SIKUKUU YA UBATIZO WA BWANA-B
Somo
I: Isa 42:1-4, 6-7
Zab:
29:1-2, 3-4, 3, 9-10
1. Mpeni
Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu; Mpeni Bwana utukufu wa
jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa
amani.
2. Sauti
ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji
mengi. Sauti ya Bwana ina nguvu; Sauti ya Bwana ina adhama. (K)
3. Sauti
ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji
mengi. (K)
4. Sauti
ya Bwana yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake
Wanasema wote, Utukufu. Bwana aliketi juu ya Gharika; Naam, Bwana ameketi hali
ya mfalme milele. (K)
Somo
II: Mdo 10:34-38
Injili:
Mk 1:7-11
Nukuu:
“Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye;
mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake;
naye atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1
“Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi
utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli,” Isa 42:3
“Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami
nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya
mataifa,” Isa 42:6
“kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa,
kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:7
“Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika
natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali
katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35
“habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa
Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na
kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo
10:38
“Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho
Mtakatifu,” Mk 1:8
“Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka,
na Roho, kama hua, akishuka juu yake,” Mk 1:10
“na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa
wangu; nimependezwa nawe,” Mk 1:11
TAFAKARI:
“Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa
wangu; nimependezwa nawe.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo kwa furaha kubwa Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana.
Swali ambalo hutujia hata kama hatutaki ni hili: Je, Yesu alihitaji kubatizwa?
Jibu ni ndiyo na hapana! “Ndiyo” ya ubatizo wa Yesu imelenga katika
“kielelezo,” “Mfano wa kufuata,” yaani kupitia mfano huo tunao uthibitisho
pasipo shaka wa maneno haya Yesu, kwamba, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Mamlaka ya Maneno haya ya Yesu (Mimi ndimi njia,
na kweli, na uzima) yanawekwa wazi na nafsi ya tatu na ya kwanza ya Mungu mwenyewe
pale Mbingu zilipofunguka, Roho Mtakatifu akashuka kama kiwiliwili, na sauti
kutoka mbinguni ikasikika, “…Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa
nawe,” Mk 1:11
Ubatizo aliokuwa anaufanya Yohane Mbatizaji ulikuwa ubatizo
wa maji kama ishara ya toba ya kweli ikiwa ndiyo, maandalizi ya ubatizo wenyewe
wa Roho Mtakatifu na Moto. Yohane Mbatizaji anaweka jambo hili wazi kwa kusema,
“Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi,
ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa
Roho Mtakatifu na kwa moto,” Lk 3:16. Je, ubatizo wa Yohane Mbatizaji ulikuwa
ni kupoteza muda? La hasha! Kwa neno “maandalizi,” linabeba dhana nzima ya
uwepo wetu hapa duniani. Mahali hapa siyo sehemu ya kudumu, bali tunapita
kuelekea umilele. Hivyo kuufikia umilele ambao sasa unawezekana ndani na katika
Kristo, maandalizi ni muhimu ikiwa ni pamoja na kuishi katika hali ya neema.
Huku ndiko kufanya toba ya kweli kama ilivyo ubatizo ule wa maji ambao ulikuwa
ni kuwaandaa watu katika kweli na haki ambayo ukamilifu wake upo kwa Kristo
mwenyewe. Lengo la toba ni ondoleo la dhambi. Hivyo, “Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba
liletalo ondoleo la dhambi,” Mk 1:4
Wapendwa
wana wa Mungu, ahadi za Mungu kwetu zinatufikia pale tunapofanya toba ya kweli
na majuto. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani
kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote
wafikilie toba,” 1Pet 3:9. Mungu leo ametimiza ahadi yake kwa uvumilivu wa watu
wake kwa kazi iliyofanywa na Yohane Mbatizaji. Kristo Yesu ndiye kielezo halisi
cha Ubatizo wa Roho Mtakafu na Moto. Hizi ndizo “habari
za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu
naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38. Wewe ndiwe Mwanangu,
mpendwa wangu; nimependezwa nawe!
Tangu sasa neema-baraka, na kweli zimefunguliwa kwa watu
wote, Yoh 1:17. Mlango huu umefunguliwa hata kwa wale walioonekana ni wapagani
kwa njia ya maono ya Petro alipokuwa akisali na mbingu zikafunguka, na chombo
kikashuka kama nguo kubwa, wakiwemo aina zote za wanyama wenye miguu minne,
watambaao, na ndege wa angani, Mdo 10:11-12. Kadiri ya maono haya Petro alisita
kupokea maagizo ya Mungu kwa sababu ndani yake walikuwepo wanyama wale
waliokatazwa kuliwa nao ni najisi, Mdo 10:14. “Pamoja
na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio
na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini
hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na
sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni
mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao;
hao ni najisi kwenu,” Law 11:4-8.
Wapagani
hawakuchangamana na Wayahudi, na mbaya kazaidi Wayahudi wale ambao kwa namna ya
pekee ndio waliokuwa Kanisa la Mwanzo. Hizi ni changamoto ambazo zitapelekea
kuwepo kwa Mkutano/Mtaguso huko Yerusalemu, Mdo 15:1-41. Kuchangamana kwao ni
najisi kama ilivyokuwa kula nyama za wanyama hawa au kugusa mizoga yake. Badala yake “sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Sauti ikamjia mara ya pili,
ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi,” Mdo 10:13,
15. Neno “Ondoka uchinje ule,” linatupa uthibitisho wa kufunguliwa neema na
baraka kwa watu wote wenye hofu ya Mungu. Tendo hili linathibitishwa na Petro
mwenyewe huko Kaisaria kwa ujumbe uliotumwa kwake na Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na
sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, Mdo 10:22. Mtume Petro kwa kuona tendo
hili kubwa likitokea hata kwa wapagani kushukiwa na Roho Mtakatifu, anatoa
hitimisho la Imani na kusema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda
haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35.
Hivyo kumcha Mungu na kutenda haki ndicho kibali
chakukubaliwa na Mungu. Kibali hiki ndicho kielelezo cha utakatifu wako. Na
utakatifu huu ndio cheo chako mbele ya Mungu licha ya utofauti wa rangi zetu,
familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na utaifa wetu. Haya yote yaliyo ya
kibinadamu bila utakatifu wa Mungu katika kumcha na kutenda haki hayana fadhila
yoyote mbele za Muumba wetu.
Kwa maana hiyo, ubatizo wa Bwana leo ni kielelezo na mfano
wa hayo yote niliyoyasema. Kwa maneno mengine Yesu kama Yesu hakuhitaji ubatizo
huo katika maana ya ubatizo wa toba liletalo
ondoleo la dhambi, Mk 1:4. Na huu ndio ule utabiri aliousema Nabii Isaya kwa
mtumishi yule atakayepewa Mamlaka na Mungu juu ya watu wake waliomridhia. “Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu,
ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye
atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1. Mamlaka yake ni pamoja na kutoa hukumu ya
haki na kweli. “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na
kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6. Je,
ujio wa Mjumbe huyu wa Mungu ni mabadiliko ya kila kitu ambacho kilikuwa hapo
mwanzo? La hasha! “Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi
hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli,” Isa 42:3.
Je, Mjumbe huyu wa Mungu atafanya nini basi kwa hali yetu ya
kila siku? Kuhusu ukweli wa jambo hili, Yesu akiwa ndiye Mjumbe halisi wa
Mungu, (Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu;
nimependezwa nawe) mwenyewe
anasema hivi, “Msidhani
ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali
kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia,
Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka
,hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Ndugu yangu, amri za Mungu ni zile zile na
mafundisho ya Kristo ni yale yale yanayotuongoza kumjua Mungu, kumpenda Mungu,
kumtumikia Mungu, na Mwisho turudi kwake Mbinguni. Mimi na wewe yatupasa kuwa
waaminifu kwa amri hizi na kuziishi ikiwa ni pamoja na mafundisho tunayopewa
kila siku. Hii ndiyo maana ya kutimiliza torati. Wayahudi wakati wa Yesu
hawakuwa waaminifu kuhusu Torati. Badala yake waliitafsi ili ikidhi mahitaji na
malengo yao. Waliishi tafsiri hii-TALMUD, kama ukweli wa Mungu uliopotoshwa.
Yesu anawarudisha kwa mizizi la sheria ya Mungu, yaani Torati itimizwe kama
yalivyokuwa makusudi ya Mungu na siyo ya mwanadamu.
Kazi
hii ya Yesu ni kuweka wazi yale yote yaliyo gizani, na kuwaweka watu wote huru.
Na haya ndiyo yaliyotabiriwa na Nabii Isaya juu wa Mtumishi huyu wa Mungu
kwamba, “kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa
gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,”
Isa 42:7. Maneno haya ya Nabii Isaya yanarudiwa na Yesu mwenyewe alipoianza
kazi yake rasmi ya kupambana na giza ili sote kutuweka huru. Naye Yesu anasema,
“Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri
maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na
vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,”
Lk 4:18-19. Ndugu yangu niliye safiri nawe katika tafakari hii, leo tunapofanya
Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, ni wakati wa kukumbuka maneno haya ya Yesu
unapoutazama ubatizo wako wenyewe. Kwa ubatizo wako haya aliyoyasema Yesu
yametimia ndani ya moyo wako. “Leo Maandiko
haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21b. Ndugu yangu wauthamini ubatizo wako?
Marieta ni mwanafunzi wa dini ambaye mara baada ya mafundisho
yake alibahatika kupata Sakramenti tatu kwa wakati mmoja, yaani, Sakramenti ya
ubatizo, Kimpaimara/kuimarishwa, na Ekaristi Takatifu. Kwa Sakramenti ya
ubatizo alipakwa Mafuta Matakatifu utosini na kifuani. Na kwa Sakramenti ya
Kipaimara alipakwa mafuta Matakatifu ya Krisma kwenye paji la uso. Na baadaye
alipokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.
Baada ya tukio hili, Marieta hakuonekana tena Kanisani.
Sakramenti hizi za mkupuo zilikuwa ndiyo tiketi ya ‘bye bye.’ Marieta
alijichanganya sana na malimwengu na kwa waganga wa kienyeji ndiko kulikokuwa
hija yake. Waganga hawa walimtengeneza kweli kweli. Alipewa chale utosini, paja
la uso, kifuani na kiunoni kama mkanda wa risasi wa Rombo mcheza filamu.
Lakini pamoja na kinga hii kama alivyoambiwa na magwiji
hawa, Marieta hakuacha kuweweseka na kupandisha maruhani kila mara. Marafiki
zake walimshauri awe anakwenda Kanisani kusali. Hata hivyo maruhani hawa humwangusha
chini na kugaagaa hasa wakati wa kufukiza ubani na Mageuzo. Je, tatizo lipo
wapi?
Ndugu yangu, wewe uliyebatizwa umeingia mkataba na Mungu na
kuwa kiungo cha Kristo. Unapousaliti ubatizo wako kwa kwenda kwa waganga wa
kienyeji, na kupigwa chale sehemu zile ulizopakwa Mafuta Matakatifu ya Krisma
unausaliti ubatizo wako na kujiweka wakfu kwa shetani. Kwa tendo hili unakosa
kinga kwani hata malaika mlinzi wako anaondoka kwa sababu mwili wako kama
hekalu la Roho Mtakatatifu ni chafu, 1Kor 6:19. Hivyo utembeapo njiani mwili
wako unakuwa kama mnara wa simu, yaani, “network” ni “full.” Pepo yeyote
anayerandaranda lazima akuingie kwa sababu huna kinga tena, 1Pet 5:8. Haya
ndiyo mateso ya wengi leo.
Ponya yako katika tatizo hili lazima ufanye ukiri wa toba
ya kweli, na kuziungama dhambi zako ili upate uponyaji ndani yako. Kiti cha
huruma ya Mungu kipo muda wote. Ni wewe tu!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti
yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba,
vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, na unayenipenda upeo, asante kwa neema na baraka zako zisizo na
ukomo. Amina.