ya ukombozi. Ni wajibu wake kumkabidhi mwingine aendeleze kazi ile ya ukombozi. Je, ni mara ngapi unaupokea udhaifu wako ili kupisha kazi na matakwa ya Mungu? Yoshua anakuwa mrithi wa Musa. Ni mara ngapi tupo tayari kuachia ngazi na kuona uzuri kwa wengine ili waendeleze pale tulipoachia? Bila unyenyekevu wa kweli hatuwezi kuwa tayari kujipokea na kuwapokea wengine katika mazuri yao na mapungufu yao. Hivyo Mungu anatuwasa, Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha,” Kum 31:6. Mungu wetu ni UPENDO, na tunakuwa watoto wake tunapoishi upendo huo.

Injili yetu ya leo inatuzamisha zaidi katika fadhila hii ya unyenyekevu. Yesu anamfananisha mnyenyekevu na mtoto mdogo. Mwenye fadhila ya unyenyekevu mara zote hujiachilia kwa Mungu kila kitu, kama alivyo mtoto mdogo anavyojiachilia kwa wazazi wake. Kujiachilia huku kunatutoa woga na kutujaza ujasiri. Hivyo Yesu anatuambia hivi: “Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Ndugu yangu, fadhila ya unyenyekevu ni njia itupelekayo kwenye ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4. Kujinyenyekeza kwetu hakutupunguzii utu wetu bali kunatujengea utu huo kwa watu na zaidi, mbele ya Mungu. Unyenyekevu hautufanyi wajinga, bali ni shule ya kutuongezea maarifa ya kuishi kile tulichoitiwa kila mmoja kadiri ya wito wake. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee,” Mt 18:14. Unyenyekevu utupeleka kwa Baba. Kuishi fadhila hii ni tendo la kujisalimisha nafsi kuliko kwema.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUJALIE UNYENYEKEVU. AMINA

domingo, 9 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 19 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 19 YA MWAKA-B
10/8/2015
Somo: 2Kor 9:6-10
Zab: 111
Injili: Yoh 12:24-26
Nukuu:
Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6

Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:7

Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24

Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele,” Yoh 12:25

TAFAKARI: “Unaweza kutoa bila kupenda, ila huwezi kupenda bila kutoa.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunapotembea mabarabarani, tuwapo maofisini, tuwapo majumbani mwetu, tuwapo sehemu za starehe kama kwenye mahoteli na mabaa, tunakutana na omba omba wengi sana na kutokana na kero zao za kutuomba tunajikuta mara nyingi tunatoa bila kupenda. Tunafanya hivyo ili tuondokana na kero ile. Endapo tunafanya jambo hili kwa mtazamo huu, ni sawa na kupanda haba na matokea yake tutavuna hapa. Ni tendo la utoaji lisilo na neema ya Mungu ndani yake. Kwa upande mwingine tunapopenda kweli basi hatuachi kutoa.

Furaha ni kama kikohozi huwezi kukizuia. Upatwapo na kikohozi itakulazimu kukohoa tu. Tendo hili ni sawa na pendo la kweli. Pendo la kweli litakulazimu kutoa bila kujibakiza. Huku ndiko kule kupanda kwa ukarimu kunakotupelekea kuvuna kwa ukarimu. Hivyo Mtume Paulo anasema, “Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6. Kupata neema na baraka za Mungu, ni kulitenda jambo hilo pasipo kulazimishwa na wala si kwa huzuni. Tunafanya kwa upendo wa kweli tukimtazama Yesu Kristo kama kielelezo chetu. Hivyo, kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:7. Je, mtazamo wako wa utoaji upoje?

Injili ya leo inatuzamisha zaidi katika tendo hili la kujitoa kwa ajili ya wengine. Ukweli ni kwamba huwezi kujitoa bila kujibakiza ukabaki katika hali ile ile. Tendo hili la kujitoa bila kujibakiza linatubadili mwono wetu na mfumo mzima wa maisha. Je, Yesu ana maana gani anaposema, “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Ndugu yangu, ni katika kufa tunapata uzima, na, ni katika uzima yatupasa kufa ili uzima ule uendelee siku kwa siku na milele yote. Fumbo hili na mfano huu wa chembe ya ngano Yesu anautoa akionyesha ni kwa mauti gani ataufia ulimwengu ili kuupa uzima wa milele hasa kwa wale wanaomwamini. Vile vile kwa fumbo hili na mfano huu wa chembe ya ngano Yesu anatutaka tuwe mfano kwa maisha tunayoishi kadiri ya wito wa kila mmoja wetu.

Wapendwa tukichukulia maisha ya familia, Baba huleta uzima katika familia yake anapojitoa kabisa na bila kujibakiza. Kwa kufanya hivi mke wake anaongezeka na watoto pia. Ni kwa namna hiyo hiyo Mama katika familia anapojitoa kabisa na bila kujibakiza analeta uzima katika familia yake kwa Mume wake kuongezeka na watoto pia. Kwa upande wa watoto huleta uzima katika familia kwa kutimiza nyajibu zao, mfano, kusoma vizuri na kwa bidii na kutumia rasilimali fedha vizuri ili kesho wawe furaha na matumaini kwa wazazi wao. Mfumo wa maisha haya ni sawa na mshumaa unaotoa mwanga huku ukifa kwa kuyeyuka. Nami kama Mtawa na Padre, yanipasa kufa kila siku ili pale nilipo pawe na uhai wa kweli. Nakufa kila siku kwa kutimiza wajibu wangu vyema. Huku ni kuichukia nafsi yako kwa ajili ya uzima wako na wale walio wako na chini yako. Hivyo Yesu anasema,Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele,” Yoh 12:25. Je, maisha yako na majitoleo yako yanamatokeo ya uzima wa milele?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIJALIE NEEMA YA KUJITOA BILA KUJIBAKIZA. AMINA

sábado, 8 de agosto de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 19 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 19 YA MWAKA-B
9/8/2015
Somo I: 1Fal 19:4-8
Zab: 33:2-9
Somo II: Efe 4:30-5:2
Injili: Yoh 6:41-51

Nukuu:
“Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu,” 1Fal 19:4b

Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule,” 1Fal 19:5

Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi,” Efe 4:30

tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi,” Efe 4:32

Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato,” Efe 5:1-2 

Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44

“Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu,” Yoh 6:45b

Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima,” Yoh 6:47-48

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51

TAFAKARI: “Kristo yu hai na chakula atoacho Yesu ni mwili wake, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Usife Moyo, tunaye atupiganiaye daima.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa ana adhimisha Dominika ya 19 ya mwaka “B” wa Kanisa. Masomo yote matatu ya leo yanatuelekeza njia ya kufuata, na sababu ya uzima wetu. ‘Ni kweli kwamba kifo cha nyani miti yote huteleza.’ Ila kwa upande wetu, na hasa tunaomwamini Kristo, msemo huu ‘kifo cha nyani miti yote huteleza,’ hauna mashiko. Ni kwa imani thabiti Eliya anajiachilia mikoni mwa Mungu alipofikia mkwamo wa matumaini yake yote na kupata jibu hapo hapo. Maandiko matakatifu yanatuambia, Eliya “Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu,” 1Fal 19:4b. Kujiachia huku kwa Nabii Eliya kunamfanya kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule,” 1Fal 19:5. Ndugu yangu katika Kristo, ‘pasipo njia Mungu ufanya njia.’ Je, waamini jambo hilo?

Ndugu yangu, katika Injili ya leo Mungu yule aliyekuwa mbali sana na wanadamu, ndiye leo Emanueli, yaani ‘Mungu pamoja nasi.’ Ni kwa kupitia fumbo zima la kumwilishwa kwa neno, sote leo kwa kuamini neno huyu wa Bwana tunapata uzima wa milele. Hivyo tangia sasa, Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, (Yesu Kristo) asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44. Uzima wetu leo bila Kristo haiwezekani. Je, mafundisho haya ya Yesu yanasema jambo lolote juu ya maisha yako? Je, ni jambo gani linalokupa uzima leo na sasa? Vipi basi kuhusu maisha yako ya umilele? Je, ni cheo chako leo? Je, ni utajiri wako leo? Je, ni akili zako leo? Je, ni mafanikio yako kitaaluma leo? Ndugu yangu, Yesu anatuambia hivi: “Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu,” Yoh 6:45b. Tunajifunza kwa Baba yetu aliyembinguni haya yafuatayo: Upole, Unyenyekevu, uaminifu, utii, Upendo wa kweli, na zaidi huruma yake.

Msingi wa ufahamu wote wa elimu kuhusu Mungu upo kwenye Imani ya kweli. Kuamini yote aliyotufundisha Kristo na kuyaishi. Kumchukua Kristo katika kweli na haki, na siyo kama tukio la kihistoria ambalo lilikuwa hai wakati fulani tu katika historia yake. Yesu yu hai jana, leo na milele yote. Naye anasema, Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima,” Yoh 6:47-48. Pamoja na kwamba uzima wetu wa leo na sasa wawezwa kusogezwa kwa chakula hiki tukiangaikiacho na kinachoharibika, Yesu tu ndiye chakula cha uzima. Chakula cha uzima ni kile kilichoshuka kutoka mbinguni, yaani neno aliyefanywa mwili, KUMWILISHWA. Huyu ndiye Kristo tunayemwamini na kumfuata. Yesu mwenyewe anasema, Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51. Je, natambua ukweli huu ninaposhiriki mwili na damu ya Yesu? Au huwa nayapokea maumbo haya ya mke na divai kwa mazoea tu? Je, napokea mwili na damu ya Yesu katika hali safi? Je, ni kitu gani kinachonizuia kumpokea Kristo na kujazwa uzima wake? Kwa nini basi nakumbatia vikwazo na kukosa uzima huu wa milele? Nitajifungia hadi lini kwenye gereza hili la kiroho? Kwa mtindo huu nayapenda kweli maisha yangu? Ndugu yangu ambaye upo kwenye kifungo hiki chukua hatua na fanya mabadiliko juu ya maisha yako.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, kutokuishi ukweli huu ni kumuhuzunisha Roho Mtakatifu. Huyu ndiye anayetufunulia siri zote kuhusu ufalme wa Mungu, kutuongoza na kututakatifuza katika kweli na haki. Hivyo,msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi,” Efe 4:30. Kwa ubatizo wetu, kuimarishwa kwetu, na kwa kuwekwa wakfu kwetu kama makleri tunatiwa muhuri huu wa Roho Mtakatifu hata siku ya ukombozi wetu. Je, ndugu yangu, unaishi ahadi zako za ubatizo? Je, wasimama hodari kama askari wa Kristo kwa sakramenti yako uliyopokea ya KipaImara? Je, upo tayari kuufia ukweli kama Kristo kwa maisha yako ya wakfu kama mtawa na mkleri? Hapa ndipo penye changamoto yetu ya Imani kila mmoja wetu kadiri ya wito wake. Tusisahau kuwa wote tunaitwa katika utakatifu ambao ndicho cheo chetu.

Wapendwa wana wa Mungu, kuishi cheo hicho, yaani UTAKATIFU tulioitiwa yatupasa kuishi mfumo huu wa maisha, yaani, kama asemavyo Mtume Paulo, tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi,” Efe 4:32. Msamaha wa kweli ni uthibitisho wa kile tunachokiishi na kukiamini kuhusu Kristo. Kristo pamoja na kuwambwa pale msalabani hakuacha kutoa msamaha. Jambo la pili ni kuishi maisha ya Upendo kama wana wa Mungu. Upendo usiobagua kabila, rangi, ukanda, na wala utaifa. Sote kwa upendo na huruma ya Mungu tumekuwa kama tulivyo na ilivyompendeza Mungu. Utofauti zetu ndio uzuri wa Mungu. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato,” Efe 5:1-2. Ndugu yangu, mimi na wewe tunayokazi moja tu hapa duniani. Nayo ni kumtafuta Mungu kila siku ya maisha yetu. Mungu huyu na Yesu huyu tunakutana naye nyumbani mwetu, kazini mwetu, mabarabarani tunamopita na zaidi katika fumbo la mwili na damu yake. Hapa ndipo penye uponyaji wa kweli.

Wengi wetu kama alivyo Mama Christina, tumejiwekea nidhamu ya kiroho ya kwenda kila siku asubuhi Ibada ya  Misa Takatifu, na tunaona bila kufanya hivyo twamkosea Mungu sana. Lakini mara nyingi tunasahau kuwa Mungu huyu, na Kristo huyu yupo kwa namna tofauti tofauti na tunapishana naye tunapoelekea huko Makanisani.

Mama Christina siku moja alijidamka mapema asubuhi kuwahi misa za wiki kama iliyokuwa ada kwake. Alipofika mlango kuu wa Kanisa lile alikutana na maneno haya; “LEO SIPO HAPA UMENIACHA NYUMBANI KWAKO.” Mara ile mama yule alishtuka na kuanza kujiuliza “kulikoni maneno haya?” Katika tafakari ile alikumbuka jambo hili. “Jana yake alipotoka kazini mfanyakazi wake alimwambia hali yake ni mbaya sana na anahisi ana malaria. Christiana hakufanya lolote, wala kumsikiliza. Hivyo alidai atengewe maji ya kuoga na amechoka sana. Hivyo aliwaza kuhusu kesho kudamka na kwenda Kanisani.”

Ndugu yangu, Mara nyingi Mungu wetu na Yesu wetu tunayemfuata tunamwacha majumabani mwetu, au kupishana naye barabarani tunapoelekea Makanisani.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUPE UZIMA WAKO ILI TUUONE PIA KWA WALE TUNAOKUTANA NAO KILA SIKU. AMINA.