JUMANNE WIKI YA 23 YA MWAKA-I
Somo I: Kol 2:6-15
Zab: 145:1b-2, 8-9, 10-11
1.
Nitalihimidi
jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele
na milele.
(K) Bwana ni
mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
2.
Bwana ana
fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana
ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K).
3.
Ee Bwana,
kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena
utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. (K).
Aleluya:
Yoh 15:16
Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
niliyewachagua ninyi;
nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na
matunda yenu yapate kukaa;
ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.
Injili:
Lk 6:12-19
Nukuu:
“Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo
katika yeye,” Kol 2:6.
“wenye
shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama
mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani,” Kol 2:7.
“Hata kulipokuwa mchana
aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita
Mitume,” Lk 6:13.
“Simoni, aliyemwita jina la pili Petro,
na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na
Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na
Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:14-16.
TAFAKARI:
“Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana,
enendeni vivyo hivyo katika yeye,” Kol 2:6.
Wapendwa wana wa Mungu,
imani ‘sio jambo la kujaribu na kuona tokeo lake’ kama wesemavyo wenzetu, ‘try
and error.’ Wala imani sio tokeo la ‘faida katika shaka.’ Bali imani ni “…kuwa
na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1.
Kristo Yesu ni hakika ya mambo yatarajiwayo, Yoh 14:6. Ni katika mazingira haya
Mtume Paulo anasisitiza jambo hili, “…kama
mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye,” Kol 2:6.
Ukimpata Kristo katika maisha yako umepata vyote. Kwa maana nyingine, “wenye
shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama
mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani,” Kol 2:7. Na moyo usio na shukrani
ukausha mema yote.
Jambo la
kujiuliza ni hili, kwa nini wewe uliye batizwa na kukiri imani ndani na katika
Kristo unatangatanga? Nabii Yeremia anatukumbusha jambo hili, “…Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye
mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5. Ni katika
mazingira haya Mtume Paulo anasema, “Angalieni
mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya
mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa
jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Leo tuutazamapo ulimwengu wetu tunaona baadhi ya
watu wakijiinua na kumweka Mungu katika mifuko yao na wao kuwa miungu watu.
Ndugu
yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, ni katika Kristo tu kuna
“…utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili,” Kol 2:9. Mengine yote
yatokayo kwa mwanadamu ni mbwembwet tu. Wewe na mimi tumetimilika “…katika yeye
aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka,” Kol 2:10. Bila Kristo Yesu kujikweza
kwako ni kupotea muda bure! Ukweli ni kwamba, ‘katika yeye tumetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa
kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo,’ Kol 2:11. Ni katika Kristo na
ndani yake tumezikwa katika ubatizo, tumefufuliwa naye katika wafu, kuwa
washindi kwa kufanywa hai pamoja naye akiisha kutusamehe makosa yetu, na kuwa
wajasiri katika msalaba wake ambao ndio utukufu wetu kama wakristo, Kol
2:12-15. Na ndio maana twasema hakuna ‘utukufu pasipo msalaba wake Kristo.
Yesu Kristo kama
kiongozi wetu na aliyeishi kile alichokisema, ili kutimiza hazma ya kile
alichokijia, yaani, kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi, aliyaweka yote
wazi tangu mwanzo. Na kauli mbiu yake kama dira ya kila mmoja kufuata ili
kufika kule alikotaka sote tufike, yaani, uzima wa milele ni hii,“Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia;
tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Kwa maana nyingine, huruma na neema ya
Mungu hufanya kazi yake pale tunapoipokea huruma na neema hiyo kwa kufanya toba
ya kweli na majuto ya dhambi.
Na
hata baada ya kutoa kauli mbiu yake hiyo, Yesu alionyesha wazi mpango kazi wake
mwanzoni kabisa kabla ya kufanya chochote. Na mambo yalikuwa hivi; “Akaenda
Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama
ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya,
akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu,
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:16-19. Mpango
kazi mzima wa Yesu hauna uchochezi wa aina yoyote ile, wala vitisho. Ni habari
njema kweli kweli na iliyojaa matumaini.
Baada ya kutoa mpango
kazi wake, Yesu akiwa Mungu na Mwanadamu, alihitaji watu wa karibu naye ili
kuitenda kazi ile aliyoijia kama tulivyoona hapo mwanzo. Kuwapata watu hawa,
Yesu hakukurupuka, bali aliyaweka yote mikononi mwa Baba yake aliye mtuma.
Hivyo, “Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku
kucha katika kumwomba Mungu,” Lk 6:12. Ni baada ya maombi haya, Yesu
anawachagua wanafunzi wake. Na “hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake;
akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume,” Lk 6:13. Hawa
ndio wale Thenashara-Mitume kumi na wawili, Mt 10:2-5, yaani, “Simoni,
aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na
Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni
aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,”
Lk 6:14-16.
Hawa Thenashara ndio
waliokuwa wasaidizi wake wa karibu katika kutimiza lile alilolijia yaani,
kukuweka wewe na mimi huru kutoka utumwa wa dhambi. Na hawa Thenashara,
“akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi,” Lk 9:1.
‘Aliwapa mamlaka’ ikimaanisha uhuru wa kufanya yale yampendezayo Mungu. Katika
kweli hii, Yesu aliruhusu ubunifu katika utendaji kila mmoja kadiri ya karama
zake. Hakika Kristo Yesu ni Kiongozi kweli kweli, na mfano kwetu ulio hai. Tujifunze
kwake.
Baada ya kufanikisha
mpango huu, ikiwa ni pamoja na kuweka wazi kauli mbiu yake, Mk 1:15, mpango
kazi wake, Lk 4:16-19, na kuwachagua watu wake wa karibu, yaani, Thenashara, Lk
6:14-16, alianza mara moja kazi ile aliyoijia. Hivyo “waliokuja kumsikiliza na
kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na
makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka
ukiwaponya wote,” Lk 6:17b-19. Yesu kamwe hakupoteza muda wake kupambana na
watesi wake. Kwa maana nyingine, Yesu hakuwa na muda wa kupoteza kupambana na
wapinzani wake; Mafarisayo, Waandishi, na Wazee, bali aliutumia muda wake wote
wa miaka ile mitatu kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mbinguni. Matokeo ya
kazi yake ni uwepo wa wewe na mimi leo kama Wakristo na wafuasi wake wenye hofu
ya Mungu. Ni wajibu msingi kwa matiki hiyo kwamba wewe na mimi yatupasa kuwa
mawakili wa Kristo pale tulipo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu
na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha
kutusamehe makosa yote,” Kol 2:13.
Tusali:-Ee
Yesu mwema, nifanye wakili wako wema pale nilipo kila kadiri ya wito na karama
ulizonijalia. Amina