JUMAPILI
YA 23 YA MWAKA-C
Somo
I: Hek 9:13-18
Zab/Kit: 90:3-4, 5-6, 12-13, 14, 17
1. Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu. Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku
ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu Kizazi baada ya
kizazi
2.
Wawagharikisha,
huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika
na kukauka. (K)
3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa
hekima. Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie
watumishi wako. (K)
4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na
kufurahi siku zetu zote. (K)
5. Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya
mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)
Somo
II: Flm 9-10, 12-17
Injili:
Lk 14:25-33
Nukuu
“Ni mtu yupi awezaye
kulijua shauri la Mungu? Au ni nani atakayeelewa na mapenzi yake?” Hek 9:13
“Kwa kuwa mawazo ya
mwanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa,” Hek 9:14
“lakini, kwa ajili ya
upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa
Kristo Yesu pia,” Flm 9.
“Nakusihi kwa ajili ya
mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye
mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya
Injili,” Flm 10, 13.
“Kama mtu akija kwangu
naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake
waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi
wangu,” Lk 14:26.
“Mtu ye yote
asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,”
Lk 14:27.
“Basi,
kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi
wangu,” Lk 14:33.
TAFAKARI:
“Asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 23 ya mwaka “C” wa Kanisa.
Wazo kuu la leo kadiri ya masomo yetu ni juu ya upendo wa dhati ambao ni
SADAKA. Upendo wa kweli ni sadaka kwa sababu unakulazimu kutoa bila kujibakiza.
Kwa hali na mazingira fulani unaweza kutoa bila kupenda. Na unafanya hivyo
kuondokana na karaha au usumbufu fulani, rejea habari ile ya kadhi asiye mcha
Mungu, wala kujali watu, na mjane yule aliyekuwa anadai haki yake, Lk 18:1-5.
Kwa upande mwingine huwezi kupenda bila kutoa. Na huwezi kama kiongozi
kuwatumikia watu kama huwapendi. Na hapa ndipo tunapoona upendo wa dhati ambao
ni Sadaka. Na “kabla ya sikukuu ya Pasaka,
Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda
kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh
13:1. Na “hakuna aliye na
upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,”
Yoh 15:13. Hii ndiyo sadaka kama tunda la upendo wa dhati.
Ni wazi wewe na mimi
kila mmoja anayo mapungufu yake. Hakuna aliye kamilika kwa kila kitu, na hii
ndiyo hali yetu itokanayo na ubinadamu wetu. “Ni
mtu yupi awezaye kulijua shauri la Mungu? Au ni nani atakayeelewa na mapenzi
yake?” Hek 9:13. Kutokana na udhaifu huu
twaitaji neema ya Mungu kuushinda ubinadamu wetu kuelekea ukamilifu kama Mungu
alivyo mkamilifu, Mt 5:48. “Kwa kuwa mawazo ya mwanadamu yana woga, na
makusudi yetu yanaelekea kushindwa,” Hek 9:14. Kwa neema ya Mungu, na sisi
tukijibiidisha kuushinda ubinadamu wetu tuifikie ile mede ya dhahabu ya mwito
mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu, Flp 3:14. Tunaitaji neema ya Mungu katika
hatua hii pia kwa sababu “mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na
kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbufu,” Hek 9:15.
Pamoja na hitaji hilo
la neema ya Mungu kukabiliana na yale yaliyopita nguvu na ufahamu wetu kama
wanadamu, twahitaji Roho Mtakatifu kama upendo wa Mungu Baba na Mwana. Roho
huyu ni alama ya Umoja na Upendo ndani yetu na wale wanaotuzunguka. Roho huyu
utusaidia kuyapembua yaliyo ya Mungu na wanadamu. Ndugu yangu, “Naye ni yupi
aliyeyavumbua mashauri yako, isipokuwa ulimpa Hekima na kumpelekea Roho yako
takatifu kutoka juu?” Hek 9:17. Ni kwa neema za Mungu na Roho wake Mtakatifu
utuwezesha kuufikia ule upendo sadaka.
Pendo Sadaka linaelezwa
vizuri na kwa undani katika Injili yetu ya leo. Yesu anatupatia mapaswa ya
ufuasi wetu kwake, na pendo sadaka tutakalo paswa kutoa. “Kama mtu akija kwangu
naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake
waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi
wangu,” Lk 14:26. Kumbe kuwa mwanafunzi wa Kristo ni kumpenda kwa dhati Kristo
kule kuliko kwa kwanza. Tuelewe Kristo hasemi tusiwapende wazazi wetu na ndugu
zetu. La hasha! bali Yeye Kristo apewa nafasi ya kwanza. Tunampa Kristo nafasi
ya kwanza kwa sababu hii kubwa, naye anasema, “Mimi
ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh
14:6. Wazazi wetu, ndugu, jamaa na marafiki zetu wanamwitaji Kristo kwa
kuwa ndiye njia halisi, kweli kamili, na uzima wa milele ili kumfikia Baba yetu
wa Mbinguni. Ni nani basi kati yetu asiyehitaji huruma na upendo wa Mungu?
Pendo hili ni sadaka
kwa sababu linakutaka pia ujiachie mikononi mwa Kristo na kuachana na yale yote
yanayo ipa heri na matumaini nafsi yako. “Basi, kadhalika kila mmoja wenu
asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk 14:33. Huku
ndiko kujikana nafsi. Moja ya mambo makubwa ya kujikana nafsi ni kuzishika
vyema na kwa ukamilifu na uaminifu amri za Mungu na neno lake. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Mtu
asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu,
ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:15, 24. Ndugu yangu unayesafiri nami
kati tafakari hii, kuzishika amri na neno la Mungu kwa kupenda bila shuruti
ndiko kuuchukua msalaba wa Yesu na kumfuata. “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba
wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk 14:27. Na tu
wanafunzi wa Yesu kama tunapendana sisi kwa sisi.
Pendo
hili ni utayari wa kujitoa zaidi na zaidi kwa rafiki hadi tone la mwisho yaani,
uhai uliokuwa nao kwa ajili ya wengine. “Hakuna aliye na upendo
mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh
15:13. Wewe kama Mama au Baba katika familia unatoa pendo sadaka pale ambapo
waithamini ndoa yako na familia yako na upo tayari kujitoa bila kujibakiza ili
wewe upungue watoto waongezeke na Mwenzi wako wa ndoa aongezeke. Na kwa tendo
hilo, Kristo ataonekana kwa watu. Nami kama Mtawa na Mkleri yanipasa kwa furaha
nithamini maisha yangu ya wakfu na niwe tayari kupungua ninapotoa huduma kwa
wengine bila kujibakiza ili Kristo aongezeke na kuonekana kwa watu.
Ni kwa ajili ya upendo
sadaka Mtume Paulo haoni shaka kumtoa Onesimo kwa Filemoni kwa ajili ya vifungo
vya Injili. “Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo
vyangu, yaani, Onesimo; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate
kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili,” Flm 10, 13. Naye anamwambia
Filemoni, “kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee,
na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia,” Flm 9. Kadiri ya mapokeo, Paulo anaandika
Waraka kwa Filemoni akiwa Rumi kunako mwaka 61-63 Baada ya Kristo. Mtume Paulo
anampasha habari Filemoni kwamba mtumwa wake Onesimo aliyemtoroka atarudi. “Basi
kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe,” Flm 17.
Waraka huu unafunua
moyo wa Paulo na mafundisho yake juu ya utumwa, Rum 6:15. Mtume Paulo hakatazi
utumwa kama ulivyokuwa zamani, bali anakazia sana kuwa bwana Mkristo lazima
amjali mtumwa wake kama ndugu katika Kristo, Kol 3.22-4.1. “Lakini sikutaka
kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama
kwa lazima, bali kwa hiari,” Flm 14. Ndani na katika Kristo Yesu sisi sote ni
ndugu licha ya historia zetu.
Marietha akiwa ndiye
mkubwa katika familia ya watoto watano ya Mzee Jahiro, alikuwa na wakati mgumu
wa kumtumza Mama yake Mzazi aliyekuwa na ugonjwa wa kupooza. Baba wa familia,
yaani, Mzee Jahiro, aliuwawa kikatili kutokana na msimamo wake wa kusimamia
haki kwa wote akiwa kama kiongozi wa kijiji kile.
Marietha ambaye kwa
sasa ndiye muhimili wa familia, alitegemea sana biashara yake ya kuuza vocha za
simu katika kituo cha mabasi. Maisha hayakuwa rahisi hata kidogo ukilinganisha
kipato chake, na hitaji la familia ikiwa ni pamoja na wadogo wake wanne na mama
mgonjwa. Mama Marietha muda wote alikuwa kitandani na wakati mwingine kutolewa
nje endapo hali ya hewa iliruhusu. Hali hii ilimuhuzunisha sana Mama Marietha
kwani alionja mzigo mzito aliokuwa nao mwanaye Marietha.
Hali hiyo ya Marietha
ilimpelekea Mama yake kuyavumilia mateso na hata kukaa kimya alipohisi maumivu
makali sana. Wakati mwingine ilimlazimu kutabasumu alipomwona Marietha amechoka
na kukata tamaa kutokana na ugumu wa maisha. Tabasamu hili lilikuwa faraja
kubwa sana kwa Marietha, na hakuacha kujitoa bila kujibakiza kwa familia yake.
Muda wote anapobaki
nyumbani, Mama Marietha husali rozari hadi pale amwonapo mwanaye jioni
nyumbani. Mama Marietha huikabidhi kila siku familia yake mikononi mwa Mama
Bikiri Maria, na kwa namna ya pekee mwanaye Marietha ambaye ndiye mpiganaji
mkubwa wa mkate wa kila siku. Baada ya miaka mitatu mambo yalibadilika sana.
Marietha alifungua kituo cha huduma ya M-Pesa na duka la nguo. Waliokuwa
wanasoma, yaani, wadogo zake walifaulu vizuri na kuendelea na masomo yao ya
sekondari na wengine wawili chuo kikuu. Marietha alishangaa sana neema na
baraka za Mungu zilivyokuwa zinammiminikia.
Siku mmoja Marietha
aliwahi nyumbani mapema ili amshirikishe mama yake furaha na mafanikio yake
katika biashara. Marietha alimsimulia yote mama yake na kumwambia,
“ninayofuraha kubwa sana kuwa na Mama kama wewe licha ya ugonjwa ulio nao. Mama
nakupenda sana kwani umenifundisha mambo mengi na hasa uvumilivu.” Huku machozi
ya furaha yakimtoka, Mama Marietha alimjibu mwanaye, “Mwanangu, maisha yetu
kama familia na hasa wewe kama nguzo yetu baada ya kifo cha baba yako na mimi
kupooza, nilikuwa naikabidhi familia yetu kila siku mikononi mwa Mama yetu
Bikira Maria, na hasa wewe. Mama huyu amekuwa kimbilio letu kila siku.
Usimwache katika maisha yako.”
Siku ile ilikuwa ya
furaha sana. Hata hivyo Mama Marietha aliwaomba watoto wake wasali Salamu Maria
moja ili apumzike. Walifanya hivyo na kila mmoja alienda zake kulala. Kama
ilivyokuwa kawaida ya Marietha kabla ya kwenda kwenye biashara zake humtakia
hali mama yake, ikiwa ni pamoja na kumtengea chai. Marietha alipoingia chumbani
mwa mama yake hali haikuwa kama kawaida. Mama Marietha alikuwa kesha fariki katika
hali ya utulivu na tabasamu kubwa. Kutazama pembeni, Marietha aliona bahasha
juu ya meza na ndani yake kulikuwa na Rozari na ujumbe huu, “kamwe usimwache
Mama Bikira Maria. Ndiye anayekupigania kwa mwanaye Yesu Kristo, na kukubeba
hadi leo.”
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa kuwa mawazo ya mwanadamu yana
woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa,” Hek 9:14.
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie neema na nguvu katika kukupenda bila kujibakiza. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario