jueves, 5 de septiembre de 2019

TAFAKARI: JUMATATU YA WIKI YA 23 YA MWAKA-I


JUMATATU WIKI YA 23 YA MWAKA-I

Somo: Kol 1:24-2:3
Zab: 62:6-7, 9
1.     Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana. Kwa Mungu wokovu wangu, Na utukufu wangu; Mwamba wa nguvu zangu, Na kimbilio langu ni kwa Mungu.
(K) Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.
2.     Hakika binadamu ni ubatili, Na wenye cheo ni uongo, Katika mizani huinuka; Wote pamoja ni hafifu kuliko ubatili. (K)
Aleluya: Yoh 10:27
Kondoo wangu waisikia sauti yangu;
nami nawajua, nao wanifuata.
Injili: Lk 6:6-11
Nukuu:
“Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika,” Kol 2:1-3.
“Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Lk 6:9.
“Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Lk 6:10.
“Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu,” Lk 6:11.
TAFAKARI: “…Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika,” Kol 2:1-3.
Wapendwa wana wa Mungu, ni vyema tukajiuliza swali hili kabla ya kuzama ndani zaidi katika tafakari yetu ya leo. Kwa nini Kristo awe sababu ya kila kitu katika maisha yetu? Jibu tunalipata kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume, Sura ya nne, mstari wa kumi na mbili. Tunasoma hivi, “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Ni katika msingi huu wa kila kitu ndani na katika Yeye-Christocentric, Mtume Paulo haoni haya kusema kwamba, … sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo,” Kol 1:24. Mkristo bila Kristo ni ujasiri wa samaki kuishi JANGWANI. Mwisho wa ujasiri huu ni haki ya kifo pasipo shaka.
Mtume Paulo haona hasara ya kukosa yote na kumpata Kristo kama fahari yake, Gal 6:14. Nguvu ya Mtume Paulo katika misioni yake yote ina msingi ndani na katika Kristo Yesu. Kwa maantiki hiyo, Paulo anasema, “Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu,” Kol 1:29. Je, wewe na mimi tunao ujasiri huo kama wafuasi wake Kristo hasa pale tunapopatwa na sintofahamu katika imani yetu? Je, twafanya juhudi yoyote tunapolemewa na upinzani hasa kutoka kwa wampingao Kristo? Mtume Paulo anataka wewe na mimi tuufahamu ukweli huu kama alivyowaambia Wakolosai:-“…nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika,” Kol 2:1-3. Je, bila Kristo waweza toboa mbingu? Ewe uliye mfuasi wa Kristo, na mwenye kumwamini Kristo, bila Kristo u mwepesi kuliko karatasi.
Tukizama zaidi katika Injili ya leo tunaelewa kweli hii; Kristo anatutaka tuwe na uhai, na tena tuwe nao tele. Kristo Yesu ndiye Njia, kweli, na Uzima wetu, Yoh 14:6. Kristo akiwa ndiye Mchungaji mwema wa kondoo zake, anajitofautisha na mwivi mwenye nia ya kuiba na kuwachinja kondoo. Katika hili Yesu anasema, “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:10-11. Ni kwa namna hiyo ya uchungaji mwema, na akiwa katika sinagogi akifundisha siku ya sabato, Yesu anakutana na mtu aliyepooza mkono, Lk 6:6. Huyu ni kondoo wake na mwenye kuhitaji uponyaji. Kwa upande wa pili, Mafarisayo walioishikilia sheria ya sabato hasa kutokufanya kazi, wanamtega Yesu waone atakachofanya ili wawe na sababu ya kumtia hatiani, Lk 6:7. Watu hawa hawana nia ya kuutokomeza uovu, bali kuuridhia na kuushabikia uovu kwa manufaa yao binafsi.
Pamoja na hali na mazingira hayo Yesu anasimamia mafundisho sahihi juu ya Upendo wa Mungu, na kuuvunja ukimya ule wa uovu. Na ndivyo alivyo yatambua “mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama,” Lk 6:8. Huu ndio ujasiri wa Mkristo hai na mwenye kuiona kweli, kuisema kweli, na kuisimamia kweli. Na baada ya kuiona kweli, kuisema kweli, na kuisimamia kweli, “ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?” Lk 6:9. Swali hili la Yesu limebeba mafundisho ya kweli kuhusu huruma na upendo wa Mungu.
Lengo la Yesu hapa ni kuziamsha kama sio kuzifufua dhamiri zao zilizokuwa zimekufa. Aulizalo Yesu kwa Mafarisayo anakuuliza wewe na mimi pia. Na mwisho katika kuisimamia kweli kisawa sawa, Yesu “akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Lk 6:10. Na hili ndilo anguko lao wale wauridhiao na kuushabikia uovu, “wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu,” Lk 6:11. Mwisho wa chuki ni aibu! Leo wengi wetu kadiri ya itikadi zetu za dini, siasa, mila na desturi zetu yawezekana tukatendeana ndivyo sivyo. Lakini elewa ndugu yangu ‘mwisho wa chuki ni aibu’ kwani KWELI usimama mahali pake hata kama utaipindisha kwa wakati kadiri ya nafasi na ushawishi uliokuwa nao katika jamii.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu,” Kol 1:29.
Tusali:-Ee Yesu, tufanye vyombo vyako vya haki, kweli, Upendo na Amani. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario