jueves, 5 de septiembre de 2019

TAFAKARI: JUMANNE YA WIKI YA 23 YA MWAKA-I


JUMANNE WIKI YA 23 YA MWAKA-I

Somo I: Kol 2:6-15
Zab: 145:1b-2, 8-9, 10-11
1.     Nitalihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele.
(K) Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
2.     Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K).
3.     Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. (K).
Aleluya: Yoh 15:16
Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi;
nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa;
ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.
Injili: Lk 6:12-19
Nukuu:
Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye,” Kol 2:6.
“wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani,” Kol 2:7.
“Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume,” Lk 6:13.
“Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:14-16.
TAFAKARI:Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye,” Kol 2:6.
Wapendwa wana wa Mungu, imani ‘sio jambo la kujaribu na kuona tokeo lake’ kama wesemavyo wenzetu, ‘try and error.’ Wala imani sio tokeo la ‘faida katika shaka.’ Bali imani ni “…kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1. Kristo Yesu ni hakika ya mambo yatarajiwayo, Yoh 14:6. Ni katika mazingira haya Mtume Paulo anasisitiza jambo hili, “…kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye,” Kol 2:6. Ukimpata Kristo katika maisha yako umepata vyote. Kwa maana nyingine, “wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani,” Kol 2:7. Na moyo usio na shukrani ukausha mema yote.
Jambo la kujiuliza ni hili, kwa nini wewe uliye batizwa na kukiri imani ndani na katika Kristo unatangatanga? Nabii Yeremia anatukumbusha jambo hili, “…Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5. Ni katika mazingira haya Mtume Paulo anasema, “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Leo tuutazamapo ulimwengu wetu tunaona baadhi ya watu wakijiinua na kumweka Mungu katika mifuko yao na wao kuwa miungu watu.
Ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, ni katika Kristo tu kuna “…utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili,” Kol 2:9. Mengine yote yatokayo kwa mwanadamu ni mbwembwet tu. Wewe na mimi tumetimilika “…katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka,” Kol 2:10. Bila Kristo Yesu kujikweza kwako ni kupotea muda bure! Ukweli ni kwamba, ‘katika yeye tumetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo,’ Kol 2:11. Ni katika Kristo na ndani yake tumezikwa katika ubatizo, tumefufuliwa naye katika wafu, kuwa washindi kwa kufanywa hai pamoja naye akiisha kutusamehe makosa yetu, na kuwa wajasiri katika msalaba wake ambao ndio utukufu wetu kama wakristo, Kol 2:12-15. Na ndio maana twasema hakuna ‘utukufu pasipo msalaba wake Kristo.
Yesu Kristo kama kiongozi wetu na aliyeishi kile alichokisema, ili kutimiza hazma ya kile alichokijia, yaani, kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi, aliyaweka yote wazi tangu mwanzo. Na kauli mbiu yake kama dira ya kila mmoja kufuata ili kufika kule alikotaka sote tufike, yaani, uzima wa milele ni hii,“Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Kwa maana nyingine, huruma na neema ya Mungu hufanya kazi yake pale tunapoipokea huruma na neema hiyo kwa kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi.
Na hata baada ya kutoa kauli mbiu yake hiyo, Yesu alionyesha wazi mpango kazi wake mwanzoni kabisa kabla ya kufanya chochote. Na mambo yalikuwa hivi; “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:16-19. Mpango kazi mzima wa Yesu hauna uchochezi wa aina yoyote ile, wala vitisho. Ni habari njema kweli kweli na iliyojaa matumaini.
Baada ya kutoa mpango kazi wake, Yesu akiwa Mungu na Mwanadamu, alihitaji watu wa karibu naye ili kuitenda kazi ile aliyoijia kama tulivyoona hapo mwanzo. Kuwapata watu hawa, Yesu hakukurupuka, bali aliyaweka yote mikononi mwa Baba yake aliye mtuma. Hivyo, “Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu,” Lk 6:12. Ni baada ya maombi haya, Yesu anawachagua wanafunzi wake. Na “hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume,” Lk 6:13. Hawa ndio wale Thenashara-Mitume kumi na wawili, Mt 10:2-5, yaani, “Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:14-16.
Hawa Thenashara ndio waliokuwa wasaidizi wake wa karibu katika kutimiza lile alilolijia yaani, kukuweka wewe na mimi huru kutoka utumwa wa dhambi. Na hawa Thenashara, “akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi,” Lk 9:1. ‘Aliwapa mamlaka’ ikimaanisha uhuru wa kufanya yale yampendezayo Mungu. Katika kweli hii, Yesu aliruhusu ubunifu katika utendaji kila mmoja kadiri ya karama zake. Hakika Kristo Yesu ni Kiongozi kweli kweli, na mfano kwetu ulio hai. Tujifunze kwake.
Baada ya kufanikisha mpango huu, ikiwa ni pamoja na kuweka wazi kauli mbiu yake, Mk 1:15, mpango kazi wake, Lk 4:16-19, na kuwachagua watu wake wa karibu, yaani, Thenashara, Lk 6:14-16, alianza mara moja kazi ile aliyoijia. Hivyo “waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote,” Lk 6:17b-19. Yesu kamwe hakupoteza muda wake kupambana na watesi wake. Kwa maana nyingine, Yesu hakuwa na muda wa kupoteza kupambana na wapinzani wake; Mafarisayo, Waandishi, na Wazee, bali aliutumia muda wake wote wa miaka ile mitatu kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mbinguni. Matokeo ya kazi yake ni uwepo wa wewe na mimi leo kama Wakristo na wafuasi wake wenye hofu ya Mungu. Ni wajibu msingi kwa matiki hiyo kwamba wewe na mimi yatupasa kuwa mawakili wa Kristo pale tulipo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote,” Kol 2:13.
Tusali:-Ee Yesu mwema, nifanye wakili wako wema pale nilipo kila kadiri ya wito na karama ulizonijalia. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario