sábado, 6 de enero de 2018

TAFAKARI: SIKUKUU YA UBATIZO WA BWANA MWAKA-B


SIKUKUU YA UBATIZO WA BWANA-B

Somo I: Isa 42:1-4, 6-7

Zab: 29:1-2, 3-4, 3, 9-10

1.     Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu; Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.

(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

2.     Sauti ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji mengi. Sauti ya Bwana ina nguvu; Sauti ya Bwana ina adhama. (K)

3.     Sauti ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji mengi. (K)

4.     Sauti ya Bwana yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu. Bwana aliketi juu ya Gharika; Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)

Somo II: Mdo 10:34-38

Injili: Mk 1:7-11

Nukuu:

Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1

Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli,” Isa 42:3

Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6

“kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:7

Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35

“habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38

“Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu,” Mk 1:8

“Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake,” Mk 1:10

“na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Mk 1:11

TAFAKARI:Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa furaha kubwa Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana. Swali ambalo hutujia hata kama hatutaki ni hili: Je, Yesu alihitaji kubatizwa? Jibu ni ndiyo na hapana! “Ndiyo” ya ubatizo wa Yesu imelenga katika “kielelezo,” “Mfano wa kufuata,” yaani kupitia mfano huo tunao uthibitisho pasipo shaka wa maneno haya Yesu, kwamba, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Mamlaka ya Maneno haya ya Yesu (Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima) yanawekwa wazi na nafsi ya tatu na ya kwanza ya Mungu mwenyewe pale Mbingu zilipofunguka, Roho Mtakatifu akashuka kama kiwiliwili, na sauti kutoka mbinguni ikasikika, “…Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Mk 1:11

Ubatizo aliokuwa anaufanya Yohane Mbatizaji ulikuwa ubatizo wa maji kama ishara ya toba ya kweli ikiwa ndiyo, maandalizi ya ubatizo wenyewe wa Roho Mtakatifu na Moto. Yohane Mbatizaji anaweka jambo hili wazi kwa kusema, “Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Lk 3:16. Je, ubatizo wa Yohane Mbatizaji ulikuwa ni kupoteza muda? La hasha! Kwa neno “maandalizi,” linabeba dhana nzima ya uwepo wetu hapa duniani. Mahali hapa siyo sehemu ya kudumu, bali tunapita kuelekea umilele. Hivyo kuufikia umilele ambao sasa unawezekana ndani na katika Kristo, maandalizi ni muhimu ikiwa ni pamoja na kuishi katika hali ya neema. Huku ndiko kufanya toba ya kweli kama ilivyo ubatizo ule wa maji ambao ulikuwa ni kuwaandaa watu katika kweli na haki ambayo ukamilifu wake upo kwa Kristo mwenyewe. Lengo la toba ni ondoleo la dhambi. Hivyo, “Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,” Mk 1:4

Wapendwa wana wa Mungu, ahadi za Mungu kwetu zinatufikia pale tunapofanya toba ya kweli na majuto. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba,” 1Pet 3:9. Mungu leo ametimiza ahadi yake kwa uvumilivu wa watu wake kwa kazi iliyofanywa na Yohane Mbatizaji. Kristo Yesu ndiye kielezo halisi cha Ubatizo wa Roho Mtakafu na Moto. Hizi ndizo “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38. Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe!

Tangu sasa neema-baraka, na kweli zimefunguliwa kwa watu wote, Yoh 1:17. Mlango huu umefunguliwa hata kwa wale walioonekana ni wapagani kwa njia ya maono ya Petro alipokuwa akisali na mbingu zikafunguka, na chombo kikashuka kama nguo kubwa, wakiwemo aina zote za wanyama wenye miguu minne, watambaao, na ndege wa angani, Mdo 10:11-12. Kadiri ya maono haya Petro alisita kupokea maagizo ya Mungu kwa sababu ndani yake walikuwepo wanyama wale waliokatazwa kuliwa nao ni najisi, Mdo 10:14. “Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu,” Law 11:4-8.

Wapagani hawakuchangamana na Wayahudi, na mbaya kazaidi Wayahudi wale ambao kwa namna ya pekee ndio waliokuwa Kanisa la Mwanzo. Hizi ni changamoto ambazo zitapelekea kuwepo kwa Mkutano/Mtaguso huko Yerusalemu, Mdo 15:1-41. Kuchangamana kwao ni najisi kama ilivyokuwa kula nyama za wanyama hawa au kugusa mizoga yake. Badala yake “sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi,” Mdo 10:13, 15. Neno “Ondoka uchinje ule,” linatupa uthibitisho wa kufunguliwa neema na baraka kwa watu wote wenye hofu ya Mungu. Tendo hili linathibitishwa na Petro mwenyewe huko Kaisaria kwa ujumbe uliotumwa kwake na Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, Mdo 10:22. Mtume Petro kwa kuona tendo hili kubwa likitokea hata kwa wapagani kushukiwa na Roho Mtakatifu, anatoa hitimisho la Imani na kusema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35.

Hivyo kumcha Mungu na kutenda haki ndicho kibali chakukubaliwa na Mungu. Kibali hiki ndicho kielelezo cha utakatifu wako. Na utakatifu huu ndio cheo chako mbele ya Mungu licha ya utofauti wa rangi zetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na utaifa wetu. Haya yote yaliyo ya kibinadamu bila utakatifu wa Mungu katika kumcha na kutenda haki hayana fadhila yoyote mbele za Muumba wetu.

Kwa maana hiyo, ubatizo wa Bwana leo ni kielelezo na mfano wa hayo yote niliyoyasema. Kwa maneno mengine Yesu kama Yesu hakuhitaji ubatizo huo katika maana ya ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, Mk 1:4. Na huu ndio ule utabiri aliousema Nabii Isaya kwa mtumishi yule atakayepewa Mamlaka na Mungu juu ya watu wake waliomridhia. “Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1. Mamlaka yake ni pamoja na kutoa hukumu ya haki na kweli. “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6. Je, ujio wa Mjumbe huyu wa Mungu ni mabadiliko ya kila kitu ambacho kilikuwa hapo mwanzo? La hasha! Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli,” Isa 42:3.

Je, Mjumbe huyu wa Mungu atafanya nini basi kwa hali yetu ya kila siku? Kuhusu ukweli wa jambo hili, Yesu akiwa ndiye Mjumbe halisi wa Mungu, (Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe) mwenyewe anasema hivi, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Ndugu yangu, amri za Mungu ni zile zile na mafundisho ya Kristo ni yale yale yanayotuongoza kumjua Mungu, kumpenda Mungu, kumtumikia Mungu, na Mwisho turudi kwake Mbinguni. Mimi na wewe yatupasa kuwa waaminifu kwa amri hizi na kuziishi ikiwa ni pamoja na mafundisho tunayopewa kila siku. Hii ndiyo maana ya kutimiliza torati. Wayahudi wakati wa Yesu hawakuwa waaminifu kuhusu Torati. Badala yake waliitafsi ili ikidhi mahitaji na malengo yao. Waliishi tafsiri hii-TALMUD, kama ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Yesu anawarudisha kwa mizizi la sheria ya Mungu, yaani Torati itimizwe kama yalivyokuwa makusudi ya Mungu na siyo ya mwanadamu.

Kazi hii ya Yesu ni kuweka wazi yale yote yaliyo gizani, na kuwaweka watu wote huru. Na haya ndiyo yaliyotabiriwa na Nabii Isaya juu wa Mtumishi huyu wa Mungu kwamba, “kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:7. Maneno haya ya Nabii Isaya yanarudiwa na Yesu mwenyewe alipoianza kazi yake rasmi ya kupambana na giza ili sote kutuweka huru. Naye Yesu anasema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Ndugu yangu niliye safiri nawe katika tafakari hii, leo tunapofanya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, ni wakati wa kukumbuka maneno haya ya Yesu unapoutazama ubatizo wako wenyewe. Kwa ubatizo wako haya aliyoyasema Yesu yametimia ndani ya moyo wako. “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21b. Ndugu yangu wauthamini ubatizo wako?

Marieta ni mwanafunzi wa dini ambaye mara baada ya mafundisho yake alibahatika kupata Sakramenti tatu kwa wakati mmoja, yaani, Sakramenti ya ubatizo, Kimpaimara/kuimarishwa, na Ekaristi Takatifu. Kwa Sakramenti ya ubatizo alipakwa Mafuta Matakatifu utosini na kifuani. Na kwa Sakramenti ya Kipaimara alipakwa mafuta Matakatifu ya Krisma kwenye paji la uso. Na baadaye alipokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Baada ya tukio hili, Marieta hakuonekana tena Kanisani. Sakramenti hizi za mkupuo zilikuwa ndiyo tiketi ya ‘bye bye.’ Marieta alijichanganya sana na malimwengu na kwa waganga wa kienyeji ndiko kulikokuwa hija yake. Waganga hawa walimtengeneza kweli kweli. Alipewa chale utosini, paja la uso, kifuani na kiunoni kama mkanda wa risasi wa Rombo mcheza filamu.

Lakini pamoja na kinga hii kama alivyoambiwa na magwiji hawa, Marieta hakuacha kuweweseka na kupandisha maruhani kila mara. Marafiki zake walimshauri awe anakwenda Kanisani kusali. Hata hivyo maruhani hawa humwangusha chini na kugaagaa hasa wakati wa kufukiza ubani na Mageuzo. Je, tatizo lipo wapi?

Ndugu yangu, wewe uliyebatizwa umeingia mkataba na Mungu na kuwa kiungo cha Kristo. Unapousaliti ubatizo wako kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji, na kupigwa chale sehemu zile ulizopakwa Mafuta Matakatifu ya Krisma unausaliti ubatizo wako na kujiweka wakfu kwa shetani. Kwa tendo hili unakosa kinga kwani hata malaika mlinzi wako anaondoka kwa sababu mwili wako kama hekalu la Roho Mtakatatifu ni chafu, 1Kor 6:19. Hivyo utembeapo njiani mwili wako unakuwa kama mnara wa simu, yaani, “network” ni “full.” Pepo yeyote anayerandaranda lazima akuingie kwa sababu huna kinga tena, 1Pet 5:8. Haya ndiyo mateso ya wengi leo.

Ponya yako katika tatizo hili lazima ufanye ukiri wa toba ya kweli, na kuziungama dhambi zako ili upate uponyaji ndani yako. Kiti cha huruma ya Mungu kipo muda wote. Ni wewe tu!

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4

Tusali:-Ee Yesu Mwema, na unayenipenda upeo, asante kwa neema na baraka zako zisizo na ukomo. Amina.

TAFAKARI: SIKUKUU YA EPIFANIA, TOLEO LA BWANA


SIKUKUU YA EPIFANIA, TOLEO LA BWANA

JUMAPILI, JANUARI 7

Somo I: Isa 60:1-6

Zab: 72: 1-2, 7-8, 10-11, 12-13

1.     Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, Na mwana wa mfalme haki yako. Atawaamua watu wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

(K) Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie.

2.     Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia. K)

3.     Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa. Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie. (K)

4.     Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

Somo II: Efe 3:2-3a, 5-6

Injili: Mt 2:1-12

Nukuu:

Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia,” Isa 60:1 

Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako,” Isa 60:3

“Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia,” Isa 60:5

ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri,” Efe 3:2-3a

Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6

“Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia,” Mt 2:1-2 

Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3

“Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8

“Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane,” Mt 2:11

Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine,” Mt 2:12

TAFAKARI:Mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Epifania, yaani, Toleo la Bwana. Leo Mama Kanisa anatukumbusha mambo makuu matatu muhimu. Kwanza, toleo la Bwana ni ufunuo na udhihirisho wa Kristo katika ulimwengu. Ni ufunuo wa Kristo kwa Mataifa yote ya ulimwengu ambapo kunajidhihirisha kwa wataalamu wa nyota-Mamajusi, wakiongozwa na nyota ile ya ajabu. “Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako,” Isa 60:3. Wokovu wa Yesu Kristo unajionyesha kama nuru au mwanga wa alfajiri unaoliondoa jiza na uvuli wa mauti ambao unautawala ulimwengu. Mungu mwenyewe ndiye pambazuko.

Siku ya leo inadhihirika wazi machoni mwa wanadamu kwamba Kristo ndiye Mfalme wa ulimwengu wote, kwa ajili ya watu wote, na mmiliki wa utajiri wote. “Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia,” Isa 60:5. Ukweli huu unajifunua kwa tunu zile alizopewa mtoto Yesu. “Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane,” Mt 2:11.

Toleo hili la Bwana la dhihirisha ukuhani wa Kristo kwa tunu ile ya uvumba. Huyu ndiye kwa huduma yake atavitakatifuza vyote katika ulimwengu huu na kuvikomboa. Tendo hili linakwenda sambamba na sadaka ile atakayo itoa pale Msalabani. Tendo hili la upendo mkubwa wa Mungu kwa wanadamu, leo linajifunua kwa tunu hii ya manemane. Manemane yanatabiri kifo chake kama ilivyo taratibu za Wayahudi kuhifadhi Maiti na kuzika. “Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika,” Yoh 19:39-40. Mambo haya makuu matatu yanajifunua kwetu leo.

Pili, toleo hili la Bwana, Epifania, linatupa namna ya kuishi kama Wakristo-wafuasi wa Kristo. Tendo hili ya kufunuliwa na kudhihishwa kwa Kristo ulimwenguni pote linatuondoa katika hali ile ya kuwa “wakristo wa kidunia” na kutufanya Wakristo wa ulimwengu-wamishionari. Leo tunafanywa Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote na siyo Mkristo wa kidunia. Wakristo wa kidunia kadiri ya Rich Warren, humtazama Mungu kwanza kwa ajili ya kukidhi haja zao binafsi. Wanapenda kuhudhuria mikutano na semina za kujenga, lakini hutawakuta katika mkutano wa umisheni kwa sababu hawaupendelei. Maombi yao yanajali mahitaji yao binafsi, baraka, na furaha yao. Ni ile imani ya ‘mimi kwanza.’ Waaminiwa mtindo huu husukumwa mara zote na swali hili: Je, Mungu anawezaje kufanya maisha yangu kuwa na furaha? Wanapenda kumtumia Mungu kwa malengo yao badala ya wao kutumiwa kwa malengo yake (Mungu).

Wapendwa wana wa Mungu, kinyume cha hapo, Wakristo wa tabaka la ulimwengu mzima wanajua waliokolewa ili watumike na kutayarishwa kwa ajili ya utume. Wako tayari kupokea jukumu la mtu binafsi na wanafurahia upendeleo huo wa kutumiwa na Mungu. Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote ndio watu pekee walio hai kikamilifu katika sayari hii. Furaha yao, uhakika na hamasa yao vinaambukiza kwa sababu wanajua wanafanya tofauti. Wanaamka asubuhi wakitazamia Mungu kufanya kazi kuwapita katika njia mpya. Je, unataka kuwa Mkristo wa aina gani? Leo katika toleo la Bwana, Mungu anakualika kushiriki katika tendo kubwa kuliko yote, la aina yake na la muhimu sana katika historia-ufalme wake. Hivi ndivyo Yesu alivyowaambia wanafunzi wake kabla ya kapaa, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari,” Mt 28:18-20. Tendo hili linamfanya Kristo kuendelea kudhihirika ulimwenguni kote.

Tatu, toleo hili la Bwana leo linatukumbusha kwamba uinjilishaji hapa duniani ni jambo la pekee. Yapo malengo matano ya Mungu kwa maisha yako hapa duniani. Mungu alikuumba ili uwe mshiriki katika jamii yake, kielelezo cha tabia yake, mtu anayetukuza utukufu wake, mtumishi wa neema yake, na mjumbe wa Habari zake Njema. Katika malengo haya matano, hii la tano linaweza tu kutendwa hapa duniani. Yale mengine manne utaendelea kuyafanya milele kwa namna fulani. Hivyo kutangaza Habari Njema ni muhimu sana; una muda mfupi tu wa kushirikisha wengine ujumbe wa maisha yako na kutimiza utume wako.

Ujumbe wa Mtume Paulo kwa watu wa mataifa anaonyesha mpango wa wokovu wa Mungu umejifunua wazi kwa Watakatifu, Mitume wake na Manabii. Hata hivyo watu hawa wa mataifa wameupokea wokovu wa Mungu kwa ufunuo wa Roho. Watu hawa wa Mataifa ni warithi pia wa ahadi hizi za Mungu. Katika mpango huu wa wokovu hakuna tena matabaka. Hii ndiyo siri kubwa inayoibuliwa leo kwa tendo hili la toleo la Bwana. “Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6. Sote tu huru ndani na katika Kristo Yesu.

Hivyo tuna mwili mmoja tu wa Kristo, nalo ndilo Kanisa. Sote tu viungo vya mwili huo mmoja na Kanisa hilo moja, yaani Kanisa la Kristo. Kwa utarajibu na mwono huu, sote tunashiriki fumbo la Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo. Kristo katika mtazamo huu ndiye mrithi wa kweli wa ahadi zile za Mungu. “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo,” Gal 3:16

Yesu Kristo Mfalme na Masiha kwa mara ya kwanza anakutana na wana wa ulimwengu wote. Injili ya Matayo inatajirisha simulizi la toleo la Bwana kwa vielelezo vya Kibiblia-Maandiko Matakatifu. Unabii ule wa Nabii Mika unatimia, yaani; (nyota Yakobo, zawadi za dhahabu na uvumba). Kristo ndiye Mfalme Mpya wa Wayahudi, na Musa mpya, mwakilishi wa ulimwengu mzima. Tendo hili la toleo la Bwana ni tishio kwa falme nyingine za ulimwengu huu. “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3. Habari za ufalme huu mpya ni habari njema kwa masikini na wenye hofu ya Mungu. Wale wote wasio na hofu ya Mungu huongozwa na mipango miovu ya shetani. Mungu hata hivyo uiweka mipango yao miovu wazi kwa ajili ya kuwanusuru wanyonge na waadilifu wake. “Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine,” Mt 2:12. Huyu ndiye Mungu asiyeshindwa katika mipango yake kwa wapendwa wake. Na huyu ndiye tunayesujudia leo siku ya Epifania, toleo la Bwana.

Je, ungepata leo nafasi ya kumtolea Yesu tunu ungempa kitu gani? Mathias Makyadi kutoka Kongo alikuwa ni mmoja wa wanovisi (wanafunzi wa hatua muhimu sana katika maisha ya kitawa) kati ya wanovisi kumi wa shirika fulani la kimisionari. Kila wiki mmoja wa wanovisi hupewa muda wa saa moja kutafakari mbele ya Ekaristi Takatifu. Waweza kutumia muziki wa ala ukuongoze katika tafakuri yako au ukimya tulivu.

Tendo la kufanya tafakuri lilikuwa gumu sana kwa Mathias Makyadi. Hivyo ilipofika zamu yake ulikuwa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo Mathias alimwambia Yesu wa Ekaristi hivi, “kutafakari kwa ukimya kadiri ya utaratibu uliozoeleka hapa mimi siwezi. Hivyo naomba nikupe kile nilichonacho kama shukrani na upendo wangu kwako.” Mathias aliondoka na kwenda chumbani mwake akachukua redio kaseti yake na kuweka mziki wa kwao “ndombolo” na kucheza kwa nguvu zake sote, kwa kutumia akili yake yote, na moyo wake wote.

Mara aliingia Mlezi wake kwenye kile kikanisa  kwani kelele zile zilisikika kila viambata vya nyumba ile ya Unovisi. “Kwa nini unafanya kelele mahali hapa na kucheza mbele ya Yesu wa Ekaristi?” Mlezi wa wanovisi alisema kwa jazba na hasira. “Baba, hiki ndicho ninachoweza kumpa Yesu wa Ekaristi kilicho cha thamani kubwa na ninachoweza kumpa kwa moyo wangu wote,” Mathias amjibu Mlezi wake kwa upole. Baada ya kuyatafakari maneno yale ya Mathias, Mlezi wake aliondoka bila ya kusema neno.

Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu anacho kitu cha kumpa Yesu leo kama walivyofanya Mamajusi na alivyofanya Mathias. Lakini zaidi ya yote, mimi na wewe tunaweza kumpa dhambi zetu kwani ndiyo mali yetu halali. Huu ni mwito wa kufanya toba ya kweli na majuto pale tunapoutanguliza zaidi ubinadamu wetu. Tunapojitazama sisi na huruma ya Mungu, tutazame mali hii halali tuliyonayo. Kristo Mfalme, ni Huruma, Upendo, Msamaha, Haki, na Kweli. Zawadi hii ataibadilisha na kuwa nyeupe kama sufu. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi,” Ufu 19:14

Tusali: Ee Yesu, nijalie neema ya kutopoteza furaha yako ndani ya moyo wangu. Amina