sábado, 5 de agosto de 2017

TAFAKARI: SIKUKUU YA KUNG'ARA KWA BWANA WETU YESU KRISTO-A


SIKUKUU YA KUNG’ARA KWA BWANA WETU YESU KRISTO

Somo I: Dan 7:9-10, 13-14

Zab: 97:1-2, 5-6, 9

Somo II: 2Pet 1:16-19

Injili: Mt 17:1-9

Nukuu:

Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14

Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,” 2Pet 1:17

“akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru,” Mt 17:2

“Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye,” Mt 17:3

“Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya,” Mt 17:4

“Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5

“Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana,” Mt 17:6

“Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope,” Mt 17:7

“Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake,” Mt 17:8

“Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu,” Mt 17:9

TAFAKARI: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anasheherekea Sikukuu ya kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tukio hili la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linafunua Utukufu na Umungu ya Yesu kabla na baada ya mateso na kifo chake kama sadaka iliyo hai na yenye kumpendeza Mungu. Huu ni mpango wa Mungu tangu zamani ili kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi. Nabii Danieli alifunuliwa siri hii katika ndoto, na leo inatimia ndani na katika Kristo. “Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Tukio hili la pekee la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linadhihirisha uwezo na mamlaka aliyonayo.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa upendo usio na kipimo, wakati ulipotimia, (Ebr 1:1-2), katika historia hii ya wokovu, Mungu mwenyewe amejimwilisha na kukaa nasi. “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Hivyo wapendwa katika Kristo, lnjili ya leo inauweka sawa ukweli huu kwa mambo makuu matatu; Dira yetu ya kufuata kama Wakristo, Utimilifu wa nyakati, na Hatma yetu iliyojengeka katika agano la umilele. Haya yote yanafanyika katika tukio hili la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya simulizi la Injili ya leo.

Kwanza, ni dira yetu ya kufuata kama Wakristo. Heshima na cheo chako kama Mkristo ni utakatifu wako. Hivyo maisha yetu kama Wakristo kuelekea umilele yatafikika na kuwezekana kama ni tokeo la utakatifu wetu kwa kuyaona maisha kama ni jukumu la muda fupi hapa duniani na kama pia sehemu pekee ya maandalizi. Udhihirisho wa utakatifu huu kama dira yetu ya maisha ni tendo lile la kung’ara Kristo Yesu. “Akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru,” Mt 17:2. Kristo anavikwa Utukufu wake ambao ataunyakua rasmi mara baada ya mateso, kifo na ufufuko huko Yerusalemu. Hivyo Utukufu wa Kristo hautenganishwi na msalaba/mateso. Kwa maana nyingine hakuna Utukufu pasipo msalaba. Kama Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6, nasi wafuasi wake itatupasa kupita njia hiyo ya msalaba, ukweli huu anaotufundisha, ili tuufikie uzima ule, yaani maisha ya milele. Kristo ni masiha ya Msalaba, nasi twamfuata Masiha wa Msalaba ili tuifikie taji ile ya Utukufu baada ya kuhesabiwa haki.

Pili, ni ukamilifu wa nyakati. Katika tendo hili la kung’ara, tunaelezwa tokeo la watu wawili, yaani Musa na Eliya katika mazungumzano na Yesu. “Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye,” Mt 17:3. Katika tendo hili, Musa anawakilisha Torati, na Eliya Unabii. Hivyo leo Yesu anaikamilisha Torati na Unabii. Naye Yesu anatuambia, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Torati inatimilizwa kwa amri ya upendo kwa Mungu na jirani.Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Ni ndani na katika Kristo tu tunapata neema na kweli kwa mkono wake. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Na huku ndiko kutimilika kwa sheria na kutamalaki kwa upendo, kweli, na neema.

Leo pia unabii wote ulionenwa juu ya Kristo na historia nzima ya wokovu wetu unakamilika. Unabii huu unafika ukomo wake kwa uwepo wa Kristo ambaye ni UPENDO WA MUNGU kwetu. Mtume Paulo anasema, Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,” 1Kor 13:8. Huyu ndiye Kristo Yesu! Kung’ara kwake Bwana wetu Yesu Kristo kulikoonyesha Ufukufu wake, kunaamsha furaha ya ndani ya Mtume Petro na kuyasema ya moyoni mwake. “Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya,” Mt 17:4. Hata hivyo hilo halikuwa kusudi la Yesu kubaki mlimani pale. Yesu inabidi ashuke na kuukumbatia Msalaba kama alama ya ushindi na  hapo ndipo wokovu wako na wangu ulipotundikwa. Hii ndiyo safari kuelekea kilele kile cha wokovu kama Masiha wa Msalaba.

Tatu, ni hatma yetu iliyojengeka katika agano la milele. Kristo ndiye kielelezo chetu na wokovu wetu. Leo Mungu Baba anauweka ukweli huu hadharani na kusema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5. Hili ndilo agano la milele kati yetu na Mungu, na Kristo akiwa ndiye daraja na mlango halisi wa sisi kupitia kwani ni kwake tu tutakuwa salama kama njia, ni kwa Kristo tu tunalishwa kweli katika kweli, na Kristo tu ndiye uzima halisi. Hivyo hapana tena ufunuo ulio wa wazi na kamili zaidi ya ufunuo huu wa Mungu kupitia mwanaye Mpenzi. Tendo hili linathibitishwa na sauti ya Mungu mwenyewe kwa viumbe vyote, Mt 17:5. Ndugu yangu, Je, unafuata sauti gani katika maisha yako? Sauti hii kutoka mbinguni inampa Yesu Kristo Heshima, Mamlaka, na Utukufu. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,” 2Pet 1:17. Nasi tunapoisikia sauti hiyo na kuishi kweli hiyo, twajazwa nguvu, heshima na utukufu kwa kuishi ndani na katika Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, zipo sauti nyingi katika maisha yetu. Je, sauti hizo zinatupeleka karibu na Kristo Yesu au zinatutenganisha na ukweli wake? Kusikia sauti hii ni kuyafanya mapenzi yake. Na kufanya mapenzi yake maana yake ni tuyafanye kila mmoja kadiri ya wito wake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake,” Mt 17:8

Tusali:-Ee Yesu, tujalie neema ya kuyafanya mapenzi yako. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario