jueves, 5 de septiembre de 2019

TAFAKARI: JUMAMOSI YA WIKI YA 22 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 22 YA MWAKA-I
Somo: Kol 1:21-23
Zab: 54:2-3, 5 na 7.
1      Ee Mungu, uyasikie maombi yangu, Uyasikilize maneno ya kinywa changu. Kwa maana wageni wamenishambulia; Watu watishao wananitafuta nafsi yangu; Hawakumweka Mungu mbele yao.
(K) Bwana ndiye msaada wangu
2      Atawarudishia adui zangu ubaya wao; Uwaangamize kwa uaminifu wako. Kwa kuwa limeniokoa na kila taabu; Na jicho langu limeridhika Kwa kuwatazama adui zangu. (K)
Injili: Lk 6:1-5
Nukuu:
Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake,” Kol 1:21-22a.
“Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato,” Lk 6:5.
TAFAKARI: “Kristo katuweka huru, hivyo tusimame katika kweli kila siku.”
Wapendwa wana Mungu, Kristo katuweka huru, hivyo tusimame katika kweli kila siku. Kusimama katika kweli ni kuthamini na kuishi kweli ya Mungu na kuwa na hofu yake. Hofu ya Mungu tuliyonayo msingi wake ni upendo wa Mungu hasa kwa kumtoa mwanaye mpenzi kama sadaka, na kututoa kutoka utumwa wa dhambi. Ukombozi wetu ni wa gharama kubwa sana. Je, wauthamini Ukristo wako kwa kuishi Imani ya kweli? Mtume Paulo anatukumbusha habari hii kwa kusema, “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake,” Kol 1:21-22a.
Ni kwa mantiki hiyo hapo juu kwamba Kristo ndiye kielelezo cha yote yale tuyafanyayo ili tuurithi ufalme wa Mbingini tulioandaliwa na kuutamani. Je, yale yote niyafanyayo leo na sasa yanaendana na sadaka ya Yesu pale msalabani? Yesu anataka Wayahudi, na wewe na mimi tuelewe kwamba yale tuyafanyayo yaendane na thamani ya upendo wa Mungu kwetu, na Yeye, yaani Kristo ndiye msingi wa vyote. Kristo akiwa msingi wa maisha yetu na sababu ya yale yote tuyafanyayo, basi tutakuwa huru kweli kweli kwa sababu tutajua ni nini tunayemtumikia. Hivyo Yesu anawaambia Wayahudi “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato,” Lk 6:5. Kristo ndiye mizania ya kweli kuhusu Mungu tunayemwamini na kumwabudu. Kristo ndiye anayejua siri ya ufalme wa Mungu, na kwa kupitia Yeye nasi tunafunuliwa siri hiyo. Ndugu yangu Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato,” Lk 6:5.
Tusali:-Ee Yesu kwako tu huru.

No hay comentarios:

Publicar un comentario