IJUMAA WIKI YA 16 YA MWAKA-I
Somo: Kut 20:1-17
Zab: 19:7, 8, 9, 10.
Injili: Mt 13:18-23
Nukuu:
“Usijifanyie sanamu ya
kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini
duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa
kuwa mimi, Bwana wako, ni Mungu mwenye wivu,” Kut 20:4-5
“Naye aliyepandwa penye
udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye
azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini,” Mt 13:23
TAFAKARI: “Usijifanyie
sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, bali
kuwa udongo mzuri pale ulipo.”
Wapendwa
wana wa Mungu, somo la kwanza la tuonyesha taswira
halisi ya Mungu. Ni yeye tu tuwezaye kumsujudia na kumtumikia. Sisi binadamu
tunamsujudia na kumtumikia Mungu, kwa sababu yeye ndiye alfa na omega, (Ufu
22:13) na anatuambia kuwa, “mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu;
nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha
wanichukiao,” Kut 20:5. Tunapomsaliti na kutompa mastahili yake Mungu wetu wa
kweli, adhabu yake huenda hadi kizazi cha nne. Mahangaiko haya kwa upande
fulani hubeba mambo yale ambayo kwayo twateseka bila kujua chanzo chake.
Inawezekana jamii fulani, koo fulani, familia fulani, mahali fulani, kwa wakati
fulani, walimwasi Mungu kwa matendo yao maovu na kukaa hivyo bila kufanya toba
ya kweli.
Wapendwa wana wa Mungu,
katika ulimwengu wa roho huwa
tunarithi pia maovu na baraka. “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi
yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi
nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na
kulikuza jina lako; nawe uwe baraka,” Mwa 12:1-2. Huku ni kurithi baraka za Mungu.
Ukristo katika Tanzania yetu hii ya leo haujazidi ya miaka
150. Sehemu nyingi ni chini ya miaka 10 tu. Hivyo basi kati ya kizazi cha tatu
na cha nne watu wengi walikuwa wanaishi nje ya ukristo kwa miaka mingi. Hivyo
walitenda dhambi kama:-Kuabudu sanamu, Kuabudu miti mikubwa, Kuabudu milima,
Kuabudu vyanzo vya maji, Kuabudu mizimu, Kuabudu mababu waliokufa
Hata leo wapo wanaoishi katika hali ya kufanya matambiko,
mazindiko, na dhambi zinazoleta uovu kwako, ndugu zako, wanao, na wajukuu mpaka
vilembwekezi. “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala
mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala
kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi,
Bwana wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata
kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,” Kut 20:4-5. Ndugu yangu, huku
ndiko kurithi laana. Tutapata usalama tu tutakapoziacha njia hizi na kumsujudia
na kumtumikia Mungu wa kweli. Naye anasema, “nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao,
na kuzishika amri zangu,” Kut 20:6.
Ndugu yangu, leo hii
watu wengi wamevipa umaana vitu kuliko uhusiano wao na Mungu. Jamii yetu ya
Tanzania leo tumekuwa na matukio mengi sana ya kushangaza na kusikitisha.
Tunapenda utajiri wa haraka na usio wa kutoka jasho. Tunapenda madaraka pasipo
kuwajibika. Tunapenda vyeo pasipo kujiandaa. Kutokana na mfumo huu, na matamanio yake, imetufanya kama Taifa
kuwa moja ya nchi katika bara letu la Afrika kuongoza kwa ushirikina.
Ushirikina ni matokea ya kutokuwa na imani dhabiti. Kwa upande mwingine,
ushirikia ni kuwa na imani ya nguvu fulani kutoka kwenye kitu ambacho hakina
uhusiano na hicho unachokitafuta au kukifikiria.
Ni ukweli usio tia
shaka kwamba, watu wengi leo hasa kwenye ulingo wa siasa, wanatumia njia zisizo
rasmi kufikia malengo yao. Watu hawa wapo tayari hata kutoa maisha ya watu kama
kafara kufikia malengo yao. Waathirika wakubwa katika kundi hili ni watoto
wachanga na walemavu wa ngozi “maalbino.” Hofu yangu na ya walio wengi ni kuona
pale vyombo vya usalama, na vyombo vya kutoa haki kama mahakama kutokufanya cho
chote. Tafsiri ya wazi ni kwamba wahusika wa mambo hayo ni watu na viongozi
waliopewa dhamana kubwa ya uongozi.
Kwa maana nyingine,
miungu inayoabudiwa leo ni Utajiri, Uongozi, Madaraka, na Umaarufu. Ndugu
yangu, “thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima,
nayo ni uzima.” Tuna kuwa na utajiri, heshima na uzima tunapomcha Mungu na si
vinginevyo. Je, mbele ya Mungu yatupasa kujisifu kwa jambo gani? Mungu asema
hivi, “ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na
kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika
nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,” Yer 9:24.
Kwa maana nyingine,
“Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekina yake, wala
mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa
sababu ya utajiri wake,” Yer 9:23. Sote yatupasa kuutafuta kwanza ufalme wa
Mungu. Hili ndilo kusudia la kwanza la uumbaji wetu, kwamba, “utafuteni kwanza
ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa,” Mt 6:23. Tumeumbwa ili tumjue, tumpende, tumtumikie na
mwisho turudi kwambe mbinguni.
Mtume Paulo anatupa
sababu ya Imani yetu na ufuasi wetu kwa Kristu. Tunamuishi na kumhubiri Kristo
aliyesulubiwa kwa sababu Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Jambo
hili kwa Wayahudi ni kikwazo, na Wayunani ni upuuzi. Wayahudi ni kikwazo kwa
sababu kifo cha Kristo siyo mategemeo yao kwa Masiha waliyemtegemea. Masiha
waliyemtegemea ni yule ambaye angewaweka huru kutoka dola ya Kirumu. Ni masiha
wa kisiasa zaidi. Yesu anasema, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme
wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije
nikatiwa mkononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa,” Yoh 18:35. Hiki
ndicho kikwazo kikubwa kwa Wayahudi. Kwa Wayunani ni upuuzi kwa mtu mwenye
nguvu na mfanya miujiza kama Yesu kufa kifo cha aibu, tena cha msalaba. Kwa
ufahamu na falsafa yao, jambo hili haliwezekani. Hawaoni utukufu wa msalaba
zaidi ya karaha. Bali twajua, “wenye hekima wataurithi utukufu, bali kukuzwa
kwa wapumbavu ni fedheha,” Mit 3:35. Yesu Kristo ndiye kielelezo na njia sahihi
ya kuurithi ufalme wa Mungu.
Wapendwa
wana wa Mungu, Injili ya leo inatoa ufafanuzi wa habari ile ya Mpanzi. Leo Yesu
anafafanua lugha ile ya picha aliyoitumia kadiri ya mazingira na watu wake.
Lengo la lugha ile ya picha kuhusu Mpanza, ni kuelezea kweli hiyo ya Mungu
ndani ya mioyo yetu. Hivyo alichokifanya Mpanzi ilikuwa ni namna neno la Mungu
lifanyavyo kazi ndani ya mioyo yetu na kutubadilisha. Ili neno la Mungu liwe
tumaini la kweli, na ushuhuda wa kweli ndani yetu, na kwa wale wanaotuzunguka,
lazima neno hilo tulisikie, tulipokee, kulitafakari, kulishirikishe, na mwisho
tuwe sehemu ya neno hilo kwa kuwa mashahidi wa neno hata ikibidi kufa kwa kweli
hiyo. Kulipokea neno lazima uwe na utayari wa kulisikia neno. Usipokuwa na
utayari huu ni sawa na “mbegu nyingine zilianguka karibu na
njia, ndege wakaja wakazila,” Mt 13:4. Na huu ndio ufafanuzi wa Yesu; “Kila mtu
alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua
lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia,” Mt 13:19
Kulitafakari neno la
Mungu kunakuhitaji kulisikia neno hilo na liguse maisha yako. Kutafakari neno
ni kama kucheua kile ulichokula. Kama hili halikufanyika ni sawa na mbegu zile “zilizoanguka
penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa
kina, na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka,” Mt
13:5-6. Na hapa Yesu anatuambia kwa kuifafanue lugha ile ya picha, kwamba, “Naye
aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa
furaha; lakini hana mizizi ndani
yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno,
mara huchukizwa,” Mt 13:20-21. Kulipokea neno kwa furaha na kukosa mizizi ndani
yake, ni kukosa tafakari ya kina juu ya kile ulichokisikia au kukisoma. Ni
kutokulicheua neno, na hivyo neno hilo kutokuwa sehemu ya maisha yako, na
kutokukupa uwezekano wa kulishirikisha kwa wengine. Huwezi kutoa usichokuwa
nacho. Je, itawezekana kweli kushirikisha kwa wengine kile usichokuwa nacho?
Wapendwa wana wa Mungu,
kuwa na uwezo wa kulishirikisha neno la Mungu kunategemea sana namna
tunavyolicheua neno la Mungu, yaani, uwezo ule wa kulitafakari neno la Mungu na
kuleta mabadiliko kwanza ndani yetu. Tunaposhindwa kufanya hivyo ni sawa na
mbegu “zilizoanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga,” Mt 13:7. Kumbe
tunaweza kushirikishana neno la Mungu vizuri pale tunapokuwa na mazingira
mazuri ya kulitafakari neno la Mungu kama lilivyo, na siyo tulivyo kwa kujionea
huruma. Na hapa Yesu anafafanua lughu hii ya picha na kusema, “Naye aliyepandwa
penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na
udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai,” Mt 13:22. Leo ni wangapi tu sehemu ya Jumuiya ndogo ndogo
iliyopo kwenye eneo lako, ikiwa ni pamoja na kwenda kwenye jumuiya hiyo na kuwa
sehemu ya familia hiyo, ukiumega mkate na kushirikishana neno la Mungu? Leo
jumuiya hizi sehemu nyingi zimekuwa kundi la watoto, akina mama, tena wajane,
na wazee. Hakuna vijana, na wala hakuna akina Baba. Je, hayo malimwengu
unayoyakubatia yana uzima ndani yake au umebaki kujifariji katika upumbavu? Tukifanikiwa
katika hatua hii, yaani, kuliishi neno la Mungu, ni wazi tu mashahidi wazuri wa
neno la Mungu ndani yetu na wale wote wanaotuzunguka.
Kuwa
mashahidi na washuhuda wa neno ni sawa na mbegu zile zilizoanguka “penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia,
moja sitini, moja thelathini,” Mt 13:8. Hiki ndicho atakacho Yesu kwako na
kwangu, yaani, tuwe mashahidi wa kweli wa neno la Mungu. Na huu ndio ufafanuzi
wa Yesu juu ya udongo mzuri: “Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye
alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na
huyu sitini, na huyu thelathini,” Mt 13:23. Kuzaa huku matunda kwa viwango
tofauti tofauti kunatokana na nguvu ya
Roho ile isukumayo ufahamu wetu juu ya neno ambalo sasa siyo tu tumelisika,
bali tumelipokea. Na siyo tu tumelipokea, bali tumelitafakari kwa kina na
kulicheua. Na siyo tu tumelitafakari kwa kina na kulicheua, bali kwa sasa
tumelishirikisha vyema kwa wengine (uinjilishaji upya). Na mwisho siyo tu
tumelishirikisha neno hilo kwa wengine bali tumekuwa sehemu ya neno hilo, kwa
kuwa mashahidi na washuhuda wa kweli kwa sababu maisha yetu yanaakisi kweli
hiyo. Kumbe haitoshi kufanya mambo mazuri katika ukamilifu wake, bali yakupasa
kuwa mkamilifu katika maana halisi ya ukamifu kama anavyotuasa Yesu, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa
mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Naye
aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa
nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini,”
Mt 13:23
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nifanye udongo mzuri ili niufunue uzuri na utukufu wako pale nilipo.
Amina