ALHAMISI WIKI YA 22 YA MWAKA-I
Somo: Kol
1:9-14
Zab: 98:
2-3ab, 3cd-4, 5-6
1
Bwana
ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. Amezikumbuka
rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Bwana ameufunua wokovu
wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
2
Miisho yote
ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni
sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
3
Mwimbieni
Bwana zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi. Kwa panda na sauti ya
baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
Injili:
Lk 5:1-11
Nukuu:
“mwenende
kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila
kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu,” Kol 1:10.
“Naye
alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa
Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol
1:13-14.
“Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka
mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4.
“Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya
kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,”
Lk 5:5.
“Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu,
akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8.
“Yesu
akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b.
TAFAKARI: “Kama ushakutana na Kristo katika Maisha yako lazima akubadili
mwenendo wako.”
Wapendwa
wana wa Mungu, yawezekana hadi leo licha ya kuingizwa katika urika wa wana wa
Mungu na warithi wa ufalme wake kwa sakramenti ya ubatizo, bado haujawahi
kukutana na Kristo katika maana ya kuguswa kuliko ndani kabisa ya maisha yako.
Tunakutana na Kristo pale tu tunapoanza kuyachukulia maisha yetu na ufuasi wetu
kwake kwa namna iliyo hai na ya kuguswa kwa yale yote tuyafanyayo ndani na
katika Kristo Yesu. Mara tuifikiapo hatua na hali hii, tendo hili haliwi tena
tendo au swala la kihisia, hadithi au simulizi fulani la kufikirika, bali
maisha halisi.
Ndugu
yangu, maisha halisi ndani na katika Kristo yanatuwajibisha kwa kila namna,
tunapendezwa nayo, maisha hayo huzaa matunda mema, na mwisho maisha hayo
utuongezea ufahamu juu ya Mungu. Ni kwa mantiki hii Mtume Paulo anawasihi
Wakolosai nasi pia kwamba, “tuenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana,
mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika
maarifa ya Mungu,” Kol 1:10. Tunawajibika kuuona ukweli huu tunapopima uzito wa
dhambi na wokovu aliotupatia Kristo kwa sadaka ya Kifo chake pale msalabani.
Hakika ni upendo mkubwa sana kwetu wanadamu. Kristo ndiye pekee anayetuweka
huru kutoka nguvu za giza na kutuingiza katika ufalme wa Mungu kwa pendo lake,
kwa sababu ni kwake tu kwenye ukombozi na msamaha wa dhambi zetu. Hivyo Kristo,
“alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa
Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol
1:13-14. Je, ndugu yangu una sababu yoyote ya kuacha kumsamehe mwenzako kwa
vigezo vyovyote vile ulivyo navyo?
Ukristo na ufuasi wangu kwake una maana gani ninapotazama tendo hili la
msamaha? Nisipobadilika katika tendo hili hakika bado sijakutana na Kristo Yesu.
Ndugu
zangu, mahangaiko katika maisha yetu ya kila siku yasiwe ukuta wa kutokuona
uwepo na nguvu ya Kristo Yesu ndani ya yale tuyafanyayo hata kama tunauzoefu
nayo. Kama kweli wasadiki Kristo ndiye Mwokozi, basi ni kwa namna hiyo hiyo
huyaweza yote yaliyo chini ya miguu yake kwa sababu, “amevitia vitu vyote chini
ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa;
ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,”
Efe 1:22-23. Yesu Kristo analiweka jambo hili hadharani anapowakuta Simon Petro
na wenzake waliokuwa mahodari wa kuvua samaki usiku kucha bila kupata chochote.
Naye Yesu anamwambia Simoni, “Tweka mpaka
kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4. Kwa maana nyingine Yesu
anamwambia Simoni Petro kwamba “jaribu tena pasipo kuwa na shaka na urushe kete
yako ya mwisho katika ukamilifu wote.” Maneno haya ya Yesu yanamtia shaka
kidogo Simoni Petro kutokana na uzoefu aliokuwa nao katika kuvua samaki. Hata
hivyo Simoni anamwamini Yesu pasipo shaka na kufanya alivyoagizwa. Hivyo, “Simoni
akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha,
tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” Lk 5:5. Ndugu zangu,
“ni kwa neno lake Yesu, Simoni Petro anazishusha nyavu.” Ni kwa njia ya neno
Mungu aliumba ulimwengu kutoka utupu. Hivyo ni kwa neno hili: “Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh
1:3-4. Je, bado unamashaka na Neno wa Mungu, yaani Yesu Kristo?
Muujiza
wa wingi wa samaki uliotokana na hali isiyoyakawaida kadiri ya ufahamu aliokuwa
nao Simoni juu ya uvuvi unamfanya akutane na Kristo katika maisha halisi na
kujiona alivyo kiroho. Hapa ndipo pale tunaposema kwamba unapokutana na Kristo
ndani na katika Yeye lazima akubadilishe. Kubadilishwa kwa Simoni kunajionyesha
katika hali ya dhambi iliyoisuta nafsi yake. Hivyo katika mguso huu, “Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa
Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk
5:8. Je, ninapokutana na matendo makuu ya Mungu katika maisha yangu nauona
udhaifu wangu? Je, matendo hayo makuu ya Mungu ni mastahili yangu yanayotokana
na mafanikio yangu na juhudi zangu bila mkono wa Mungu?
Wapendwa wana wa Mungu, tunapokutana na Kristo katika
uhalisia wa maisha yetu ya kila siku, hali hiyo hughubikwa na hofu kubwa kwa
sababu tunajiona kama tulivyo kwani Kristo huwa kioo cha kujitazamia nafsi na
roho yetu. Tupatapo hali hiyo, tusisahau kuwa Yesu anatuambia kama alivyo mwambia
Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b. Maana yake yake,
“usihofu kwani ninakuandaa kwa makubwa zaidi ya hayo niliyokutendea.” Mungu
wetu mara zote utuwazia mambo makubwa zaidi ya yale tuyafanyayo kila siku, na
neema na baraka anazotujalia pasipo mastahili yetu, Yer 29:11.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Simoni
akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha,
tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” Lk 5:5.
Tusali:-Ee Yesu, matendo yako kwangu ni ya ajabu sana! Utukuzwe na
kuheshimiwa milele. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario