JUMATATU WIKI YA 18 YA MWAKA-I
Somo: Hes
11:4-15
Zab:
81:11-12, 13-14, 15-16
Injili:
Mt 14:13-21
Nukuu:
“Twakumbuka samaki
tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu,
na vitunguu saumu; lakini sasa
roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa
hii mana tu,” Hes 11:5-6
“Nipate wapi nyama ya
kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula,” Hes
11:13
“Mimi siwezi kuwachukua
watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda,” Hes
11:14
“Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula,” Mt
14:16
TAFAKARI: “Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.”
Wapendwa
wana wa Mungu, masomo yetu ya leo, yaani, somo la kwanza na Injili, yanaonyesha
upendo na ukarimu wa Mungu wetu. Tukumbuke kuwa safari ya ukombozi wa Taifa la
Israeli kutoka utumwani Misri haikuwa rahisi. Ugumu wa mioyo ya wana wa Israeli
unakuwa tishio kwa Musa kuyatenda yale Mungu anayoyataka. Wana wa Israeli bado
wanakumbuka maisha yao Misri licha ya utumwa waliokuwa nao huko. Hakika njaa
haina adabu! “Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na
matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana
kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu,” Hes 11:5-6.
Watu hawa hawaoni mkono wa Mungu katika wokovu wao. Wanadai kupewa nyama. Jambo
hili linakuwa sikitiko kubwa kwa Musa, naye anasema, “Nipate wapi nyama ya
kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula,” Hes
11:13. Maisha yetu ni zaidi ya kula na kunywa. Tupo hapa duniani kwa muda mfupi
tu, tena tunajiandaa kwa maisha yale ya umilele. Naye Mtume Paulo anatupa
angalizo juu ya kweli hii, na kusema, “…maana ufalme wa Mungu si kula wala
kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17. Na
huyu Roho siye yule Roho “Mtakavitu,” bali MTAKATIFU.
Musa
anafikia hatua ya kukata tamaa kutokana na ugumu wa ndugu zake. “Mimi siwezi
kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa
kunishinda,” Hes 11:14. Ni kweli katika uongozi wetu na nafasi mbalimbali
tunakutana na mizigo mizito na wakati mwingine haibebeki kiurahisi. Katika hali
hii tunapata nguvu tu pale tunapomjeukia Mungu na kuwa na hofu naye.
Injili
yetu ya leo tunaona ukarimu wa Mungu kwa watu wake. Yesu anawaonea huruma wale
waliokuwa wanasikiliza neno lake la uzima. Kibinadamu wanafunzi wa Yesu wanatoa
ushauri kwa Yesu kuwa watu waachwe waende zao vijini na kutafuta chakula. Yesu
anawakumbusha wajibu wao kuwa yawapasa kuwalisha watu hao chakula. Hivyo ushauri
na agizo la Yesu ni hili: “Hawana haja kwenda
zao, wapeni ninyi vyakula,” Mt 14:16.
Wapendwa Taifa la Mungu, kwa ubatizo wetu tunashiriki ukuhani wa Kristo, unabii na ufalme
wake. Hivyo kila mmoja kadiri ya wito wake anajukumu la kuwapa chakula watu
wale aliwakabidhiwa. Na zaidi chakula hiki siyo tu hiki cha leo na kesho bali
neno la uzima wa milele. Na juu ya neno Yesu anasema, “mbingu n anchi zitapita;
lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Mt 24:35.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mimi siwezi
kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa
kunishinda,” Hes 11:14
Tusali:-Ee Yesu
nijalie neema ya kukuona wewe kwa wale wote ninaokutan nao kila siku. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario