JUMAMOSI WIKI YA 17 YA MWAKA-I
Somo: Law 25:1, 8-17
Zab: 67:1-2, 4, 6-7
Injili: Mt 14:1-12
Nukuu:
“Nawe utajihesabia Sabato saba za miaka, maana, miaka
saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka kwenu, maana miaka
arobaini na kenda,” Law 25:8
“Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa
mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu, nanyi
kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa
yake,” Law 25:10
“Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake,” Law
25:13
“Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi
ndimi Bwana, Mungu wenu,” Law 25:17
“Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako
kuwa naye,” Mt 14:4
“Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote
atakaloliomba,” Mt 14:7
“Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake,
na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe,” Mt 14:9
TAFAKARI: “Simama katika kweli
na tenda haki, mche Mungu wako kwa kuwa Yeye ndiye Bwana, Mungu wako.”
Wapendwa
wana wa Mungu, ni wito kwa kila mmoja wetu na hasa aliyepewa dhamana ya
kuongoza kusimama katika kweli na kutenda haki. Kufanya hivyo ni kutambua na
kuongozwa na hofu ya Mungu ukijua wazi kwamba ni wajibu kiimani kumcha Mungu
muumba wako kwa kuwa yeye ndiye Bwana Mungu wako. Kumcha Mungu ni kufanya yale
Mungu ayapendayo na yenye kuiumba taswira yake kwa viumbe vyake. Ni kutambua
kwa undani kabisa kwamba uwepo wapo bila Mungu si chochote wala lolote. Ni
kutambua pia hakuna uhai bila Mungu. Hofu hii ya Mungu ndiyo kieleleza cha
Ibada zote hazifanyazo mwanadamu kwa kutambua uwepo wa Mungu wake kwa kila kitu
akifanyacho. Tufanyapo ibada hizi isiwe ni kutimiza wajibu tu wa kiliturjia,
bali tuzame katika kweli ya kile tukifanyacho kwa Imani thabiti.
Hivyo,
Waisraeli katika maana hiyo hapo juu wanaifanya sabato kuwa hai kinadharia na
matendo. “Nawe utajihesabia Sabato saba za
miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka
kwenu, maana miaka arobaini na kenda,” Law 25:8. Tendo hili linapofanyika kwa
miaka 49, kilele chake, yaani mwaka ule wa 50, hufanywa yote kwa matendo zaidi.
Mwaka huu ujulikana kama mwaka wa jubilee. Ni wakati wa kuanza upya katika
yote, kusamehe yote, kuachilia yote, na hasa wafungwa. Kwa ujumla ni mwaka wa
kuishi kimatendo upendo wa Mungu. “Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake,” Law 25:13
Ni mwaka wa kuishi neema na baraka za Mungu. Kila mmoja
alitafuta namna ya pekee kabisa kujitakasa na kuwa mpya mwili na roho. Hivyo, “mwaka
wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa
watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu, nanyi kila mtu atairudia milki
yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake,” Law 25:10. Hakika ni
kipindi cha upatanisho wa kweli na kuishi katika haki na kweli ya Mungu. Hii
ndiyo hofu ya Mungu itusukumayo kumcha usiku na mchana. Naye Mungu anasema, “wala
msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu
wenu,” Law 25:17
Mpendwa,
katika Injili ya leo tunaona hathari za matumizi mabaya ya madaraka
yanayosababisha maafa makubwa kwa wale watetezi wa haki katika jamii inayowazunguka.
Ni jambo la hatari sana kuwa na kiongozi anayeongozwa na mihehuko ya hisia
zake, huku akitegemea sifa kutoka kwa watu. Kiongozi mwenye misukumo hii ya
kihisia ni rahisi sana kuzikanyaga haki za wale anaowaongoza. Hii ni pamoja na
kuwa makini katika ahadi azitoazo kiongozi mbele za watu. Herode anamwahidia
binti yake chochote apendacho baada ya kucheza vizuri na kuufurahisha umati wa
watu siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake. “Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote
atakaloliomba,” Mt 14:7. Mfalme Herode anajifunga kwa kauli yake mwenyewe.
Mfalme Herode hakuwa na lakusema binti yake alipokitaka kichwa na Yohane
Mbatizaji zaidi ya kutimiza ahadi yake na kulinda heshima yake kama kiongozi. “Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya
viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru
apewe,” Mt 14:9. Je, ni watu wangapi huwa kafara kunakotokana na utafutaji wa
sifa na umaarufu wa baadhi ya viongozi wetu?
Ni mbaya
sana kutafuta umaarufu kwa kukanyaka haki za watu, na hasa wale ambao wapo
kinyume chetu kutokana na matendo yetu yasiyo haki na hofu ya Mungu. Yohane Mbatizaji ni mhanga wa viongozi wale wenye kupenda
sifa na umaarufu. Kosa la Yohane Mbatizaji ni kusimama katika kweli. Umauti
unamfika Yohone Mbatizaji kwa sababu alimwambi Mfalme Herode “Si halali kwako kuwa naye,” Mt 14:4. Wapo
wahanga wengi wa mtindo wa Yohane Mbatizaji katika familia zetu, Jumuiya zetu
ndogondogo za Kikristo, Jumuiya zetu za kitawa, Makanisani mwetu, sehemu zetu
za kazi, na mbaya zaidi leo katika mfumo mzima wa utawala. Wapendwa tuutafute
kwanza ufalme wa Mbinguni na mengine yote tutapewa kwa ziada.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote
atakaloliomba,” Mt 14:7
Tusali: Ee Yesu tujalie imani thabiti tuutafute ufalme wa mbingni.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario