SIKUKUU YA EPIFANIA, TOLEO LA BWANA
JUMAPILI,
JANUARI 7
Somo
I: Isa 60:1-6
Zab:
72: 1-2, 7-8, 10-11, 12-13
1. Ee
Mungu, mpe mfalme hukumu zako, Na mwana wa mfalme haki yako. Atawaamua watu
wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
(K) Naam, wafalme wote na
wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie.
2. Siku
zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia. K)
3. Wafalme
wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe
vipawa. Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie. (K)
4. Kwa
maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)
Somo
II: Efe 3:2-3a, 5-6
Injili:
Mt 2:1-12
Nukuu:
“Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako
imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia,” Isa 60:1
“Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme
kuujia mwanga wa kuzuka kwako,” Isa 60:3
“Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na
kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa
utakuwasilia,” Isa 60:5
“ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa
kwa ajili yenu; ya kwamba kwa
kufunuliwa nalijulishwa siri,” Efe 3:2-3a
“Siri hiyo hawakujulishwa
wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na
manabii zamani hizi katika Roho; ya
kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na
washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya
Injili,” Efe 3:5-6
“Yesu
alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama,
mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa
Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia,”
Mt 2:1-2
“Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu
pia pamoja naye,” Mt 2:3
“Akawapeleka
Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha
kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8
“Wakaingia
nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia;
nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na
manemane,” Mt 2:11
“Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode,
wakaenda zao kwao kwa njia nyingine,” Mt 2:12
TAFAKARI:
“Mataifa wataijilia nuru yako, Na
wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Epifania, yaani, Toleo la Bwana. Leo
Mama Kanisa anatukumbusha mambo makuu matatu muhimu. Kwanza, toleo la Bwana ni
ufunuo na udhihirisho wa Kristo katika ulimwengu. Ni ufunuo wa Kristo kwa
Mataifa yote ya ulimwengu ambapo kunajidhihirisha kwa wataalamu wa
nyota-Mamajusi, wakiongozwa na nyota ile ya ajabu. “Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa
kuzuka kwako,” Isa 60:3. Wokovu wa Yesu Kristo unajionyesha kama nuru au
mwanga wa alfajiri unaoliondoa jiza na uvuli wa mauti ambao unautawala
ulimwengu. Mungu mwenyewe ndiye pambazuko.
Siku ya leo
inadhihirika wazi machoni mwa wanadamu kwamba Kristo ndiye Mfalme wa ulimwengu
wote, kwa ajili ya watu wote, na mmiliki wa utajiri wote. “Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo
wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri
wa mataifa utakuwasilia,” Isa 60:5. Ukweli
huu unajifunua kwa tunu zile alizopewa mtoto Yesu. “Wakaingia
nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia;
nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na
manemane,” Mt 2:11.
Toleo hili la Bwana la
dhihirisha ukuhani wa Kristo kwa tunu ile ya uvumba. Huyu ndiye kwa huduma yake
atavitakatifuza vyote katika ulimwengu huu na kuvikomboa. Tendo hili linakwenda
sambamba na sadaka ile atakayo itoa pale Msalabani. Tendo hili la upendo mkubwa
wa Mungu kwa wanadamu, leo linajifunua kwa tunu hii ya manemane. Manemane
yanatabiri kifo chake kama ilivyo taratibu za Wayahudi kuhifadhi Maiti na
kuzika. “Akaenda Nikodemo naye,
(yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na
uudi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa
mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama
ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika,” Yoh 19:39-40. Mambo haya makuu
matatu yanajifunua kwetu leo.
Pili, toleo hili la Bwana, Epifania, linatupa namna ya
kuishi kama Wakristo-wafuasi wa Kristo. Tendo hili ya kufunuliwa na kudhihishwa
kwa Kristo ulimwenguni pote linatuondoa katika hali ile ya kuwa “wakristo wa
kidunia” na kutufanya Wakristo wa ulimwengu-wamishionari.
Leo tunafanywa Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote na siyo Mkristo wa kidunia.
Wakristo wa kidunia kadiri ya Rich Warren, humtazama Mungu kwanza kwa ajili ya kukidhi
haja zao binafsi. Wanapenda kuhudhuria mikutano na semina za kujenga,
lakini hutawakuta katika mkutano wa umisheni kwa sababu hawaupendelei. Maombi
yao yanajali mahitaji yao binafsi, baraka, na furaha yao. Ni ile imani ya ‘mimi
kwanza.’ Waaminiwa mtindo huu husukumwa mara zote na swali hili: Je, Mungu
anawezaje kufanya maisha yangu kuwa na furaha? Wanapenda kumtumia Mungu kwa
malengo yao badala ya wao kutumiwa kwa malengo yake (Mungu).
Wapendwa wana wa Mungu, kinyume cha hapo, Wakristo wa
tabaka la ulimwengu mzima wanajua waliokolewa ili watumike na kutayarishwa kwa
ajili ya utume. Wako tayari kupokea jukumu la mtu binafsi na wanafurahia
upendeleo huo wa kutumiwa na Mungu. Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote ndio
watu pekee walio hai kikamilifu katika sayari hii. Furaha yao, uhakika na
hamasa yao vinaambukiza kwa sababu wanajua wanafanya tofauti. Wanaamka asubuhi
wakitazamia Mungu kufanya kazi kuwapita katika njia mpya. Je, unataka kuwa
Mkristo wa aina gani? Leo katika toleo la Bwana, Mungu anakualika kushiriki
katika tendo kubwa kuliko yote, la aina yake na la muhimu sana katika
historia-ufalme wake. Hivi ndivyo Yesu alivyowaambia wanafunzi wake kabla ya
kapaa, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote
kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote
niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata
ukamilifu wa dahari,” Mt 28:18-20. Tendo hili linamfanya Kristo kuendelea
kudhihirika ulimwenguni kote.
Tatu,
toleo hili la Bwana leo linatukumbusha kwamba uinjilishaji hapa duniani ni
jambo la pekee. Yapo malengo matano ya Mungu kwa maisha yako hapa duniani.
Mungu alikuumba ili uwe mshiriki katika jamii yake, kielelezo cha tabia yake,
mtu anayetukuza utukufu wake, mtumishi wa neema yake, na mjumbe wa Habari zake
Njema. Katika malengo haya matano, hii la tano linaweza tu kutendwa hapa duniani.
Yale mengine manne utaendelea kuyafanya milele kwa namna fulani. Hivyo
kutangaza Habari Njema ni muhimu sana; una muda mfupi tu wa kushirikisha
wengine ujumbe wa maisha yako na kutimiza utume wako.
Ujumbe wa Mtume Paulo kwa watu wa mataifa anaonyesha mpango
wa wokovu wa Mungu umejifunua wazi kwa Watakatifu, Mitume wake na Manabii. Hata
hivyo watu hawa wa mataifa wameupokea wokovu wa Mungu kwa ufunuo wa Roho. Watu
hawa wa Mataifa ni warithi pia wa ahadi hizi za Mungu. Katika mpango huu wa
wokovu hakuna tena matabaka. Hii ndiyo siri kubwa inayoibuliwa leo kwa tendo
hili la toleo la Bwana. “Siri hiyo hawakujulishwa
wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na
manabii zamani hizi katika Roho; ya
kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na
washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya
Injili,” Efe 3:5-6. Sote tu huru ndani na
katika Kristo Yesu.
Hivyo tuna mwili mmoja tu wa Kristo, nalo ndilo Kanisa.
Sote tu viungo vya mwili huo mmoja na Kanisa hilo moja, yaani Kanisa la Kristo.
Kwa utarajibu na mwono huu, sote tunashiriki fumbo la Kristo kwa Sakramenti ya
Ubatizo. Kristo katika mtazamo huu ndiye mrithi wa kweli wa ahadi zile za
Mungu. “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa
wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani,
Kristo,” Gal 3:16
Yesu
Kristo Mfalme na Masiha kwa mara ya kwanza anakutana na wana wa ulimwengu wote.
Injili ya Matayo inatajirisha simulizi la toleo la Bwana kwa vielelezo vya
Kibiblia-Maandiko Matakatifu. Unabii ule wa Nabii Mika unatimia, yaani; (nyota
Yakobo, zawadi za dhahabu na uvumba). Kristo ndiye Mfalme Mpya wa Wayahudi, na
Musa mpya, mwakilishi wa ulimwengu mzima. Tendo hili la toleo la Bwana ni
tishio kwa falme nyingine za ulimwengu huu. “Basi mfalme Herode aliposikia
hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3. Habari za ufalme huu
mpya ni habari njema kwa masikini na wenye hofu ya Mungu. Wale wote wasio na
hofu ya Mungu huongozwa na mipango miovu ya shetani. Mungu hata hivyo uiweka
mipango yao miovu wazi kwa ajili ya kuwanusuru wanyonge na waadilifu wake. “Nao
wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa
njia nyingine,” Mt 2:12. Huyu ndiye Mungu asiyeshindwa katika mipango yake kwa
wapendwa wake. Na huyu ndiye tunayesujudia leo siku ya Epifania, toleo la
Bwana.
Je,
ungepata leo nafasi ya kumtolea Yesu tunu ungempa kitu gani? Mathias Makyadi
kutoka Kongo alikuwa ni mmoja wa wanovisi (wanafunzi wa hatua muhimu sana
katika maisha ya kitawa) kati ya wanovisi kumi wa shirika fulani la
kimisionari. Kila wiki mmoja wa wanovisi hupewa muda wa saa moja kutafakari
mbele ya Ekaristi Takatifu. Waweza kutumia muziki wa ala ukuongoze katika
tafakuri yako au ukimya tulivu.
Tendo la
kufanya tafakuri lilikuwa gumu sana kwa Mathias Makyadi. Hivyo ilipofika zamu
yake ulikuwa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo Mathias alimwambia Yesu wa
Ekaristi hivi, “kutafakari kwa ukimya kadiri ya utaratibu uliozoeleka hapa mimi
siwezi. Hivyo naomba nikupe kile nilichonacho kama shukrani na upendo wangu
kwako.” Mathias aliondoka na kwenda chumbani mwake akachukua redio kaseti yake
na kuweka mziki wa kwao “ndombolo” na kucheza kwa nguvu zake sote, kwa kutumia
akili yake yote, na moyo wake wote.
Mara
aliingia Mlezi wake kwenye kile kikanisa
kwani kelele zile zilisikika kila viambata vya nyumba ile ya Unovisi.
“Kwa nini unafanya kelele mahali hapa na kucheza mbele ya Yesu wa Ekaristi?”
Mlezi wa wanovisi alisema kwa jazba na hasira. “Baba, hiki ndicho ninachoweza
kumpa Yesu wa Ekaristi kilicho cha thamani kubwa na ninachoweza kumpa kwa moyo
wangu wote,” Mathias amjibu Mlezi wake kwa upole. Baada ya kuyatafakari maneno
yale ya Mathias, Mlezi wake aliondoka bila ya kusema neno.
Wapendwa
wana wa Mungu, kila mmoja wetu anacho kitu cha kumpa Yesu leo kama walivyofanya
Mamajusi na alivyofanya Mathias. Lakini zaidi ya yote, mimi na wewe tunaweza
kumpa dhambi zetu kwani ndiyo mali yetu halali. Huu ni mwito wa kufanya toba ya
kweli na majuto pale tunapoutanguliza zaidi ubinadamu wetu. Tunapojitazama sisi
na huruma ya Mungu, tutazame mali hii halali tuliyonayo. Kristo Mfalme, ni
Huruma, Upendo, Msamaha, Haki, na Kweli. Zawadi hii ataibadilisha na kuwa
nyeupe kama sufu. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa
nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera,
zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Na majeshi yaliyo
mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe,
safi,” Ufu 19:14
Tusali: Ee Yesu, nijalie
neema ya kutopoteza furaha yako ndani ya moyo wangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario