SIKUKUU YA KUNG’ARA KWA BWANA WETU
YESU KRISTO
Somo I: Dan 7:9-10,
13-14
Zab: 97:1-2, 5-6, 9
Somo II: 2Pet 1:16-19
Injili: Mt 17:1-9
Nukuu:
“Naye
akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote,
na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita
kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14
“Maana
alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka
katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,”
2Pet 1:17
“akageuka sura yake
mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru,” Mt
17:2
“Na tazama, wakatokewa
na Musa na Eliya, wakizungumza naye,” Mt 17:3
“Petro akajibu
akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa
vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya,” Mt
17:4
“Alipokuwa katika
kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika
lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye;
msikieni yeye,” Mt 17:5
“Na wale wanafunzi
waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana,” Mt 17:6
“Yesu akaja, akawagusa,
akasema, Inukeni, wala msiogope,” Mt 17:7
“Wakainua macho yao,
wasione mtu ila Yesu peke yake,” Mt 17:8
“Na walipokuwa
wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya
maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu,” Mt 17:9
TAFAKARI:
“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anasheherekea Sikukuu ya kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Tukio hili la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linafunua Utukufu na Umungu
ya Yesu kabla na baada ya mateso na kifo chake kama sadaka iliyo hai na yenye
kumpendeza Mungu. Huu ni mpango wa Mungu tangu zamani ili kumkomboa mwanadamu
kutoka utumwa wa dhambi. Nabii Danieli alifunuliwa siri hii katika ndoto, na
leo inatimia ndani na katika Kristo. “Naye
akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote,
na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita
kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Tukio hili la
pekee la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linadhihirisha uwezo na mamlaka
aliyonayo.
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa upendo usio na kipimo, wakati ulipotimia, (Ebr 1:1-2),
katika historia hii ya wokovu, Mungu mwenyewe amejimwilisha na kukaa nasi. “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Hivyo
wapendwa katika Kristo, lnjili ya leo inauweka sawa ukweli huu kwa mambo makuu
matatu; Dira yetu ya kufuata kama Wakristo, Utimilifu wa nyakati, na Hatma yetu
iliyojengeka katika agano la umilele. Haya yote yanafanyika katika tukio hili
la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya simulizi la Injili ya leo.
Kwanza, ni dira yetu ya
kufuata kama Wakristo. Heshima na cheo chako kama Mkristo ni utakatifu wako.
Hivyo maisha yetu kama Wakristo kuelekea umilele yatafikika na kuwezekana kama
ni tokeo la utakatifu wetu kwa kuyaona maisha kama ni jukumu la muda fupi hapa
duniani na kama pia sehemu pekee ya maandalizi. Udhihirisho wa utakatifu huu
kama dira yetu ya maisha ni tendo lile la kung’ara Kristo Yesu. “Akageuka sura
yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru,”
Mt 17:2. Kristo anavikwa Utukufu wake ambao ataunyakua rasmi mara baada ya
mateso, kifo na ufufuko huko Yerusalemu. Hivyo Utukufu wa Kristo hautenganishwi
na msalaba/mateso. Kwa maana nyingine hakuna Utukufu pasipo msalaba. Kama
Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6, nasi wafuasi wake itatupasa kupita
njia hiyo ya msalaba, ukweli huu anaotufundisha, ili tuufikie uzima ule, yaani
maisha ya milele. Kristo ni masiha ya Msalaba, nasi twamfuata Masiha wa Msalaba
ili tuifikie taji ile ya Utukufu baada ya kuhesabiwa haki.
Pili, ni ukamilifu wa
nyakati. Katika tendo hili la kung’ara, tunaelezwa tokeo la watu wawili, yaani
Musa na Eliya katika mazungumzano na Yesu. ““Na tazama, wakatokewa
na Musa na Eliya, wakizungumza naye,” Mt 17:3. Katika tendo hili, Musa
anawakilisha Torati, na Eliya Unabii. Hivyo leo Yesu anaikamilisha Torati na
Unabii. Naye Yesu anatuambia, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja
kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na
nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata
yote yatimie,” Mt 5:17-18. Torati inatimilizwa kwa amri ya upendo kwa Mungu na
jirani. “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni
vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Ni ndani na katika
Kristo tu tunapata neema na kweli kwa mkono wake. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa
mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Na
huku ndiko kutimilika kwa sheria na kutamalaki kwa upendo, kweli, na neema.
Leo pia unabii wote
ulionenwa juu ya Kristo na historia nzima ya wokovu wetu unakamilika. Unabii huu
unafika ukomo wake kwa uwepo wa Kristo ambaye ni UPENDO WA MUNGU kwetu. Mtume
Paulo anasema, “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo
unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,”
1Kor 13:8. Huyu ndiye Kristo Yesu! Kung’ara kwake Bwana wetu Yesu Kristo
kulikoonyesha Ufukufu wake, kunaamsha furaha ya ndani ya Mtume Petro na
kuyasema ya moyoni mwake. “Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi
kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na
kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya,” Mt 17:4. Hata hivyo hilo halikuwa kusudi
la Yesu kubaki mlimani pale. Yesu inabidi ashuke na kuukumbatia Msalaba kama
alama ya ushindi na hapo ndipo wokovu
wako na wangu ulipotundikwa. Hii ndiyo safari kuelekea kilele kile cha wokovu
kama Masiha wa Msalaba.
Tatu, ni hatma yetu
iliyojengeka katika agano la milele. Kristo ndiye kielelezo chetu na wokovu
wetu. Leo Mungu Baba anauweka ukweli huu hadharani na kusema, “Huyu ni
Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5. Hili
ndilo agano la milele kati yetu na Mungu, na Kristo akiwa ndiye daraja na
mlango halisi wa sisi kupitia kwani ni kwake tu tutakuwa salama kama njia, ni
kwa Kristo tu tunalishwa kweli katika kweli, na Kristo tu ndiye uzima halisi.
Hivyo hapana tena ufunuo ulio wa wazi na kamili zaidi ya ufunuo huu wa Mungu
kupitia mwanaye Mpenzi. Tendo hili linathibitishwa na sauti ya Mungu mwenyewe
kwa viumbe vyote, Mt 17:5. Ndugu yangu, Je, unafuata sauti gani katika maisha
yako? Sauti hii kutoka mbinguni inampa Yesu Kristo Heshima, Mamlaka, na Utukufu.
“Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa
sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye,” 2Pet 1:17. Nasi tunapoisikia sauti hiyo na kuishi kweli
hiyo, twajazwa nguvu, heshima na utukufu kwa kuishi ndani na katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, zipo sauti nyingi katika
maisha yetu. Je, sauti hizo zinatupeleka karibu na Kristo Yesu au
zinatutenganisha na ukweli wake? Kusikia sauti hii ni kuyafanya mapenzi yake.
Na kufanya mapenzi yake maana yake ni tuyafanye kila mmoja kadiri ya wito wake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake,”
Mt 17:8
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie neema ya kuyafanya mapenzi yako. Amina