viernes, 28 de julio de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 16 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 16 YA MWAKA-I

Somo: Kut 24:3-8

Zab: 50:1b-2, 5-6, 14-15

Injili: Yoh 11:19-27

Nukuu:

Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda,” Kut 24:3

“Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote,” Kut 24:8

“na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao,” Yoh 11:19

“Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa,” Yoh 11:21

“Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa,” Yoh 11:22

“Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;” Yoh 11:25

“Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni,” Yoh 11:27

TAFAKARI: “Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa,” Yoh 11:22.

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu kwa nyakati mbalimbali alifanya maagano na watu wake kwa malengo mbalimbali yakilenga ushirika wake na viumbe vyake, katika safari nzima ya kuvikomboa, na hasa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Agano hili lilifanya kuaminiana na kutekeleza maagizo yake kwa pande zote mbili. “Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda,” Kut 24:3. Mungu haikumpasa kujisainisha katika agano kwa sababu yeye mwenyewe ni UAMINIFU, na kwamwe katika Ukuu wake hawezi kwenye kinyume chake mwenyewe.

Maagano haya kama ishara ikiwa ni kielelezo kwa upande wa binadamu iliendana na uteketezaji wa viumbe vingi visivyo na doa. Damu ya viumbe hili vilihesabika kama ndiyo muhuri na kusahilisha muungano huu wa kiagano. “Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote,” Kut 24:8. Hivi ni hatua za awali katika safari nzima ya mwokovu wetu. Je, kwa nini Mungu hakulifanya jambo hili mara moja tu na watu wake wakamwelewa? Bila shaka tendo na safari hii ya wokovu wa Mwanadamu umepita katika hatua mbalimbali kwa lengo la kumfanya mwanadamu huyu atambue uzuri na umaana wa thamani ya wokovu wake, na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Ni kupitia Kristo Yesu ambaye ndiye ufunuo halisi na wawazi wa Mungu mwenyewe tumefumbuliwa kweli ya Mungu, na kwake tu, yaani neema yake,  inatosha kama asemavyo Mtume Paulo, 2Kor 12:9.

Ndugu yangu, kile alichokisema Yesu, yaani, “…mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:32, ndicho anachotaka kukithibitisha mbele ya wanafunzi wake. Na zaidi ya hayo Yesu anakutaka wewe na mimi leo kuamini pasipo shaka yoyote kwamba Yeye ndiye njia, na kweli, na uzima; na mtu haji kwa Baba, ila kwa njia yake, Yoh 14:6. Ni katika mantiki hii Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba, “…Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha,” Yoh 11:11. Hata hivyo wanafunzi wake hawakufahamu alichomaanisha Yesu kwa maneno hayo. Tafsiri ya alichokisema Yesu ni hiki: “…alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa,” Yoh 11:13-14.

Ukweli ni kwamba hata baada ya Yesu kuiweka habari ile ya Rafiki yake wazi, yaani, Lazaro kuwa amekufa, Tomaso aitwaye Pacha-mwanafunzi wake Yesu, anabeba habari ile kwa wepesi mkubwa bila kufikiri na kuzama ndani kwa kile alichokisema Yesu. Na hivi ndivyo ilivyokuwa: “Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye,” Yoh 11:16. Hapa Tomaso anaonekana mtu asiye na hofu wala shaka, ila wakati utathibitisha kile alicho Tomaso. Ni Tomaso huyu huyu baada ya ufufuko wa Yesu aliyekuwa mtu mwenye mashaka mengi juu ya ufufuko wa Kristo.

Swali la kujiuliza ni hili:-ikiwa Yesu alijua fika habari ya kuumwa kwake Lazaro hadi kupatwa na mauti, kwa nini basi alijichelewesha kufika na kumponya ugonjwa wake kabla ya kufikwa na mauti hiyo? Ndugu yangu mpendwa, sehemu ya kwanza la swali hili Yesu mwenyewe kesha ijibu. Na jibu ni hili: -“Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,” Yoh 11:4. Na sehemu ya pili ya jibu la swali hili inathibitisha kile alicho Kristo Yesu, yaani, ndani na katika Yeye ipo njia, kweli na uzima, Yoh 14:6. Na ndiyo maana kwa makusudi kabisa Yesu anafika siku ya nne baada ya kifo cha rafiki yake Lazaro. Siku ya nne ikiwa mwili waanza kuoza hakuna tena uwezekano wa kurudi katika ‘hali hai’ kadiri ya mila na desturi za kiyahudi. Hivyo “…Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne,” Yoh 11:17

Kuchelewa kwa Yesu kunaongeza uzuni na majonzi kwa dada zake Lazaro- Martha na Mariamu. “Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa,” Yoh 11:21-22, 32. Lakini ukweli ni kwamba alipo Kristo halijaharibika jambo kwa sababu, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Yesu anawandolea hofu, mashaka, na uzuni Martha na Mariamu kwa kuthibitisha kile alicho, kwamba, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?” Yoh 11:25-26. Naye Martha pasipo shaka anamjibu Yesu, “Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni,” Yoh 11:27. Huzuni na majonzi haya ya Martha na Mariamu, pamoja na majirani zao, ikiwa ni pamoja na imani ile waliyokuwa nayo juu ya Kristo Yesu, inaunyong’onyeza moyo wa Yesu sana. “Yesu akalia machozi,” Yoh 11:35. Tendo hili linathibitisha pasipo shaka asili ya pili wa Yesu, yaani, ‘ubinadamu wake.’ Hakika Yesu anakupenda wewe na mimi upeo, Yoh 13:1.

Wapendwa wana wa Mungu,

“Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;” Yoh 11:25

Tusali: Ee Yesu na yote yangu, usiniache hasa pale napozama katika mashaka na sintofahamu kubwa katika maisha yangu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario